Majini Wanajua Siri Za Watu? Vipi Mtu Aweze Kuwaona?

 

Majini Wanajua Siri Za Watu? Vipi Mtu Aweze Kuwaona?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Ilikuwa napenda kuliza swala kuhusu majini: majini hujua vipi siri za watu? Na vile vile mtu afanye nini awaone? 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakika ni kuwa majini hawajui siri kabisa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuambia kuhusu Majini waliotaabika kumfanyia kazi Nabiy Sulaymaan ('Alayhis Salaam) na ilhali Nabiy huyo ameagaa dunia, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 فَلَمَّا قَضَيْنَا عَلَيْهِ الْمَوْتَ مَا دَلَّهُمْ عَلَىٰ مَوْتِهِ إِلَّا دَابَّةُ الْأَرْضِ تَأْكُلُ مِنسَأَتَهُ ۖ فَلَمَّا خَرَّ تَبَيَّنَتِ الْجِنُّ أَن لَّوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ الْغَيْبَ مَا لَبِثُوا فِي الْعَذَابِ الْمُهِينِ ﴿١٤﴾

Basi Tulipomkidhia mauti, hakuna kilichowajulisha kifo chake isipokuwa mdudu wa ardhi akila fimbo yake. Basi alipoanguka ikawabainikia majini kwamba lau wangelikuwa wanajua ya ghayb, basi wasingebakia katika adhabu ya kudhalilisha. [Sabaa: 14]

 

Ama kujua kwao baadhi ya mambo ni kule kukaa kwao katika baadhi ya makao ili kusikiliza, lakini baada ya kuja kwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) yule aliyekuwa akienda kusikiliza atakuta kimondo (kijinga cha moto) kinamvizia kama Ananvyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  

 

وَأَنَّا لَمَسْنَا السَّمَاءَ فَوَجَدْنَاهَا مُلِئَتْ حَرَسًا شَدِيدًا وَشُهُبًا﴿٨﴾وَأَنَّا كُنَّا نَقْعُدُ مِنْهَا مَقَاعِدَ لِلسَّمْعِ ۖ فَمَن يَسْتَمِعِ الْآنَ يَجِدْ لَهُ شِهَابًا رَّصَدًا﴿٩﴾

Na kwamba sisi tulitafuta kuzifikia mbingu, basi tukazikuta zimejaa walinzi wakali na vimondo. Na kwamba sisi tulikuwa tukikaa huko vikao kwa ajili ya kusikiliza, basi atakayetega sikio kusikiliza sasa atakuta kimondo kinamvizia. [Al-Jinn: 8-9]

 

 Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    ametuelezea hayo kuwa majini huwa wanadoea ili kupata habari. Wanapofika kwa wachawi wao au wale wanaowatumia katika asili mia moja huwa ni ukweli waliochanganya na 99 ya uongo.

 

Kwa sababu wao wanatuona nasi hatuwaoni huweza wao wakapata maalumati yetu kutoka kwetu kisha wakayapeleka kwa wale wachawi. Kuhusu sisi kuwaona hakuna njia kwani wao ni viumbe wasioonekana na wana Aadam. Pia si muhimu kwetu kuweza kuwaona kwani kufanyika hilo halitatuongezea sisi katika iymaan na taqwa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share