Mwanamume Kuswali Fardhi Nyumbani Ikiwa Msikiti Uko Mbali

 

 

SWALI:

 

 Mwanamume anaruhusiwa kuswali fardh nyumbani ikiwa msikiti uko mbali.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Muislamu mwanamme anaruhusiwa kuswali nyumbani kukiwa na dharura zinazokubalika kisheria. Miongoni mwa sababu hizo ni ukosefu wa usalama, mvua, Msikiti kuwa mbali kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Haikalifishi nafsi isipokuwa kwa kitu kinachoweza bila taklifu yoyote ile.

Lakini inapasa kutambua kuwa Swalah ya Jamaa imewajibika kwa wanaume ila tu kama kuna dharura, hivyo Muislamu asitafute sababu ndogo ikamzuia kukosa Swalah za Jamaa.

Tufahamu kuwa hata katika vita Waislamu wameamrishwa waswali Jamaa japokuwa inabidi waswali nusu nusu yaani wabadilishane makundi katika Swalah yenyewe yaani nusu waswali nusu ya Swalah na nusu ya kundi likamilishe Rakaa nyinginezo:

 

((وَإِذَا كُنتَ فِيهِمْ فَأَقَمْتَ لَهُمُ الصَّلاَةَ فَلْتَقُمْ طَآئِفَةٌ مِّنْهُم مَّعَكَ وَلْيَأْخُذُواْ أَسْلِحَتَهُمْ فَإِذَا سَجَدُواْ فَلْيَكُونُواْ مِن وَرَآئِكُمْ وَلْتَأْتِ طَآئِفَةٌ أُخْرَى لَمْ يُصَلُّواْ فَلْيُصَلُّواْ مَعَكَ وَلْيَأْخُذُواْ حِذْرَهُمْ وَأَسْلِحَتَهُمْ وَدَّ الَّذِينَ كَفَرُواْ لَوْ تَغْفُلُونَ عَنْ أَسْلِحَتِكُمْ وَأَمْتِعَتِكُمْ فَيَمِيلُونَ عَلَيْكُم مَّيْلَةً وَاحِدَةً وَلاَ جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن كَانَ بِكُمْ أَذًى مِّن مَّطَرٍ أَوْ كُنتُم مَّرْضَى أَن تَضَعُواْ أَسْلِحَتَكُمْ وَخُذُواْ حِذْرَكُمْ إِنَّ اللّهَ أَعَدَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا))

 

((Na unapokuwa pamoja nao, ukawaswalisha, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao. Na watakapomaliza sijida zao, basi na waende nyuma yenu, na lije kundi jingine ambalo halijaswali, liswali pamoja nawe. Nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Waliokufuru wanapenda mghafilike na silaha zenu na vifaa vyenu ili wakuvamieni mvamio wa mara moja. Wala si vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkawa wagonjwa, mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika Allaah Amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha)) [An-Nisaa: 102]

 

Kwa jinsi ilivyo na umuhimu mkubwa Swalah ya Jamaa imefika hadi kuwa angeliweza kupewa amri Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuchoma moto nyumba za wale wasiokwenda kuswali Jamaa.

 

غن ابي  هريرة أنه صلى الله عليه وسلم:  ((وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَقَدْ هَمَمْتُ أَنْ آمُرَ بِحَطَبٍ فَيُحْطَبَ ثُمَّ آمُرَ بالصلاة فَيُؤَذَّنَ لَهَا ثُمَّ آمُرَ رجلا فَيَؤُمَّ النَّاسَ ثُمَّ أُخَالِفَ إِلَى رِجَالٍ فَأُحَرِّقَ عَلَيْهِمْ بُيُوتَهُمْ))  البخاري

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, nilikuwa nawaza kukusanywa kuni, kisha ningeliamrisha mtu aimamishe Swalah, kisha ningelikwenda nyuma na kuchoma nyumba za wanaume wasiohudhuria Swalah [ya Jamaa])) [al-Bukhaariy na Muslim] Ni lazima umbali wa msikiti uwe kiasi kikubwa na isiwe umbali mdogo tu ikawa sababu ya kumfanya Muislamu asiende msikitini kuswali Jamaa kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) hakumpa ruhusa kipofu alipotoa hoja kuwa hana wa kumuongoza kwenda msikitini. Bali alimuamrisha aende madamu anasikia adhaan.

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ قَالَ أَتَى النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَجُلٌ أَعْمَى [وهو ابن أم مكتوم] فَقَالَ : يَا رَسُولَ اللَّهِ، إِنَّهُ لَيْسَ لِي قَائِدٌ يَقُودُنِي إِلَى الْمَسْجِدِ فَسَأَلَ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ يُرَخِّصَ لَهُ فَيُصَلِّيَ فِي بَيْتِهِ ، فَرَخَّصَ لَهُ ، فَلَمَّا وَلَّى دَعَاهُ ، فَقَالَ : ((هَلْ تَسْمَعُ النِّدَاءَ بِالصَّلاةِ ؟)) قَالَ : نَعَمْ . قَالَ : ((فَأَجِبْ))   مسلم    

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesema: Alikuja mtu kipofu kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) aliyesema: Sina mtu wa kuniongoza msikitini. Akaulizwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amruhusu ili aswali nyumbani akamruhusu, kisha aliporudi alimuuliza: ((Je, unasikia adhaan ya Swalah?)) Akasema: Ndio. Akasema: ((Basi imewajibika kwako)) [Muslim]

Pia tutambue kuwa kuna fadhila kubwa kuswali Swalah ya Jamaa hivyo bila shaka Muislamu hatopenda kukosa hizo fadhila kama zifuatazo:

 

عن ابنِ عمَر رضي اللَّه عنهما أَنَّ رسولَ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال : ((صَلاةُ الجَمَاعَةِ أَفضَلُ مِنْ صَلاةِ الفَذِّ بِسَبْعٍ وَعِشْرِينَ درَجَةً )) متفقٌ عليه

Kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhiya Allahu 'anhumaa) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swalah ya Jamaa ni bora kuliko Swalah ya pekee kwa daraja ishirini na saba)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Ingia katika viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi kuhusu umuhimu wa Swalah ya Jamaa

Swalah Ya jamaa Inafaa Nyumbani?

Fadhila Na Umuhimu Wa Swalah Ya Jamaa

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share