Nguzo, Waajib Na Sunnah Katika Swalaah

 

 Nguzo Waajib Na Sunnah Katika Swalaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Ni vitendo gani katika Swalah ni Sunnah na vipi ni Fardhi? Nitashukuru mkinieleza kwa Salaa za rakaa mbili, tatu na nne.
 
Jazzakallahu Khayr

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Maelezo bayana kuhusu swali lako na tutaja   kuhusu yaliyo Sunnah katika Swalaah kwa sababu ni mengi ambayo yamegawanywa katika Sunnah za maneno (As-Sunnan Al-Qawliyyah) na Sunnah za vitendo (As-Sunnan Al-Fi'iliyyah) hadi baadhi ya ‘Ulamaa  wanasema hizo Sunnah zinazidi 50.

 

Nguzo za Swalaah ni 14. Nguzo ni zile ambazo ukiswali na ukaziacha kwa makusudi Swalaah yako inabatilika, na ikiwa umeacha kwa kusahau, Swalaah yako pia itakuwa haikukamilika hadi urejee kitendo chenyewe au urejee rakaa na kisha mwishoni utoe Sajdatus-Sahw (Sajdah ya kusahau). Lakini ukiwa umesahau nguzo ya Takbiyratul-Ihraam, basi Swalaah yako basi itakubidi uiswali Swalah upya tokea mwanzo.

 

 

Nguzo Za Swalaah:

 

 

1. Kusimama katika Swalaah za fardh kwa yule mwenye uwezo. (Wanachuoni wengine wamesema nguzo ya kwanza ni Niyyah kabla ya Kusimama). Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ﴿٢٣٨﴾

Na simameni mbele ya Allaah katika hali ya utiifu [Al-Baqarah: 238]

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Swali hali ya kuwa umesimama, ukitoweza kwa kukaa na ukitoweza basi kwa kulala ubavu" [al-Bukhaariy na Abuu Daawuwd].

 

 

2. Takbiyratul-Ihraam (Takbira ya kuhirimia) kwa tamko la “Allaahu Akbar” kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Ufunguo wa Swalaah ni kuzitwaharisha, na kuifunga ni Takbiyra, na kuifungua ni kutoa Salaam" [Abuu Daawuwd na at-Tirmidhiy].

 

 

3.  Kusoma Suwrah-Al-Faatihah katika kila rakaa. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hapana Swalaah kwa ambaye hakusoma Suwrah Al- Faatihah" [al-Bukhaariy].

  

4. Kurukuu.

  

5. Utulivu (Twumaaninah) katika Rukuu

  

6. I'itidaal (hapa inaingia na kunyanyuka kutoka katika Rukuu hadi anaponyooka mtu).

 

7.    Utulivu katika I'Itidaal.

 

8.  Kusujudu.

 

9.  Utulivu katika kusujudu. Kutulia wakati wa kurukuu, kusujudu, kusimama, kukaa baina ya sijdah mbili kwa kauli ya  Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Kisha rukuu mpaka utulizane hali ya kurukuu, kisha nyanyuka mpaka ulingane sawa hali ya kusimama, kisha sujudu mpaka utulizane na hali umesujudu, kisha nyanyuka mpaka utulizane hali ya kuwa umekaa" [al-Bukhaariy]

 

10.  Kikao baina ya Sijda mbili.

 

11. Utulivu katika kikao baina ya Sijda mbili.

 

12.  Tashahhud ya mwisho.

 

13.  Kikao katika Tashahhud ya mwisho.

 

14.   Salaam (Kutoa Salaam) ya kwanza.

 

 

Utahakikisha unafuatanisha yote hayo kama utaratibu ulivyopangika.

 

 

Waajib Za Swalaah:

 

Ni lile ambalo ni wajibu kulifanya au kusema, inaondoka kwa kusahau na kulazimisha mwenye kuswali kusujudu sijdah mbili za kusahau. Yeyote mwenye kuacha kwa kusudi Swalaah yake inabatilika ikiwa anajua uwajibu wake.

Istwilahi hii inatumika kwa madhehebu ya Hanafi na Hanbali ila ma-Hanafi hawaoni kuwa mwenye kuacha wajibu kwa kusudi inabatilisha Swalaah yake bali yeye amefanya madhambi anayostahiki adhabu. Ama ma-Maaliki na ma-Shaafi'y hawana kigawanyo hichi cha Waajib kwao ila wao wana nguzo na Sunnah kwa ujumla wake.

 

Hapa tutaweka yale yaliyotajwa ambayo yanaelekea kuwa na nguvu zaidi.

 

Kwanza kabla hatujataja mambo yenyewe, tunapaswa kujua kuwa mambo ya Waajib ni yale ambayo vilevile atakapoacha mtu kwa makusudi hubatilika Swalaah yake, na atakapoacha kwa kusahau inamtosheleza yeye kusujudu Sijda mbili za kusahau (Sujuwdus-Sahw).

 

 

Mambo ya Waajib ambayo yametajwa katika kitabu cha 'Swahiyhu Fiqhis-Sunnah' kwa dalili mbalimbali za Aayah na Hadiyth ni 9 kama yafuatayo:

 

1.   Du'aa ya ufunguzi wa Swalaah (Du'aa al-Istiftaah).

 

2.  Kusema:

 

أَعـوذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْـطانِ الرَّجيـم

A’uwdhu biLLaahi minash-shaytwaanir-rajiym

 

kabla ya kusoma

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

Na kabla ya Suwrah Al-Faatihah.

 

 

3.  Kusema baada ya Suwrah Al-Faatihah:

 

آمين

Aamiyn

 

4.  Takbiyrah za kuhama baina ya kitendo na kitendo.

 

5.  Kusema:

 

سَمِـعَ اللهُ لِمَـنْ حَمِـدَه

Sami’a Allaahu liman hamidah

 

6.  Kusema katika I'itidaal.

 

 

رَبَّنـا وَلَكَ الحَمْـدُ  

Rabbanaa walakal-hamdu,  

 

7.  Kusema:

 

سُبْـحانَ رَبِّـيَ الْعَظـيم

Subhaana Rabbiyal ’Adhwiym

 

Wa kurukuu na kusema:

 

سُبْـحانَ رَبِّـيَ الأَعْلـى  

Subhaana Rabbiyal A’-laa

 

Wakati wa kusujudu.

 

 

8.   Tashahhud ya kwanza.

 

9.   Kikao cha Tashahhud ya kwanza.

 

 

Wanachuoni wengine wametaja mambo ya Waajib ni 8 kama yafuatayo:

 

 

1.  Takbiyrah nyingine zote isiyo ile ya Ihraam.

 

2.   Kusema

 

سَمِـعَ اللهُ لِمَـنْ حَمِـدَه

Sami’a Allaahu liman hamidah

 

kwa Imaam na mwenye kuswali peke.

 

 

3.   Kusema:

 

رَبَّنـا وَلَكَ الحَمْـدُ  

Rabbanaa walakal-hamdu,  

 

 

4.   Kusema:

 

   

سُبْـحانَ رَبِّـيَ الْعَظـيم

Subhaana Rabbiyal ’Adhwiym

 

 

Mara moja kwenye kurukuu.

  

 

5.   Kusema

 

سُبْـحانَ رَبِّـيَ الأَعْلـى  

Subhaana Rabbiyal A’-laa

 

kwenye kusujudu.

 

 

6.  Kusema:

 

اللّهُـمَّ اغْفِـرْ لي

Allaahummaghfir liy

 

Kwenye kikao baina ta Sijda mbili.

 

7.  Tashahhud ya mwanzo.

 

8.   Kikao katika Tashahhud ya mwanzo.

 

Hizi ndizo maarufu zaidi kwa wanachuoni wengine.

 

 

Sunnah Za Swalaah 

 

Hizi ni kauli na vitendo zinazopendeza kuletwa katika Swalaah. Mwenye kufanya hayo hupata thawabu wala Swalaah haibatiliki kwa kuachwa hata kwa kusudi. Wala sijdah ya kusahau hailetwi. Hapa tuna vigawanyo viwili vya Sunnah katika Swalaah; Sunnah za kauli na Sunnah za vitendo.  

 

 

Sunnah Za Kauli:

  

1.  Kisomo baada ya al-Faatihah.

 

2.   Adhkaar nyinginezo katika Rukuu.

 

3.  Adhkaar baada ya kusimama kutoka katika Rukuu na baada ya kusema ‘Rabbana Lakal Hamd’.

 

4.   Adhkaar  nyinginezo katika Sujuud.

 

5.  Du’aa baina ya Sijdah mbili.

 

6. Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Tashahhud ya kwanza na ya pili.

 

7.   Du’aa baada ya Tashahhud ya kwanza na ya pili.

 

8.   Salaam ya pili.

 

9.   Adhkhaar na du’aa mbalimbali baada ya Swalaah.

  

 

Sunnah Za Vitendo:

 

1.  Kuweka Sutrah (kizuizi mbele ya sehemu unayoswalia) katika Swalaah.

 

2.  Kunyanyua mikono wakati wa Takbiyratul Ihraam, na wakati wa kurukuu na na wakayi wa kunyanyuka kwayo na wakati wa kuinuka kutoka katika Tashahhud ya kwanza. Na kadhalika wakati unapoinama na kuinuka.

  

3.  Kuweka mkono wa kuume juu ya mkono wa kushoto juu ya kifua unaposimama kuswali.

 

4.   Kutazama mahali pa kusujudu.

 

5.  Kulingana sawa mgongo unaporukuu na kutonyanyua kichwa au kukiinamisha sana, na kuweka viganja kwenye magoti mawili na huku umeviachanisha vidole vya mikono na kuachanisha viwiko visiguse mbavu au tumbo lako.

 

6.  Kuteremka katika Sijdah kwa mikono miwili kabla ya magoti.

 

7.  Kuimakinisha paji la uso, pua na mikono (viganja viwili) kwenye ardhi pamoja na kupanua mikono isiguse mbavu zako; kuwe na uwazi wa kuweza kupita kinyama kidogo. Na viganja vyako viwe usawa wa mabega au masikio wakati uko katika kusujudu na viwiko vikiwa vimenyanyuliwa juu na vidole vya mikono vikiwa vinaelekea Qiblah.   Matumbo ya vidole vya miguu yakiwa ardhini visigino vikielekea juu na hali vidole vya miguu vikielekea Qiblah.

 

8.  Kulilalisha guu la kushoto na kulisimamisha la kulia wakati wa kikao baina Sijdah mbili.

 

9.  Kurefusha kikao baina ya Sijdah mbili.

 

10. Kikao cha mapumziko baada ya kukamilisha rakaa ya kwanza na ya tatu.

 

11.  Kutegemea ardhi kwa mikono wakati mtu anaponyanyuka kutoka kusujudu na kwenda kwenye rakaa nyingine.

 

12.   Kukaa kikao cha Iftiraash (Kusimamisha mguu wa kulia na kukalia mguu wa kushoto) katika Tashahhud ya mwanzo. Na kukaa kikao cha Tawarruk (kusimamisha mguu wa kulia na kuipitisha mguu wa kushoto chini ya muundi wa mguu wa kulia na huku kikalio chako kimekaa juu ya ardhi).

 

13.  Kuashiria kwa kidole cha shahada katika Tashahhud kuanzia mwanzo hadi mwisho bila kukishusha na huku unasoma na ukikitazama.

 

[Abu Maalik Kamaal Saalim, Swahiyh Fiqhus Sunnah, Mj. 1].

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share