Kutayarishwa Mihadhara Ya Kila Mwaka Inafaa?

SWALI:

 

Asalamu alekum swali yangu ni juu ya islamic conferences zina fanyika kila mwaka huku holland kuna watu wameleta uzushi kwamba conferences hizi ni bid'ah, wanasema kwa sababu inafanyika kila mwaka na hakuna dalili eti ni bid'ah, tafathali naomba jibu kuna conference inakuja ningependa kujua nifanyaje inshaALLAH, ASANTE.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu suala la kuandaa mihadhara na makongamano. Allaah Aliyetukuka Ametuumba sisi na kutupatia akili ya kuweza kutafakari. Tufahamu si kila jambo ambalo linafanyika ni Bid‘ah mbali na kuwa kilugha ni hivyo lakini sio kisheria.

 

Makongamano haya yanaingia katika yale malengo makuu ya kisheria, kuweza kueneza Dini na kufundisha watu ambao hawakupata mafunzo ya Uislamu au kutoa fatwa mbali mbali au pia kupatiana muelekeo au kupatikana faida nyengine. Hii ni njia moja ya kutafuta elimu na mbinu ya Da‘wah ambayo inawasilisha ujumbe kwa Waislamu. Lengo kubwa la wenye kukusanyika ni kupata elimu, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza sana Waislamu watafute elimu. Akasema yeyote anayetoka kutafuta elimu yu katika njia ya Allaah mpaka arudi.

 

Na Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

Wala haiwafalii Waumini kutoka wote. Lakini kwa nini hawatoki baadhi katika kila kundi miongoni mwao, wakajifunze vyema Dini, na kisha waje kuwaonya wenzao watakapo warejea, ili wapate kujihadharisha?” (9: 122).

 

Hapa tunaelezwa kuwa haifai kwa wote kwenda Jihadi bali ni lazima wabakie watu ambao watajifunza vyema Dini ili waweze kueneza ujumbe kutoka kwa Allaah Aliyetukuka. Tahadhari ni kuwa hayo makongamano yanayoandaliwa lazima muhakikishe kuwa mtapata mafunzo sahihi ya Uislamu. Lau ikiwa ni kwenda kuwapotosha katika njia sahihi basi haitawafalia kwenu kwenda hata kwa dakika moja, kwani kuna makundi mengi katika wakati huu na mengi yanadai yanahubiri Uislamu sahihi lakini kumbe ni kinyume chake.

 

Hivyo, hakuna tatizo la kuhudhuria conference ikiwa ni ya watu madhubuti wenye misimamo safi ya Qur-aan na Sunnah kwa ufahamu wa wema waliotangulia.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share