Niliweka Nadhiri Lakini Nimesahau Nadhiri Yenyewe Vipi Niitimize?

 

SWALI:

Assalaam alaykum

Ni mara ya kwanza kujiunga na darasa hili. Naanza kwa kuuliza swali:-mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 24, nimeolewa. Nimepitia mitihani mizito ambayo ilinipelekea kuweka nadhili. Baada ya kupita muda nimesahau kuwa niliahidi nini mbele ya Allah. Na nilipokumbuka kuwa niliweka nadhili nimesahau ya kwamba nilisema nitafanya nini. JE NIFANYEJE ILI NITOE NADHILI HIYO?

 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Nadhiri. Katika Lugha maana ya Nadhr (Nadhiri kwa Kiswahili) ni kujibiwa na kisheria ni kuilazimisha nafsi yako uliyochagua kufanya kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka.

Nadhiri ni aina ya ‘Ibaadah, haifai kufanywa kwa asiyekuwa Allaah Aliyetukuka. Na anayeweka Nadhiri kwa asiyekuwa Allaah Aliyetukuka ima kwa kaburi, au mfalme, au Shaykh, au Nabii, au walii, na kadhalika hakika atakuwa amefanya shirki kubwa inayomtoa mtu katika mila ya Uislamu.

Awali ya yote ni kuwa hukmu ya Nadhiri ni makruhu na baadhi ya wanazuoni wameharamisha hiyo. Imepokewa kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuweka nadhiri, akasema:

Hakika hairudishi chochote, bali inatolewa kutoka kwa bakhili” (al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah).

Mwenye kuweka Nadhiri huilamizimisha nafsi yake kitu ambacho hajalazimishwa na sheria, hivyo akaipatia uzito nafsi yake kwa Nadhiri. Hakika ni kuwa kufanya jambo la kheri inatakiwa na kila Muislamu hata bila ya kuweka Nadhiri. Hata hivyo, anapoweka Nadhiri kufanya amali njema, ni wajibu wake kutekeleza kwa kauli ya Aliyetukuka:

Na chochote mnachotoa au Nadhiri mnazoweka basi hakika Allaah Anajua” (2: 270).

Na amesema Aliyetukuka katika kuwasifu wema:

Wanatimiza ahadi (nadhiri), na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana” (76: 7).

Na tena:

Na waondoe Nadhiri zao” (22: 29).

Na amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

Aliyeweka nadhiri kumtii Allaah amtii, na aliyeweka nadhiri kumuasi Allaah, basi asimuasi” (al-Bukhaariy).

Ni ajabu kwa Muislamu awe ni mwenye kusahau jambo alilomuahidi Allaah Aliyetukuka katika utiifu na wema. Kwa kuwa hujui unachotakiwa kufanya unatakiwa ujaribu kukumbuka, ikiwa umeshindwa kabisa itabidi utoe kafara yake kwa kutoweza kutimiza uliyoyawekea nadhiri.

 

Kafara ya kutotekeleza Nadhiri ya utiifu ni kama kafara ya yamini. Kafara hii imewekewa utaratibu wa kufuatwa kama Alivyosema Allaah Aliyetukuka:

Allaah Hatakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakushikeni kwa mnavyoapa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiyepata hayo, basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapoapa. Na hifadhini yamini zenu” (5: 89).

Kwa mpangilio ni kufanya yafuatayo:

  1. Kuwalisha masikini 10 kwa kila masikini nusu swaa’ (kilo 1¼) ya chakula unachokula.

  2. Kuwavisha masikini 10 kwa nguo zinazotosheleza kwa kila mmoja kuswalia nazo.

  3. Kumuacha mtumwa Muumini huru.

  4. Akitoweza na kupata hayo matatu ya juu, afunge siku tatu mfululizo.

Ikiwa mtu ni muweza wa kulisha au kuvisha haifai kwake kufunga.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share