Mimi Na Mume Wangu Hatukubaliwi Duaa Zetu Kwa nini?

SWALI:

 

Assalamu 'Alaykum wa Rahmatullah Wabarakatuh.

 

Naommba munifahamishe jinsi ya kumuomba Allaah (Subhanahu wa Ta'ala) ili anitatulie matatizo niliyonayo. Kiufupi, nina matatizo ya maisha yaliyotukabili mimi na mume wangu kwa kipindi kirefu sasa, pa kuelekea ila kwa mola wetu Allaah (Subhanahu wa Ta'ala) kwani yeye ametuambia tumuombe atatujibu.

Tunajitahidi katika kufanya ibada, kuswali, kufunga, kuamka usiku kuswali na kuomba dua'a lakini Allaah (Subhanahu wa Ta'ala) hajatuitikia duaa zetu. Suala langu, je? Katika kufanya kwetu ibada labda tunakosea ndio maana Allaah hatuitikii? Au kuna kitu tunaongeza ambayo Allaah hawezi kutoa malipo kwa hayo? Kwa mfano kama nilivosoma kwenye makala yenu ya kila siku kuwa kuna hadithi za uzushi ambazo zinaengeza ufanyaji wa ibada mabazo hazipo katika uislamu wala sunna na ukitekeleza aina za ibada hiyo basi Allaah hakulipi bali ni dhambi tu.

 

Shukani kwa kunisaidia muislamu mwenzenu katika ibadah. Na Allaah atakulipeni mema inshaAllaah.


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mas-ala ya Du'aa. Mwanzo tufahamu kuwa Muislamu hafai kukata tamaa na rehema za Allaah Aliyetukuka:

 

"Wala msikate tamaa na rehema ya Allaah. Hawakati tamaa na rehema ya Allaah isipokuwa makafiri" (12: 87).

 

Na bila shaka Allaah pia Amesema kweli nasi ndio tunaokosea, kwani Yeye Ametuahidi:

 

"Na waja Wangu watakapokuuliza hakika Yangu, waambie kuwa Mimi niko karibu nao. Naitikia maombi ya mwombaji Anaponiomba. Basi na waniitikie na waniamini, ili wapate kuongoka" (2: 186).

 

Bila shaka, Allaah Aliyetukuka Anamkubalia kila mmoja wetu kwa namna yake. Ibn al-Qayyim anatuambia zipo njia nyingi jinsi ya Allaah Aliyetukuka Anavyojibu du'aa zetu. Miongoni mwazo ni:

 

1.     Kujibiwa unachotaka hapa hapa kama ulivyoomba.

2.     Kubadilishiwa lililo bora hapa badala ya uliloomba ambalo halingekuwa na kheri kwako.

3.     Du'aa yako kuchelewesha na kupatiwa bora Akhera.

4.     Kumuondoshea shari.

5.     Kucheleshwa kujibiwa hapa hapa duniani lakini ikawa ni mtihani kwa mwenye kuomba.

Kawaida hapa duniani kuna mitihani mingi na moja wapo ni kutiwa katika mitihani au misukosuko. Kwani Aliyetukuka Anatuambia:

 

"Na Tutakutieni katika msukosuko wa baadhi ya mambo haya; hofu na njaa na upungufu wa mali na wa watu na matunda. Na wape bishara njema kwa wanaosubiri" (2: 155).

 

 

Na pia,

 

"Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, na hali hamjajiwa na mfano wa yale yaliowajia wale waliopita kabla yenu? Yaliwapata mashaka na madhara na wakatetemeshwa sana hata Mitume na walioamini pamoja nao wakasema: 'Nusura ya Allaah itafika lini?' Jueni kuwa nusura ya Allaah iko karibu" (2: 214).

Na pia,

 

"Je, watu wanadhani wataachwa wasitiwe katika misukosuko kwa kuwa wanasema: 'Tumeamini?' Basi ndio wasijaribiwe? Hapana; bila shaka Tuliwatia katika taabu wale waliokuwa kabla yao, na kwa yakini Allaah Atawatambulisha walio wa kweli na wale waongo" (29: 2 – 3).

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Hakika Allaah Akiipenda kaumu yoyote basi huitia katika mtihani" (at-Tirmidhiy).

 

Hakika ni kuwa zipo sababu ya du'aa ya Muislamu kutojibiwa kabisa. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"…kisha akamtaja mtu anayekwenda safari ndefu, nywele zake zimechafuka na kujaa vumbi, ainua mikono yake mbinguni (akisema): Ee Mola! Ee Mola – na ilhali chakula chake ni cha haramu, kinywaji chake ni cha haramu, kivazi chake ni cha haramu, amelishwa haramu! Je, atatakabaliwaje?" (Muslim)

.

Kulingana na Aayah na Ahaadiyth tulizotaja hapo juu pamoja na nyinginezo tunaona sababu za kutojibiwa du'aa ni:

1.     Kutoamini na kutoitikia mwito wa Allaah Aliyetukuka.

2.     Ukosefu wa uongofu.

3.     Kutumia vya haramu kama chakula, kivazi, kinywaji na vyenginezo.

4.     Kuwa na kiburi.

5.     Kuomba tu wakati wa shida. "Mwenye kutaka kujibiwa du'aa wakati wa shida na dhiki akithirishe du'aa wakati wa raha" (at-Tirmidhiy na al-Haakim, aliyeisahihisha na akakubali adh-Dhahabiy).

6.     Usifanye haraka kutaka kupata jawabu. "Anajibiwa mmoja wenu maadamu hafanyi haraka, kwa kusema: Nimeomba lakini sijajibiwa" (al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

7.     Kutofanya 'Ibadah kiusahihi au kuchanganya na uzushi ndani ya 'Ibadah.

 

Kujibiwa du'aa iko mikononi mwa Allaah Aliyetukuka peke Yake. Tunahitajika kufanya yote ambayo yanamridhisha ili kupata radhi zake na kusaidiwa katika mambo mengi. Njia ambazo du'aa zetu zinajibiwa ni:

 

1.     Kuwa na Imani thabiti na yakini kuwa Allaah Aliyetukuka Atanijibu ikiwa si leo kesho.

2.     Kufanya 'Ibadah zilizo sahihi sio za kuzua.

3.     Kula vya halali.

4.     Adabu ya kuomba pia ni muhimu. Inatakiwa unapoanza mwanzo umsifu Allaah Aliyetukuka kwa kusema: "Yaa dhal Jalaal wal Ikraam" (at-Tirmidhiy) au "Allaahumma inniy as'aluka anniy ashhadu annaka Anta Allaahu laa ilaaha illa Anta al-Ahad asw-Swamad alladhiy lam Yalid wa lam Yuulad wa lam Yakullahu kufuwan ahad" (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, Ibn Maajah).

5.     Kuomba du'aa katika nyakati za kujibiwa kama baina ya Adhaan na Iqaamah, thuluthi ya mwisho ya usiku, unapofungua wakati umefunga Swawm, mchana mzima unapokuwa katika funga, ukiwa safarini na kadhalika.

6.     Kuwa na subira

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awaondoshee dhiki na taabu mlizo nazo na Awaweke mahali pema kesho Akhera.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share