Mkwe Anashiriki Mambo Ya Uchawi, Mume Anaogopa Kumnasihi Mama Yake - Vipi Mke Awakinge Wanawe?

 

Mkwe Anashiriki Mambo Ya Uchawi, Mume

Anaogopa Kumnasihi Mama Yake -

Vipi Mke Awakinge Wanawe?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam alaykum warahmatullah wabarakatuh.

Napenda kumshukuru Allaah mwingi wa rehma zisizohesabika. In shaa Allaah Ijumaa ya leo iwe njema kwa sote Amin.

 

Mkwe wangu ana mambo ya ushirikina anataka kuwakabidhi watoto wangu mzimuni. Naomba Mnipe Kinga Yangu Na Watoto Wangu. Hasara mume wangu anaogopa kumwambia kitu mama yake.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Hili ni tatizo sugu katika jamii yetu – ushirikina. Ushirikina ambao unampeleka mtu katika dhulma kubwa na kuishia kwenye Moto wa Jahannam. Inatakiwa dada yetu usimama kidete, imara kuhakikisha kuwa mkwe wako hafaulu katika hayo, na In shaa Allaah hatofaulu.

 

Mwanzo kabisa kabla ya kutaka kinga ya watoto wako una wajibu wa kuona kuwa mama mkwe wako ametoka katika ushirikina ili asipate kipigo na kichapo cha hapa duniani na Kesho Aakhirah. Ikiwa mumeo hawezi kuzungumza naye basi itabidi utafute watu wengine unaoelewana nao wanaoweza kumnasihi arudi katika Dini sahihi.

 

Pili, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia kinga nyingi kwetu sisi na watoto wetu. Miongoni mwa hizo ni:

  

  1. Ni kusoma Suwrah Al-Baqarah, kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Nyumba inayosomwa Suwrah Al-Baqarah haingii Shaytwaan”. Na hasa katika hizo ni kusoma Aayah kumi asubuhi na jioni, nazo ni Aayah 1 – 5, 255 – 257 na 284 – 286.

 

  1. Kusoma Suratul Ikhlaasw (112), Al-Falaq (113) na An-Naas (114), yaani Suwrah tatu za mwisho. Inafaa uzisome mara tatu tatu asubuhi na jioni na pia unapokwenda kulala.

  

  1. Pia kuna du’aa za kuwakinga watoto. Tafuta kijitabu kinachoitwa Hiswn al-Muslim na utazipata nyingi sana. Kinapatikana pia hapa Alhidaaya Hiswnul Muslim.

  

  1. Pia unapokutana na mumeo kimwili, inafaa msome du’aa ifuatayo: ‘Bismillaahi Allaahumma jannibniy Shaytwaana wa jannibish Shaytwaana maa razaqtanaa.’

  

  1. Pia uwe unasoma du’aa unapoingia nyumbani na unapotoka, unapoingia chooni na unapotoka na du’aa nyinginezo.

   

In shaa Allaah watoto wako watakuwa salama na hawatodhurika.

 

Vipi Kuwakinga Watoto Na Mashaytwaan?

 

Kuhusu Mashaytwaan Na Vipi Kujikinga Nao

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

 

Share