Ndugu Zake Nabii Yuusuf Walikuwa Manabii?

SWALI:

 

Assalam Aleykum,

 

Je, ni kweli kuwa ndugu zake Nabii Yusuf (a.s.) walikuwa manabii? Insha'Allaah, u can guide me on this.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) (A.S) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na ‘alayhis-salaam baada ya kutaja Mitume wengine. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu nduguze Nabii Yuusuf (‘Alayhis Salaam). Ukweli usiopingika ni kuwa hakuna chimbuko lolote la Kiislamu ambalo linatufahamisha kuhusu suala hilo. Hata hivyo, tunapoutizama Uislamu na sheria zake tutakuja pata jibu kuhusu hilo bila matatizo.

 

Tufahamu kuwa Manabii wote (‘Alayhimus salaam) wamelindwa na kuhifadhiwa na Allaah Aliyetukuka kufanya madhambi makubwa. Miongoni mwa madhambi makubwa katika Uislamu ni kuua au kutaka kuua na kufanya khiyana. Tunaposoma Surah Yuusuf (Surah ya 12) tunakuta vitimbi walivyofanya nduguze 10, katika uwongo, vitimbi na jaribio la kuua. Kwa hayo tuliyoyaeleza ni kuwa nduguze Nabii Yuusuf hawawezi kuwa walikuwa Manabii katika maisha yao bali ni Waumini wa kawaida waliofanya makosa na kutubia baada yake.

 

 Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share