Baba Yake Amemkataza Kwenda Kwa Shaykh Kusomewa Naye Anakwenda Kwa Kificho

 

SWALI:

 

Assalamu aleikum

mimi nliwahi kwenda kwa ustadh mmoja ambaye kazi yake kutibu watu maswali ya wadudu kwa quran na mashallah hua anafanyikiwa, aliponiona na mie na nlikua na matatizo yangu alinambia na mie pia nna matatizo akanambia niwe nakwenda kupata kisomo na mie mwenyewe nkawa najitahidi kusoma lakini ilikua bado nnayo lakini sipandishi.

Aliponambia niwe nakwenda nkamuomba ruhusa babangu akawa hapendi mambo haya akawa ananikataza nisiende lakini nkawa nakwenda kificho ficho yeye hajui baadae nkawacha lakini bado najiona ndivo sivo. je, inafaa nende katika kisomo ilhali babangu hataki? Ni quran ndio nayoiamini ndo mana nkawa nakwenda bila ya yeye kujua... inshallah kheir


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kukatazwa na baba kwenda kusomewa na Ustaadh.

 

Mara nyingi masuala ya ma-Ustaadh yanagubikwa na utata mwingi pamoja na kutoeleweka jinsi wanavyofanya katika kutibu masuala ya majini. Kwa ajili hiyo huenda akawa baba yako hajakuelewa na hivyo kukukataza usiende ukatibiwa na huyo Ustaadh.

 

Kwa hiyo, awali ya yote kabla ya kuendelea kwenda inafaa umweleze baba yako kuwa kisomo hicho ni cha kishari’ah na hakuna ushirikina ndani yake wala uchawi ambao umekatazwa na shari’ah ya Uislamu. Ikiwa amekataa nawe ni mgonjwa itabidi uwe unakwenda ili upate matibabu yanayo kwenda sambamba na shari’ah yetu tukufu.

 

Hata hivyo, baada ya kusoma swali lake ninaingiwa na utata kwani umesema kuwa “aliponiona na mie na nilikuwa na matatizo yangu aliniambia na mie pia nina matatizo akaniambia …” Haya maelezo ni kama yale ya wachawi wanapowaambia watu wanapowaona tu kuwa wana matatizo. Hilo ni jambo ambalo haliwezekani, na mwenye kumwamini mtu kama huyo anakuwa ameingia katika ushirikina. Kwa hiyo unatakiwa uwe na tahadhari sana, kwani Ustaadh mwenye kusoma kisomo cha kishari’ah huwa hajui matatizo yako ila baada ya kukusomea. Na hata baada ya kukusomea hatoweza kujua matatizo yako ila anaweza kufahamu kuwa umefanyiwa uchawi au umekumbwa na jini, wala sio kujua matatizo mengine.

 

Nasaha yetu kwako ni kuwa uwe mwangalifu usije ukapata hasara kwa kuingia katika madhambi makubwa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share