Zingatio: Kukopa Arusi, Kulipa Matanga

 

Zingatio: Krismasi: Kukopa Arusi, Kulipa Matanga

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Maisha yetu ndani ya Uislamu yanagusa nyanja zote za mahusiano yetu; iwapo ni baina ya mja na Rabb wake, ama mja kwa mja mwenziwe. Ndio maana hata tunakuta ndani ya Qur-aan maelezo ya kina juu ya kufanya uadilifu katika masuala ya mikopo.

 

Hakuna shaka yoyote kwamba Waislamu katika enzi za dunia ya leo wanashiriki sana kwenye masuala ya mikopo. Wala hakuna atakayekanusha kwamba migongano, fitnah na migogoro mikubwa inatokana na mikopo kufanyika kwa njia za hadaa na uongo.

 

Uislamu wetu unatuamuru kwamba, kwenye suala la deni lolote, kubwa au dogo, tusiwe ni wenye kupuuzia kufanya kwa maandiko. Hii itasadia upande mmoja utakaokwenda kinyume na makubaliano hayo kuwa na nguvu kwa ushahidi wa maandiko aliyoyafanya. Ndio maana wazee wetu walituusia kwa kusema: ‘Nguvu ya maji ni mawe (matumbawe) mlimwengu na mwanawe’. Halikadhalika, nguvu ya mkopwaji ni maandiko na mashahidi wake.

 

Mbali na suala la kuandikwa deni katika maandishi, ni lazima pia mambo matano yafuatayo yatimie:

 

1.     Iandikwe deni kwa muda uliowekwa

2.     Mwandishi aandike kwa uadilifu

3.     Wala (mwandishi) asipunguze chochote ndani yake

4.     Kwa yule (mkopaji) anayehitaji msimamizi basi aandikishe msimamizi wake

5.     Washuhudie mashahidi wawili katika walio Waislamu

 

Vipengele vikuu hivi vya deni ndani ya Uislamu, vinapatikana ndani ya Aayah refu kabisa kuliko zote ndani ya Qur-aan inayofasiriwa kama ifuatavyo:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا تَدَايَنتُم بِدَيْنٍ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى فَاكْتُبُوهُ ۚ وَلْيَكْتُب بَّيْنَكُمْ كَاتِبٌ بِالْعَدْلِ ۚ وَلَا يَأْبَ كَاتِبٌ أَن يَكْتُبَ كَمَا عَلَّمَهُ اللَّـهُ ۚ فَلْيَكْتُبْ وَلْيُمْلِلِ الَّذِي عَلَيْهِ الْحَقُّ وَلْيَتَّقِ اللَّـهَ رَبَّهُ وَلَا يَبْخَسْ مِنْهُ شَيْئًا ۚ فَإِن كَانَ الَّذِي عَلَيْهِ الْحَقُّ سَفِيهًا أَوْ ضَعِيفًا أَوْ لَا يَسْتَطِيعُ أَن يُمِلَّ هُوَ فَلْيُمْلِلْ وَلِيُّهُ بِالْعَدْلِ ۚ وَاسْتَشْهِدُوا شَهِيدَيْنِ مِن رِّجَالِكُمْ ۖ فَإِن لَّمْ يَكُونَا رَجُلَيْنِ فَرَجُلٌ وَامْرَأَتَانِ مِمَّن تَرْضَوْنَ مِنَ الشُّهَدَاءِ أَن تَضِلَّ إِحْدَاهُمَا فَتُذَكِّرَ إِحْدَاهُمَا الْأُخْرَىٰ ۚ وَلَا يَأْبَ الشُّهَدَاءُ إِذَا مَا دُعُوا ۚ وَلَا تَسْأَمُوا أَن تَكْتُبُوهُ صَغِيرًا أَوْ كَبِيرًا إِلَىٰ أَجَلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ أَقْسَطُ عِندَ اللَّـهِ وَأَقْوَمُ لِلشَّهَادَةِ وَأَدْنَىٰ أَلَّا تَرْتَابُوا ۖ إِلَّا أَن تَكُونَ تِجَارَةً حَاضِرَةً تُدِيرُونَهَا بَيْنَكُمْ فَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَلَّا تَكْتُبُوهَا ۗ وَأَشْهِدُوا إِذَا تَبَايَعْتُمْ ۚ وَلَا يُضَارَّ كَاتِبٌ وَلَا شَهِيدٌ ۚ وَإِن تَفْعَلُوا فَإِنَّهُ فُسُوقٌ بِكُمْ ۗ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ وَيُعَلِّمُكُمُ اللَّـهُ ۗ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٢٨٢﴾ 

Enyi walioamini! Mtakapokopeshana deni mpaka [1]muda maalumu uliopangwa, basi [2]liandikeni. Na [3] aandike baina yenu mwandishi kwa uadilifu. Na wala asikatae mwandishi kuandika kama Allaah Alivyomfunza. Basi aandikishe kwa imla yule ambaye ana haki (mdai) na amuogope Allaah, Rabb wake, na wala asipunguze humo kitu chochote. Basi [4] ikiwa yule ambaye ana haki amepumbaa kiakili au mnyonge, au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe msimamizi wake kwa uadilifu. Na [5] mshuhudishe mashahidi wawili wanaume miongoni mwenu. Na ikiwa hakuna wanaume wawili, basi mwanamme mmoja na wanawake wawili katika wale mnaowaridhia miongoni mwa mashahidi, ili kama mmoja wao hao wanawake wawili akikosea (akasahau), basi mmoja wao atamkumbusha mwengine. Na mashahidi wasikatae watapoitwa. Na wala msichukie kuliandika (deni) dogo au kubwa mpaka muda wake. Hivyo kwenu ndiyo uadilifu upasavyo mbele ya Allaah na ndio unyoofu zaidi kwa ushahidi; na ni karibu zaidi ili msiwe na shaka; isipokuwa itakapokuwa biashara taslimu mnayoiendesha baina yenu, basi si dhambi kwenu msipoiandika. Na shuhudisheni mnapouziana. [6] Na wala asidhuriwe mwandishi wala shahidi; na mkifanya basi hakika huo ni ufasiki kwenu. Na mcheni Allaah, na Allaah Anakufunzeni, na Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi. [Al-Baqarah: 282]

 

Tumalizie kwa kuhimizana kushikamana na misingi imara ya Uislamu wetu bila ya kupepesuka wala kutetereka. Namna hii ndio itakayosaidia kuondosha hitilafu baina yetu, kusimamisha Uislamu kwa vitendo, kuwapatia mafunzo mema wale wasio kuwa Waislamu, kutengenea mambo yetu, kutiliwa baraka katika amana zetu na kupata thawabu zitakazotuwezesha mizani yetu ya mema kuizidi mizani ya shari.

 

Tusiwe ni wenye kuufanyia kazi msamiati unaosema kwamba ‘kukopa arusi, kulipa matanga’. Bali kwetu Waislamu tufungie pazia jipya la kuufanya msemo huu kupitwa na wakati ndani ya jamii zetu. ‘Ada ya mja kunena, muungwana ni kutenda’.

 

 

Share