Maiti Kukamuliwa – Ameusia Asikurubishwe Na Moto

 

Maiti Kukamuliwa – Ameusia Asikurubishwe Na Moto

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Assalamu alaikum warahmatullahi,

 

Hivi majuzi niliandika wasia wangu kama alivyo amrisha Allaah na Nabiy wake. Katika wasia wangu niliandika kuwa maiti yangu isikurubishwe moto hata pale nitakapo kuwa nimekwa chumbani katika kuoshwa na kukafiniwa. Watu wangu wakaniuliza jee pale tutakapo kukamua, tukufukize vipi? Sasa suala langu Mashekhe wangu liko hapa. Huku kukamuliwa, je ni mila, au ni madhehebu au ni sunnah?

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Vitabu mbalimbali maarufu vya Fiqhi kama Al-Mulakhkhasw al-Fiqhiy cha Shaykh Dkt. Swaalih Fawzaan aal-Fawzaan, na pia Swahiyh Fiqhis Sunnah cha Shaykh Abuu Maalik Kamaal Sayyid Saalim.

 

Vitabu hivi ambavyo tumevitaja na vyenginevyo vinatueleza njia ambayo inafaa kufuatwa ili kumtayarisha Muislamu aliyekufa kwa mazishi. Katika moja wa njia hiyo ni kukamuliwa maiti ili kukamilisha tendo la kuoshwa, kuswaliwa na kisha kuzikwa. Waislamu na hasa wanazuoni hawakubaliani katika jambo la batili. Lakini fahamu kuwa kukamuliwa huko si kukamuliwa kama wanavyofanya baadhi ya watu au vitabu vinavyosema kuwa anakamuliwa kwa nguvu, na hadi wengine wanamkunja maiti na kuminya tumbo lake na kulikamua kwa nguvu hasa. Hayo ni makosa. Lililo sahihi ni kumkamua kwa upole, ni kama unalipapasa tumbo lake na kulibonyeza kwa upole na utaratibu na kama kipo choo kitatoka na kama hakipo basi hakipo wala hakuna haja yoyote ya kumbana, kumminya, na kumpinda kama wengine wanavyofanya kutokana na mafundisho ya baadhi ya Mashaykh na vitabu.

 

Muislamu aliye hai anafaa kujisafisha na kuondoa uchafu kwa juhudi yake kubwa. Lakini pindi anapofariki huwa hawezi kujitwahirisha wala kujisafisha hivyo inafaa walio hai wamkirimu kwa kumsafisha na kumtayarisha kwa ajili ya mazishi. Katika kumsafisha ni kumtoa uchafu ulio ndani ya matumbo. Na inafaa tufahamu kuwa kukamuliwa huko kunafanywa kwa taratibu ili asiumizwe kwa njia yoyote ile.

 

Ama kutumiwa kwa moto si jambo lenye kupendeza wakati wowote ule, lakini kwa kama kuna harufu au kunachelewa hilo, basi kunaweza kuchomwa udi au kupulizwa vinukiavyo ili kuondoa harufu mbaya iliyo katika chumba anachooshewa maiti.

 

Kwa faida zaidi ya mas-alah ya maiti, ingia kwenye viungo vifuatavyo:

 

Yampasayo Maiti

 

Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share