Ameachika Talaka Tatu Bado Anampenda Mumewe Aolewe Na Kuachika Ili Warudiane?

 

SWALI:

Kwanza napenda kumshukuru Allaah kwa kunipa afya na uzima, na la pili napenda kukushukuruni nyote mloiandaa website hii inshAllaah Allaah atakupeni kheir nyingi hapa duniani na akhera ameen.

Napenda kuuliza kwamba mimi ni mwanamke nilieachwa talaka tatu na mume wangu hawezi tena kunirejea tena, hivyo imepita muda sasa na eda yangu imemaliza, kwa bahati nzuri nimepata mume anataka kunioa sasa, lakini mimi bado nampenda sana yule mume wangu wa mwanzo na amesema hata nikiachwa yeye yupo tayari kunioa, hivyo nikubali kuolewa na huyu mume mpya halafu nitake kuachwa kwa ajili ya kurejeana na mume wangu wa mwanzo, jee ndoa hii inasihi? Tafadhali naomba majibu kutoka kwenu (Wabillah tawfiq)

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo kuhusu talaka. Hatuelewi kabisa mume au mke anayesema ninapendana sana na mwenzangu lakini zikawa talaka zinatoka ya kwanza, ya pili. Baada ya kwamba ya pili imetoka wanandoa hao hawakuweza kutatua matatizo waliyonayo mpaka na ya tatu nayo ikatolewa! Je, kweli hapo kuna mapenzi? Tufahamu kuwa talaka ya tatu inapotolewa wanandoa hao wawili hawawezi kabisa kurudiana mpaka mke aolewe na mume mwengine wakutane kimwili, waachane kikawaida bila ya mkono mwingine kuingia kati. Kwa haya, Allaah Aliyetukuka Anatueleza:

Talaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa vizuri” (2: 229).

 

Aayah inayofuata tunaelezwa yafuatayo: “Na kama amempa talaka (ya tatu) basi si halali kwake baada ya hayo mpaka aolewe na mume mwengine. Na akiachwa basi hapana ubaya kwao kurejeana wakiona kuwa watashikamana na mipaka ya Allaah. Na hii ni mipaka ya Allaah Anayoibainisha kwa watu wanaojua” (2: 230).

Tufahamu kuwa si halali kwa mume kumtaka mwanamume mwingine amuoe mtalaka wake kisha amuache. Jambo hilo limelaaniwa kabisa katika sheria, na anayehalalisha na yule anayehalalishiwa wote wana laana ya Allaah Aliyetukuka.

Ama kauli yako ya kuwa ukubali kuolewa na mtu aliyekuja kukuposa kisha utake talaka haifai kabisa kwani kwa kufanya hivyo utakuwa umefanya makosa kadhaa. Mojawapo ni kuwa umemdanganya huyo mume mpya yeye akitarajia kuwa ni mkewe wa kudumu kumbe niya yako ni nyingine. Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametahadharisha: “Mwanamke yeyote atakayeomba talaka bila ya sababu yoyote ile hatasikia hata harufu ya Peponi” (Abu Daawuud kutoka kwa Thawbaan [Radhiya Allaahu ‘anhu]).

Ushauri wetu kwako ni kuwa usifanye hivyo bali ikiwa kweli unataka kuolewa na huyo anayekuposa, basi kuwa na niya na kuishi naye milele. Ikiwa itatokea kuwa mume huyo amekuacha basi mume wako akija kukuposa tena utatoa idhini ya yeye akuoe.

Pia inawabidi mjifunze umuhimu wa talaka na si kuichezea kama mlivyofanya kwani matokeo yake ndio haya mahangaiko mliyonayo.

Twakutakia kila la kheri na fanaka.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share