Nimeweka Nadhiri Lakini Sijui Nimeahidi Nini

SWALI

ASSALAAM ALAYKUM RAHMATULLAAHI WA BARAKAATUH,

Ni mara ya kwanza kujiunga na darasa hili. Naanza kwa kuuliza

Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 24, nimeolewa. Nimepitia mitihani mizito ambayo ilinipelekea kuweka nadhili. Baada ya kupita muda nimesahau kuwa niliahidi nini mbele ya allah.Na nilipokumbuka kuwa niliweka nadhili nimesahau ya kwamba nilisema nitafanya nini.JE NIFANYEJE ILI NITOE NADHILI HIYO?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kwanza kupokea swali lako kwa mara ya pili baada ya kulituma katika anuani ipasayo tunashukuru kwa ushirikiano wako mwema.

Ama kuhusu upasalo kutenda ni kwamba madamu una hakika kuwa uliweka nadhiri (na sio nadhili kama ulivyoandika), na hali ni kama hiyo kuwa umesahau ulisema utafanya nini, basi ni vizuri kulipa kafara yake ambayo utekeleze kwa mpango ufuatao:

 

 Mwanzo:   Kuwalisha masikini kumi chakula cha wastani, akitoweza;

 

Pili:              Kuwavisha nguo idadi hiyo ya masikini, akitoweza; 

 

Tatu:          Kuacha mtumwa huru (jambo hili halipatikani sasa) hivyo utafuata amri ya nne. 

 

Nne:           Ikiwa hakuweza haya ndio itabidi afunge siku tatu (3).

 

Vile vile soma Swali na jibu katika kiungo kifuatacho upate manufaa zaidi katika mas-ala haya:

 Ameweka Nadhiri ya Kusoma Maulidi Kisha Katambua kuwa Ni Bi'dah afanyeje?

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akutakabalie kafara yako.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share