Kurudia Makosa Kila Mara Tawbah Inafaa?

SWALI:

Kama  nimefanya kosa na baadae nikatubia kwa kosa hilo na nikalia nikisema sitarudia tena lakini baada ya muda nikarudia tena kosa lilelile , jee kutubia kwangu kwa mara ya pili kutafaa? na kama kutafaa jee ni mara ngapi unaweza kuleta toba kwa kosa moja utakalo lirudia rudia?

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Jambo ambalo tunatakiwa tulielewe ni kuwa hakuna mwanadamu aliyekamilika. Ndio Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema:

((كل ابن آدم خطّاء وخير الخطّائين التوابون ) )   رواه الترمذي وحسنه الألباني

  ((Kila mwanadamu ni mkosa na mbora mwenye kukosa ni yule anayetubia))  Imepokelewa na At-Tirmidhiy na kasema ni Hadiyth Hassan Shaykh Al-Albaaniy.

Inalopasa kwako ni kutubia kikweli na sharti zake ni zifuatazo:

 

  1. Kuomba maghfira  
  2. Kuacha  hayo maasi
  3. Kujuta
  4. Kuweka nia (azma) kuwa hatorudia tena
  5. Kama kaidhulumu haki ya mtu basi ni kuirudisha hiyo haki.

Ikiwa utafuata masharti ya toba hayo kisha ukateleza na ukarudi kwa Allaah سبحانه وتعالى  Yeye Anakusamehe. Na kwa ile huruma, ukarimu, rehema na usamehevu Alionao Allaah سبحانه وتعالى  ni wa hali ya juu na Ataendelea kumsamehe mja wake maadamu atarudi Kwake kwa kutambua kuwa yupo Mola  wa kusamehe waja pindi wanapokosa. Hivyo, hakuna idadi maalumu isipokuwa inatakiwa kwa mwenye kuomba msamaha awe mkweli na mwenye nia nzuri, asiwe ni mwenye kumcheza shere Allaah سبحانه وتعالى na kwa hakika hatuwezi kwani Yeye anajua ya siri katika vifua vyetu na yaliyojificha zaidi kuliko siri. Ikiwa nia ni nzuri basi Naye Hutusaidia katika kujirekebisha katika hilo.

Ifahamike toba haitakubaliwa kwa wenye kurudia katika ukafiri mara kadhaa kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى  :

إ}}ِنَّ الَّذِينَ آمَنُواْ ثُمَّ كَفَرُواْ ثُمَّ آمَنُواْ ثُمَّ كَفَرُواْ ثُمَّ ازْدَادُواْ كُفْرًا لَّمْ يَكُنِ اللّهُ لِيَغْفِرَ لَهُمْ وَلاَ لِيَهْدِيَهُمْ سَبِيلاً{{



{{ Hakika walio amini, kisha wakakufuru, kisha wakaamini, kisha wakazidi ukafiri, Allaah hakuwa wa kuwaghufiria wala wa kuwaongoa njia}} 

An-Nisaa 4: 137

Wa Allaahu A'alam

 

Share