Binti Wa Mke Wangu Aliyekufa Sijui Kama Naruhusiwa Kumlea Au Nimpelekee Baba Yake?

SWALI:

 

Mke wangu alisilimishwa na kuolewa miaka kumi na nne iliyopita. Akajaaliwa binti mmoja miaka 14. Lakini ndoa yake na mumewe haikudumu wakatengana. Miaka mitano iliyopita nilimkuta mke wangu na tukafunga ndoa baada ya kuchukuwa talaka yake na mimi kuslimu. Ndoa yetu ikajaaliwa mtoto mmoja wa kiume na yule wa kike nimlea mimi mwenyewe hadi sasa. Sasa mke wangu amefariki, inawezekana mimi kuendelea kumlea binti yangu ama nimregeshe kwa babake kama anavyotaka babake? Baba ana watoto 4 na wake 2 kwa mda huu.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu malezi ya mtoto wako wa kambo.

Ama katika sheria ya Kiislamu pindi unapomuoa mke basi huwezi kumuoa binti yake. Hivyo, binti yako wa kambo ni Mahram wako kwa kuwa huwezi kumuoa na hivyo kumlea ni ihsani ambayo utakuwa unamfanyia na hivyo kuchuma thawabu nyingi kwa ajili hiyo.

 

Sasa ikiwa babake ni Muislamu kulingana na swali lilivyoeleweka, baba atakuwa na haki zaidi ya kumlea mtoto wake huyo.

 

Mbali na kuwa katika nchi zetu za Kiafrika baba kama huyo anaweza kwenda katika mahakama ya watoto kumdai na mahakama ikaamua kumpatia yeye.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share