Inayosemekana Miujiza Inayorushwa Katika Barua Pepe Ni Kweli?

 

Inayosemekana Miujiza Inayorushwa Katika Barua Pepe Ni Kweli?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

A. Aleykum warahmatullah wabarakatu. Swali langu ni kama lifuatavyo: kuna picha zinapatikana katika internet mfano; msichana aliyegeuka mnyama (baada ya kuzidisha sauti ya mziki mamaye akisoma Qur'an), mtoto kazaliwa akiwa na jicho moja (isreal), mtoto wa miezi (mchanga) kupata mimba na matukio mengine ambayo husemekana ni miujiza kutoka kwa Allaah (s.w).Kuna watu wanasema kua hizi ni picha tu mtu anazitengeneza na kuziweka katika internet ilikuwakumbusha binaadamu na kuwaongeza imani. sasa je ni kweli? Na kama ni hivyo inaswihi kutumia udanganyifu kama huu katka mambo ya kheir? Natumai nitajibiwa kwa ufasaha zaidi. Natanguliza shukrani. Wahadha Asalaam Aleykum Warahmatullah Wabarakatu.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Nabiy, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'aalaa) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Nabiy. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Swahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

 

Lakini Tunatanabahisha kuwa tutahadharini sana tusije tukawa tunawadanganya watu, Waislamu na wasiokuwa Waislamu kwa sababu moja au nyingine.

 

Kabla ya kuingia katika maudhui yenyewe tungependa kugusia kuhusu mas-alah ya ukweli na uongo katika Dini yetu Tukufu.  Amesema Allaah Aliyetukuka:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَكُونُوا مَعَ الصَّادِقِينَ﴿١١٩﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah na kuweni pamoja na wakweli. [At-Tawba: 119].

 

Ikiwa Allaah Aliyetukuka Ametuamrisha kuwa na wakweli ina maana kuwa sisi pia tunafaa tuwe wakweli.  Na amesema tena Aliyetukuka:

وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ

Na wasemao kweli wanaume na wanawake, [Al-Ahzaab: 35]. 

 

Imepokewa kwa Ibn Mas‘uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika ukweli unamuongoza mtu katika wema na wema unampeleka mtu Peponi. Na hakika mtu huendelea kusema ukweli mpaka akaitwa mkweli mbele ya Allaah. Na hakika uongo inampeleka mtu katika uchafu na uchafu unampeleka mtu Motoni. Na mtu huendelea kusema uongo mpaka akaandikwa kuwa ni muongo mbele ya Allaah" [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy].

 

Na imepokewa kwa Abi Muhammad, Al-Hasan bin ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhuma), mjukuu wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na raihani wake (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kuwa alisema:

 

"Nimehifadhi kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Acha lenye kukutia shaka kwa lisilokutia shaka. Hakika ukweli ni utulivu na uongo unakera" [Ahmad, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy. Isnadi yake ni Swahiyh na ameisahihisha Ibn Hibbaan]. Amesema at-Tirmidhiy kuwa hii ni Hadiyth Hasan Swahiyh.

 

Na imepokewa kwa Abu Sufyaan Sakhr bin Harb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika Hadiyth ndefu kuhusu kisa cha Hiraql (Heraclius). Alisema Hiraql: "Je, anawaamuru nini (yaani Nabiy [Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam])?" Akasema Abu Sufyaan: "Nikasema, anasema: ‘Muabuduni Allaah peke Yake wala musimshirikishe Yeye na chochote na muache wanayosema wazazi wenu na anatuamuru kusimamisha Swalah na kusema ukweli, kuwa watwaharifu na kuunganisha kizazi (kwa kuwasaidia jamaa)" [Ahmad, Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Aayah na Hadiyth tulizozitaja zinatuhimiza kuwa wakweli na hiyo ndiyo sifa ambayo tunatakiwa sisi Waislamu tujipambe nayo. Baada ya kuhimizwa kuwa wakweli, tumakatazwa kabisa kusema uongo. Amesema Allaah Aliyetukuka:

وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾

Na wala usifuatilie usiyo na elimu nayo. Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitaulizwa. [Al-Israa: 36].

 

Na amesema tena Aliyetukuka:

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ﴿١٨﴾

Hatamki kauli yeyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha (kurekodi). [Qaaf: 18].

 

Imepokewa kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kuwaNabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Mtu yeyote akiwa na mambo manne atakuwa mnafiki hasa, na atakuwa na moja katika hayo manne atakuwa na sifa ya unafiki mpaka aliache: Kama akiaminiwa anaondoa uaminifu; na akizungumza anaongopa; na anapotoa ahadi ahadi huvunja; na anapogombana anaiacha haki na kuwa jeuri” [al-Bukhaariy na Muslim].

 

 Na imepokewa kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Mwenye kubuni ndoto mbaya ambayo hakuona, atalazimishwa Siku ya Qiyaama kufunga fundo baina ya mbegu za shayiri na hataweza. Na mwenye kusikiliza mazungumzo ya watu na wao wanachukia hilo, atamiminiwa risasi iliyoyeyushwa masikioni mwake Siku ya Qiyaama. Na mwenye kuchora picha ataadhibiwa na kukalifishwa kupuliza ndani yake uhai na hataweza kufanya hivyo" [al-Bukhaariy].

 

Na imepokewa kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Uongo ulio mkubwa zaidi ni kwa mtu kudai kuwa ameona kitu kwa macho yake ambacho hakukiona" [al-Bukhaariy]. Na maana yake ni kusema: “Kuona kitu ambacho hukuona”. Hizi Hadiyth mbili za mwisho zitunatupatia ufafanuzi mzuri sana wa uongo, ikiwa katika ndoto na kudai kuwa umeona kitu haifai seuze kusingizia kuwa kuna miujiza fulani na kumbe

Ama kuhusu miujiza Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ۗ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴿٥٣﴾

Tutawaonyesha Aayaat (ishara, dalili) Zetu katika peo za mbali na katika nafsi zao, mpaka iwabainikie kwamba hiyo ni haki! Je, haitoshelezi Rabb wako kuwa Yeye ni Shahidi juu ya kila kitu? [Fusw-swilat: 53].

 

Allaah Aliyetukuka Anatuletea miujiza ambayo inaeleweka na kila mmoja, Muislamu na asiyekuwa Muislamu kwa njia moja au nyengine bila kutaka taawili wala ufafanuzi. Miujiza kawaida ni kutujulisha kuwa yupo Allaah Aliyetukuka na kuturudisha katika njia Yake ili tupate ufanisi hapa duniani na Kesho Aakhirah.

 

Yapo mengi katika mtandao (internet) ambayo yanatiwa chumvi au yanaongezwa ili kuwadanganya ndani yake wanaadamu kwa kukusudiwa au kutokusudiwa. Ikiwa ni kwa kukusudiwa hayo yatakuwa ni madhambi mbele ya Allaah Aliyetukuka. Ama kwa yule asiyejua atakuwa hana makosa lakini pindi anapojua hilo haitakuwa sawa kwake kufanya hivyo.

 

Ama kuna nyingi ambazo ni uongo wa dhahiri kama yule msichana Oman aliyeikata kata na kuikanyanga Qur-aan naye akageuzwa hapo hapo. Na yule kijana ambaye amekuwa akiletwa sana katika mtandao (internet) kwa sababu ya kuzaliwa na jicho moja na watu wakadai ni Dajjaa! Sijui tutakuwa na madajali wangapi kwani wapo wengi wenye kuzaliwa na kasoro kama hiyo. Na kuzusha hayo kuna madhara mengi makubwa kwani huyo mtoto ni mtoto wa mzazi fulani na mzazi wake kama ulivyo wewe, hatopenda mtoto wake azuliwe sifa chafu kama hiyo ya kuitwa Dajjaal! Ajiulize huyo mwenye kueneza mambo kama hayo, je, angekuwa huyo ni mtoto wake, angeridhia hayo??

 

Ama mtoto mchanga aliyepata mimba, sio mimba kama walivyoelezea madaktari bali ni kuwa mzazi (mama) alikuwa ana watoto pacha lakini mmoja akawa yuko ndani ya tumbo la nduguye mdogo. Na huu ndio muujiza wenyewe kwani Allaah Aliyetukuka Anaumba Anavyotaka. Ni hakika kuwa zipo picha nyingi zinazotengenezwa kuhofisha watu warudi kwa Allaah lakini hiyo sio njia ya sawa. Qur-aan ndio uongofu na inatakiwa iwaongoze watu, Qur-aan tunaisoma lakini haituongozi tuje tuongozwe na hivi vya udanganyifu, hiyo kwa hakika itakuwa ni ajabu na hata inaweza kutuingiza katika shirki.

 

Ama Kuhusu picha za vitu vya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), hakuna dalili yoyote inayohusiana na kuweko vitu vyake. Mwenye kusambaza hayo anapaswa  atoe dalili kwanza kama kutaja Swahaba gani waliohifadhi vitu hivyo? Na vipi wameweza kuvihifadhi hadi kuwafikia Taabi’iyn hadi kutufikia sisi? Bila ya dalili hizo, itakuwa ni kumzulia uongo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) jambo halipasi bali ni hatari kwani ni kujitayarishia makazi ya moto kama tulivyoonywa katika dini. Juu ya hivyo mambo kama haya ya vitu, hayatuongezei iymaan zetu au amali zetu, bali ni mambo ya kutushughulisha na kupotezeana muda kupelekeana mabarua pepe, muda ambao kila mmoja angeliweza kuutumia kwa kufanya ibada ya kujichumia thawabu tele.

 

Binaadamu anatakiwa aongozwe na ukweli sio uongo na huenda hii ikawa ni njia ya kuzidi kuwaepusha watu na haki. Sababu ni kuwa mtu ambaye ameanza kushika njia ya haki kwa sababu ya uongo, akija gundua kuwa alidanganywa, basi anaweza kuacha kila kitu na hiyo itakuwa inarudisha nyuma haki.

 

Kwa muhtasari ni kuwa ikiwa ni uongo basi itakuwa haifai kutumia njia hiyo kwani ulinganizi katika Uislamu una njia zake na unasimama juu ya ukweli na haki.  Na daima muhakikishe munawatahadharisha hao wanatuma mambo yasiyo na uhakika wala dalili waache tabia hiyo na muwafahamishe makemeo ya kusema uongo na kuueneza.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share