Kutuma Ujumbe Wa Makumbusho Ya Dini Kwa Kutishana Au Kubashiria

 

Kutuma Ujumbe Wa Makumbusho Ya Dini Kwa Kutishana Au Kubashiria

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalam alaikum

Miaka ya karibuni kumekuwa na tabia ya baadhi ya waislamu kutuma ujumbe kwa simu kwa wenzao unaotaja dua, dhikri fulani au mafundisho fulani kisha kuomba ujumbe utumwe kwa watu wa 5,7 au10 na utapata ulitakalo au utaona miujiza, na pia huongezea kwamba usidharau. Je nini ukweli wa jambo hilo? Naomba ufafanunuzi kwa faida ya wengi kwani nimepata msg nyingi katika simu yangu na nadhani si mimi tu.

Wabillahi tawfiq

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Tunamshukuru ndugu yetu kwa swali hili muhimu ambalo limeenea sana siku hizi kupitia katika simu za mikono na mtandao.

 

Kukumbushana mambo ya Allaah kama kupelekeana du'aa au dhikr na kadhalika ni jambo jema baina ya Waislamu kwani Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Anasema:

وَذَكِّرْ فَإِنَّ الذِّكْرَىٰ تَنفَعُ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٥٥﴾

Na kumbusha, kwani hakika ukumbusho unawafaa Waumini. [Adh-Dhaariyaat: 55] 

 

Ama kulazimisha mtu kufanya kitendo cha ibada kisichokuwa fardhi haifai. Kwanza inatupasa tutambue kuwa dini yetu haimlazimishi Muislamu kufanya kitendo zaidi ya zile fardhi alizofaridhiwa, anapofanya mtu zaidi hupata thawabu na asipofanya hapati dhambi.  Vile vile kumkirihisha mtu katika dini si jambo Alilotuamrisha Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa.

 

Hatari zaidi ya mas-alah haya ni kulazimisha mtu na kumtisha kwamba atume kwa watu  kiasi fulani na kama hakutuma mtu atapata khasara fulani au kubashiria kuwa pindi akituma atapata bahati fulani. Kwa mfano mtu anaweza kusema:  "Kama hukuutuma ujumbe huu basi utafikwa na msiba au mambo mabalaa mbali mbali na kama utautuma basi utafanikiwa katika siku tatu au kama hivyo."

 

Hakika haya ni mambo ya shirki na kufru  yaliyopita mipaka, kwasababu watu wanajaribu kujitia sifa za Uungu kuwa wanajua mambo fulani yatayotokea katika siku tatu au siku kumi na mbili na kadhalika.  Haya ni  mambo ya ghayb (yasiyoonekana).   Na elimu hii ya ghayb hakuna aijuaye isipokuwa Mwenyewe Rabb Mtukufu kama Anavyosema:

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ 

Na Kwake (Allaah) zipo funguo za ghayb; hakuna azijuaye ila Yeye tu. [Al-An'aam: 59]

 

Na Amesema Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aaliihi wa sallam katika Hadiythi iliyotoka kwa Ibn 'Umar Radhwiya Allaahu 'anhu.  

((مفاتح الغيب خمس لا يعلمها إلا الله: إن الله عنده علم الساعة، وينزل الغيث، ويعلم  ما في الأرحام، وما تدري نفس ماذا تكسب غدا، وما تدري نفس بأي أرض تموت، إن الله عليم خبير)) أحمد

"Funguo za ghayb [mambo yasiyoonekana au kujulikana] ni matano ambayo hakuna ayajuwae isipikowa Allaah.

 

"Hakika kuijua Saa (ya Qiyaamha) kuko kwa Allaah. Na Yeye Ndiye Anayeiteremsha mvua. Na Anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Allaah Ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari.” (Suwrah Luqmaan: 34). [Imesimuliwa na Imaam Ahmad].

 

Vile vile   Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Ametoa onyo kwa mtu mwenye kuingilia katika elimu yake ya ghayb.

أَطَّلَعَ الْغَيْبَ أَمِ اتَّخَذَ عِندَ الرَّحْمَـٰنِ عَهْدًا ﴿٧٨﴾كَلَّا ۚ سَنَكْتُبُ مَا يَقُولُ وَنَمُدُّ لَهُ مِنَ الْعَذَابِ مَدًّا ﴿٧٩﴾

Je, kwani ameyajua ya ghayb, au amechukua ahadi kwa Ar-Rahmaan?Laa, hasha! Tutayaandika yale anayoyasema, na Tutampanulia muda wa adhabu ya kurefuka.[Maryam: 78-79].

 

Kwa hiyo kama tunavyoona kuwa kuna hatari kubwa ya Muislamu kuingia katika kufru na shirk kwa kuingilia elimu ya ghayb ya Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa .  Na Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Anasamehe madhambi yote ila shirk.

 

Jambo muhimu kabisa ni kuwa ni wajib wa kila Muislamu anapopata ujumbe wa aina yoyote wa dini, kwanza ahakikishe usahihi wa huo ujumbe.  Kama ni Hadiyth basi Lazima Kwanza ahakikishe kama ni Hadiyth Sahihi au dhaifu, na kama ni Sahihi basi inafaa kuwapelekea wenzake kuwakumbusha bila ya kumtisha mtu au kumbashiria mtu faida ya kutuma huo ujumbe kuwa atapata faida fulani wakati Hadiyth yenyewe haikusema hivyo.  Na kama Hadiyth ni dhaifu basi ni wajib wake kumnasihi mwenzake aliyemtumia kuwacha kuituma na yeye pia asiitume kwa mtu yeyote ili kusimamisha uzushi kuenea kwa Waislamu wenzetu kwa hatari ya uzushi ni moto wa Jahannam kama alivyosema Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi aalihi wa sallam.

((من كذب علي متعمدا فليتبوأ مقعده من النار)) متفق عليه

"Atakayeniongopea makusudi basi ajitayarishie makazi yake motoni." [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

 

Na Allaah Anajua Zaidi 

 

Share