Zingatio: Akili Zinapotawaliwa Daima Hazitofanikiwa

 

Zingatio: Akili Zinapotawaliwa Daima Hazitofanikiwa

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Uislamu ni dini ambayo imekamilika kwa namna ambayo yeyote aweza kuifuata na kuisimamisha. Sio dini ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘Anhum) pekee. Bali ni dini ya Ulimwengu mzima. Historia yaonesha kwamba Uislamu ulikuwa na nguvu kubwa enzi za nyuma kuliko hali tuliyokuwa nayo sasa. Hivyo, kama misingi hii inaweza kufuatwa na wasiokuwa Waislamu, kwanini Waislamu wenyewe washindwe kuzifuata?

 

Yaonesha dhaahir kwamba hila zinabuniwa, kutekelezwa na kufanikiwa katika kuangusha mila na desturi za Kiislamu kwani hakuna taifa wala Kiongozi mmoja wa kuwaunganisha Waislamu. Uislamu ni dini yenye Shahadah moja, Qiblah kimoja, Mfungo wa Swawm mmoja na Hijjah moja tu. Hivyo yaonesha wazi wazi kuwa ni dini ya mshikamano, lakini bado haitendewi haki namna inavyotakiwa. Kilio kikubwa ni kwamba, juu ya kuwepo nguzo hizi za kutuunganisha lakini hatuna kauli moja wala vitendo vyenye muelekeo mmoja katika mila na desturi zetu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba Waumini ni wamoja na wanafanana na jengo:

 

Hakika Muumini Kwa Muumini ni kama jengo, wanashikamana pamoja)) Akafungamisha Vidole vyake Pamoja” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Badala yake, tunaiendea kinyume Hadiyth hiyo na kuwa pamoja na hila za Magharibi katika kuupiga vita Uislamu.

 

Tunashuhudia kuwepo mlolongo mkubwa wa shughuli za kuwadumaza Waislamu ili wasiwe ni wenye kuona mbali na kuweza kutoa mawazo ambayo yatakwenda kinyume na misingi ya kibepari. Misingi hii ya kibepari ni ile ambayo inamtoa thamani mwanamke, kuwadhalilisha viumbe kwa neno la demokrasia na uhuru. Imekuwa hii dunia ni uwanja wa fujo tu, mpate mpatae, mshike mshike. Hajulikani nani muadilifu wala mtenda madhambi.

 

Waislamu tumefanana na mbu kukosa kumbukumbu. Kwani hatukumbuki namna walivyopigwa vita, kubakwa, kuuawa na kuteswa Waislamu waliopo Afghanistan kwa neno la ‘ugaidi’, Iraaq kwa neno la ‘dikteta’ na Chechnya kwa neno la ‘usalama’. Yote haya yanafanywa kwa nani na kwa ajili ya kupata nini? Hakuna chengine kinachogombaniwa hapa ila kuhodhi mamlaka chini ya mkono mmoja wenye nguvu za kushika na kuachia.

 

Utawala huu wa kimabavu duniani bado unaendelea, na unalenga zaidi kunufaisha nchi za Magharibi. Mfano mzuri tu ni namna Waislamu wanavyoshughulishwa mno na mambo ya anasa na kupoteza muda.

 

Mechi za mpira ni moja kati ya zana kuu zinazotumiwa kuupiga vita Uislamu. Kama hatutakuwa makini, daima tutakuwa wapofu kwa kuhifadhi majina ya wachezaji pamoja na historia ya klabu za mpira. Huku tukiacha nyuma Siyrah tukufu ya Uislamu pamoja na matendo sahihi ya Uislamu. Hatukai kufikiria namna mzunguko wa mechi hizi zinavyopokezana, mechi zisizokuwa na mwisho kana kwamba wanaoshuhudia pia ni wenye kufanya mazoezi ya mpira.

 

Kuna mechi za ligi kuu ndani ya mikoa, nchi nzima, nchi jirani pamoja na Afrika nzima. Ukipiga hesabu utapata takriban sio chini ya mechi 100 kwa mwaka mzima. Tukitoka Afrika, tunakwenda chimbuko la ukoloni duniani na kupata mashindano ya kombe la Uingereza, carling cup na FA yanayoshindaniwa kila mwaka. Kabla yake kuna mechi za Uingereza, Spain na Ujerumani. Kama hizo hazitoshi, kuna kombe la dunia la kila baada ya miaka minne. Huku mechi zikichuja hatua kwa hatua kupata mataifa yatakayoshiriki kombe la dunia.

 

Huko ndiko akili zilipoelekezwa. Ni kutokana na mechi hizi, Waislamu wanaswali kwa kudonoa donoa namna kuku anavyodonoa mtama. Akili hazijajikomboa kuona namna Uislamu unavyoangushwa na kutengenezewa hila mpya kila siku. Iblisi na kundi lake la Magharibi hawalali wakitafakari njia mbadala za kuwapotosha Waislamu bila ya kuwabatiza.

 

Mechi hizi ndizo zinazowafanya Waislamu kushindwa kusoma fiqhi na kuelewa taratibu za ndoa, mirathi na kadhalika. Mtandao wa Alhidaaya   umejaa masuala kede kede yenye kuonesha dhaahir mmommonyoko wa maadili. Inafikia hatua Muislamu anauliza kama uzinifu (kuwa na girlfriend au boyfriend) ni halali au haramu? Yote hayo yanatokana na kukosa elimu kwa kufuata mdundiko wa pumbazo kama hizi.

 

Jee hatujafikia hatua ya kuamini namna hizi akili zilivyotekwa nyara? Bila ya shaka yoyote hazitakuwa ni akili zenye kuona mbali isipokuwa kuweka mbele mazungumzo ya mpira badala ya kupanga mikakati ya kukuza Uislamu, kuchangia miradi ya Uislamu pamoja na kuhisabu Waislamu wanaouawa kila leo na kudhulumiwa kila sekunde. Mechi hizi ndizo zinazotengeneza njia ya kuendeleza biashara za ulevi kwa matangazo ya pombe kwenye viwanja na fulana za wachezaji, kukuza uchumi wa Magharibi na kuwadumaza Waislamu.

 

Tuanze leo, tusisubiri zaidi kubadilika na kuishi Kiislamu katika kila hatua. Kama kweli tunahitaji mpira, tusiwe ni wenye kufuata tu kila kitu. Tutumie muda muafaka kufanya mazoezi ya kweli kweli kusakata kandakanda huku tukitumia muda mwingi zaidi kutafakari juu ya Uislamu wetu. Kuwa bwana wa nafsi yako na wala usiwe mtumwa kwa nafsi yako kufuata kila kipendacho nafsi.

 

Share