Kusuka Nywele Na Kuchanganya Na Nyuzi Inafaa?

 

Kusuka Nywele Na Kuchanganya Na Nyuzi Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Samahani kwa kuwasumbuwa kwanza natowa shukurani kwakutuonesha mtandao huyu kwa kweli unatupa elim mimi swali langu nikusu kama mtu amesuka nywele kachanga nauzi inaruusiwa kusali nazo ao kufunga nazo? Samahani kama nimeandika makosa naomba samahani ni  .............. kutoka Belgique wasalam

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakuna samahani dada yetu kwa kuuliza swali wala hakuna makosa yoyote yaliyopatikana katika ibara hiyo.

 

Katika mapambo ya kike yaliyokatazwa ni kuunga nywele zake kwa nywele nyingine, zikiwa ni za kweli (zake au za mwengine) au za bandia kama vile wigi au vipande vya kuongeza. Imepokewa na ‘Aaishah, dadake Asmaa’, Ibn ‘Umar, Ibn Mas‘uud na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kuwa:

 

"Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwenye kuunga nywele na mwenye kuungwa" [al-Bukhaariy].

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilitilia mkazo sana katika kupiga vita aina hii ya hadaa kufikia hadi kukataza yule zimtokaye nywele zake kwa sababu ya maradhi kuziunga kwa nywele nyingine hata akiwa ni biharusi anayepelekwa kwa mumewe [al-Bukhaariy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah].

 

Huku kuungwa kwa nywele kumeitwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni udanganyifu [al-Bukhaariy].

 

Kwa ufupi, kuunga nywele ni haramu zikiwa za kweli au za bandia nao ni udanganyifu uliokatazwa. Ama kuunga nywele kwa vitambara au nyuzi na vitu kama hivyo si katika vilivyoharamishwa kwani imepokewa na Sa‘iyd bin Jubayr kuwa: "Kutumia nyuzi za hariri au sufi katika kuunga mwanamke nywele zake – au kusukia mikia yake – si vibaya". Haya yamethibitishwa na Imaam Ahmad kuwa yanajuzu kwa kuwa vitu viwili hivyo havifanani. Wapo wanazuoni wenye muelekeo kuwa kuunganisha ni kuunganisha ikiwa ni kwa nyuzi, nywele zako au za mwingine, za kweli au za bandia ni sawa kabisa bila kutofautisha. Kwa hiyo, nasiha yetu kwa dada zetu ni afadhali muachane na kuunganisha nywele kwa chochote kiwacho.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share