Mwenye Kuzini Akitaka Kutubu Haruhusuwi Kuswali Na Kuomba

SWALI:

 

Assalam aleykum? naomba kuuliza Je! mtu akizini nikweli haruhusiwi kuswali mpaka siku arobaini zipite? kwani kuna maneno yanasemwa mtaani kwamba janaba la mzinifu ni siku arobain hata kama ataoga mara baada ya kuzini, kama ni kweli! mtu huyu hatakiwi kuswali mpaka siku arobain zipite atapata vipi nafasi ya kutubu kwa mola wake? na haliya kuwa hatakiwi kuswali?

Allah [s.w] asamehe makosa yote isipokuwa mshirikina, Je huyu mzinifu akifa kabla ya siku arobain inamaana kanyimwa nafasi yake ya kutubu? au ana njia nyingine ya kutubu? Naomba msaada wenu inshaalah. Assalam aleykum

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mwenye kuzini na toba yake katika sheria. Hakika ya mtaani ni mengi na Muislamu kuyachukua ya mabarazani na mitaani bila ya mambo hayo kuyaweka katika mizazi ya sheria. Mizani ya Muislamu ambayo anafaa kupima nayo mambo ni Qur-aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Masharti ya toba yanaelewa kuwa ni kujuta katika kufanya kosa lolote lile, kutia nia ya kutorudia tena, kujiondoa katika maasiya na kufanya mema. Ni hakika kuwa mema hufuta mabaya, kwani Allaah Aliyetukuka Anasema:Hakika mema huondoa maovu(Huud [11]: 114). Na Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) akasema mfano wa maneno hayo ya Allaah: “Mche Allaah popote ulipo na fuatisha baya kwa zuri, nalo litafuta (yaani hilo baya)” [At-Tirmidhiy]

 

Allaah Aliyetukuka Ametupatia fursa ya kutubia na Yeye ni Msamehevu sana na Anasemehe madhambi yote. Maadamu mwanadamu ametimiza masharti ya toba basi atakuwa ni mwenye kusamehewa naye anatakiwa kuanzia wakati huo afanye mema ili awe mahali pema na pazuri. Kwa hiyo, baada tu ya kutubia aanze kuswali na Swalaah zitakuwa zinakubaliwa na Allaah Aliyetukuka baada ya kuoga josho la janaba. Mas-ala ya siku arubaini hayapo kabisa katika sheria, ni uzushi usio na msingi wowote.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate makala mbalimbali muhimu kuhusu Tawbah.

 

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share