Hirizi Inafaa Kuvaliwa Kutibu Maradhi Ya Nafsi Na Jini?

 

 

 

Hirizi Inafaa Kuvaliwa Kutibu Maradhi Ya Nafsi Na Jini?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

Asallam allaikum natumai hamjambo, Swa langu ni mimi nilipwa na matatizo ya kuumwa na maradhi yasiyojulikana hospitali vipimo nilivimaliza,visomo nilisomewa sana na mimi mwenyewe kusoma lakini nilikuwa ni mtu wa kutulia tu na kulia lakini kwa baadae vilitulia na kurudi school kurudia darasa basi rehma zake Allaah [S.A.W] Mpaka nikamaliza kwa sasa nimeolewa huwa vinanitokea ninavyojisikia ni kukosa raha ya maisha[nafsi] na kupata kilio kikubwa sijui kinapotokea basi nikapelekwa kwa Maalim mmoja akanisomea na Kunipa Hazina Niwe Nakaa Nayo Je? Inafaa Au Ni Makosa?

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Ifahamike kuwa si magonjwa yote yanafahamika hospitali na magonjwa kama baridi kumpeleka mtu hospitali ni kumharibu kabisa.

 

Baadhi ya maradhi yanatibika kwa urahisi zaidi kwa kutumia matibabu ya kienyeji japokuwa kwetu Waislamu ni fani ambayo imekuwa kuanzia enzi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka wakati wetu huu hasa katika mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki na hata katika Bara Arabu.

 

Kukosa raha ya maisha huja kwa sababu nyingi mojawapo ikiwa pengine kutosikilizana na mume wako na kadhalika. Pia kutumia dawa au vitu ambavyo ni kinyume na sharia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na mojawapo ni kumshirikisha Allaah Aliyetukuka. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Hutupatia mitihani ambayo kama Waislamu tunatakiwa tupambane nayo kwa Imani na yakini sio kwenda kinyume na Aliyoamrisha. Kuhusu mitihani Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anatueleza:

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٥﴾

Na bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Na wabashirie wenye kusubiri. [Al-Baqarah: 155].

 

Ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Akatupatia dawa njema kwa haya yanayotukumba pale Alipotuambia:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٣﴾

Enyi walioamini! Tafuteni msaada kwa subira na Swalaah; hakika Allaah Yu pamoja na wanaosubiri. [Al-Baqarah: 153].

 

Subira inaleta tija iliyo kubwa nasi inafaa tuwe na sifa hiyo na tuwashinde wasiokuwa Waislamu katika hilo.

 

Tufahamu kuwa kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) ni dhulma iliyo kubwa, amali zote huharibika na ni dhambi ambalo halisamehewi na Allaah. Hayo ni kwa mujibu wa kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴿١١٦﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali. [An-Nisaa: 116].

 

Pia:

وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾

Na Luqmaan alipomwambia mwanawe huku akimuwaidhi: Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno! [Luqmaan: 13].

 

Miongoni mwa njia za shirki ni kupatiwa hazina na Maalim, Sheikh na wengineo ambao huwadanganya watu kwa kuwasomea kisomo cha uwongo kisha kuwapa hirizi wavae. Waalimu wa kweli wanasoma kile kisomo kilichosuniwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kuondosha kwa mtu ikiwa amekumbwa na jini au amefanyiwa uchawi. Mas-ala ya kutumia hazina au hirizi yamekatazwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hivyo kuwa haramu katika Dini yetu tukufu ya Uislamu.

 

Kuhusu hilo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatueleza:

 

"Mwenye kutungika hirizi hakika amefanya shirki" [Ahmad na al-Haakim, naye akaisahihisha).

Na kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Aliyetundika hirizi na mwenye kutungika azima basi Allaah Hamtimizii shida yake, na mwenye kutungika azima Allaah Hamuondolei alicho nacho"  [Ahmad na al-Haakim, naye akasema Isnadi yake ni sahihi].

 

Na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuona kipofu mmoja ana kitambaa kakifunga mkononi mwake cha njano:

 

"Kwa nini umefanya hivi?” Akasema: “Hii ni kutokana na ‘waahina’ tatizo lililonikuta". Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ivue kwani Allaah Hatakuzidisha ila matatizo tu na kama utakufa na hiyo iko juu yako basi hautafanikiwa milele" (Ahmad).

 

Kile ambacho kinajuzu kwako kufanya ni kujitibu kwa Ruqya (kisomo cha kisheria) ambamo hamna shirki ndani yake. Inatakiwa mwenye kukusomea awe atasoma zile Aayah na Surah ambazo ni tiba kwako au wewe mwenyewe mbali na kusoma surah na Aayah tofauti za Qur-aan lakini uwe ni mwenye kusoma zile Aayah ambazo zitakusaidia. Ndio katika hilo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia:

 

"Hakuna ubaya na Ruqya kama hakuna shirki" [Muslim].

 

Ikiwa kutakuwa na kisomo na shirki ndani yake kama ulivyofanyiwa itakuwa haifai. Ukitazama katika hirizi ambayo utakuwa umepatiwa hakuna kitu ndani isipokuwa karatasi isiyo na maandishi au karatasi iliyochorwa tu vitu au pengine kipande cha gazeti kama tulivyopata pindi tulipomtoa mtoto mmoja hirizi na kuifungua ndani yake.

 

Aayah ambazo zinaweza kukusaidia ni kusoma asubuhi na jioni Suwrah Al-Baqarah (2), Aayah 1-5, 255-257 na 284-286, Suwrah Al-Kaafiruun (109), Suwrah Al-Ikhlaasw (112) mara tatu, Suwrah Al-Falaq (113) mara tatu a Suwrah Al-Naas (114) mara tatu na zote ni kinga pamoja na du’aa nyingi ambazo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha na zinapatikana kwenye kitabu cha Hiswnul Muslim ambacho kiko katika ALHIDAAYA.

 

Tunamuomba Allaah Akuponyeshe wewe pamoja na Waislamu wengine wenye maradhi tofauti.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share