Kufunga Uzazi Kwa Sababu Ya Umri Mkubwa Inajuzu?

SWALI:

 

Mimi ni mwanamke wa miaka 44 nina watoto 6 na sasa nina mimba ya mtoto wa 7. Nafikiria nikishajifungua salama mara hii kufunga kabisa kizazi kwa sababu ya umri wangu mkubwa. Je naruhusiwa kufanya hivyo sitokuwa makosani?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kufunga mimba kabisa kwa ajili ya umri mkubwa.

Shari’ah haijamruhusu mwanamke mwenye umri mkubwa kufunga uzazi.

Hilo la kuwa na umri mkubwa si katika sababu za kumfanya mwanamke afunge kizazi. Na ikiwa una umri wa miaka hiyo huna muhula tena mwingi ila damu itakuwa ni yenye kukatika yenyewe pasi na kufunga kizazi.

 

Ikiwa ipo hatari ya kiafya na athari nyenginezo unaweza kufunga kizazi kwa muda kwani hujui kama unaweza kuhitajia kuzaa kwa sababu moja au nyengine. Yupo mwanamke aliyefunga kizazi kabisa alipopata watoto wawili. Mara ikaja ajali wakaaga dunia watoto wote wawili naye akatamani sana mtoto mwengine lakini kukawa hakuna njia ya yeye kuzaa tena akawa anajuta sana lakini majuto ni mjukuu.

 

Tazama pia Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliolewa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa na umri wa miaka 40. Na katika maisha yao ya kuishi pamoja kwa muda wa miaka 25 walipata watoto 6, kumaanisha alizaa akiwa na zaidi ya miaka 45.

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Kupanga Uzazi Na Sio Kuzuia Uzazi

Uzazi Wa Kupanga Unafaa?

Njia Gani Inayopasa Katika Sheria; Kuzuia Au Kupanga Uzazi?

Nimeshauriwa Kuzuia Uzazi Na Daktari

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share