Kulisha Masikini Sitini

SWALI:

Asalamu Alaykum,

Ikiwa mtu analisha masikini 60 jee mtu huyo anakuwa kafanya nini mbele ya Allah? Naomba ufafanuzi wako


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Amma ba'ad,

Kulisha masikini kwa idadi yoyote ni amali njema na Allaah سبحانه وتعالى Amesisitiza sana katika Qur-aan kulisha masikini na atakayefanya hivyo basi atapata thawaabu zake.  

Ama idadi ya kulisha masikini 60 haikutajwa kuwa khaswa ina fadhila fulani ila tu imekuja hukumu  ya Kafara ya 'Adh-Dhwihaar' ambayo inatoka katika neno la 'Adh-Dhwahr' yaani mgongo. Ilikuwa katika zama za Jaahiliyyah (zama za ujinga, kabla ya Uislamu) mume humuambia mkewe "Umekuwa kwangu kama mgongo wa mama yangu". Na ilikuwa ndio njia mojawapo ya kutoa Talaka wakati huo.Na Allaah سبحانه وتعالى Ameruhusu Ummah huu wa Kiisalmu kulipa Kafara kwa kauli hii na haihesabiki kama ni talaka kinyume na ilivyo katika Ujaahiliyyah.

Kafara hii imetajwa katika aya zifautazo ambazo ziliteremshwa baada ya Bibi Khuwaylah bint Tha'alabah kumshtakia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kwamba mumewe 'Aws bin As-Swaamit amemwambia kauli hiyo ya Adh-Dhwihaar :

 

((قَدْ سَمِعَ اللَّهُ قَوْلَ الَّتِي تُجَادِلُكَ فِي زَوْجِهَا وَتَشْتَكِي إِلَى اللَّهِ وَاللَّهُ يَسْمَعُ تَحَاوُرَكُمَا إِنَّ اللَّهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ ))

 (( الَّذِينَ يُظَاهِرُونَ مِنكُم مِّن نِّسَائِهِم مَّا هُنَّ أُمَّهَاتِهِمْ إِنْ أُمَّهَاتُهُمْ إِلَّا اللَّائِي وَلَدْنَهُمْ وَإِنَّهُمْ لَيَقُولُونَ مُنكَرًا مِّنَ الْقَوْلِ وَزُورًا وَإِنَّ اللَّهَ لَعَفُوٌّ غَفُورٌ))

((وَالَّذِينَ يُظَاهِرُونَ مِن نِّسَائِهِمْ ثُمَّ يَعُودُونَ لِمَا قَالُوا فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مِّن قَبْلِ أَن يَتَمَاسَّا ذَلِكُمْ تُوعَظُونَ بِهِ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ))

((فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ شَهْرَيْنِ مُتَتَابِعَيْنِ مِن قَبْلِ أَن يَتَمَاسَّا فَمَن لَّمْ يَسْتَطِعْ فَإِطْعَامُ سِتِّينَ مِسْكِينًا ذَلِكَ لِتُؤْمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَتِلْكَ حُدُودُ اللَّهِ وَلِلْكَافِرِينَ عَذَابٌ أَلِيمٌ))

 

((Allaah Amekwisha sikia usemi wa mwanamke anayejadiliana nawe juu ya mumewe, na anamshitakia Allaah. Na Allaah anayasikia majibizano yenu. Hakika Allaah ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona))

 

((Wale miongoni mwenu wanaowatenga wake zao, hao si mama zao. Hawakuwa mama zao ila wale waliowazaa. Na hakika hao wanasema neno linalo chusha, na la uwongo. Na Allaah ni Mwenye kughufiria, Mwenye kusamehe)).

 

((Na wale wanaojitenga na wake zao, kisha wakarudia katika yale waliyoyasema, basi wamkomboe mtumwa kabla hawajagusana. Mnapewa maonyo kwa hayo. Na Allaah anayajua yote mnayo yatenda.

 

((Na asiyepata mtumwa kumkomboa, basi na afunge miezi miwili mfululizo kabla hawajagusana. Na asiyeweza hayo basi awalishe masikini sitini. Hayo ni hivyo ili mumuamini Allaah na Mtume wake. Na hiyo ndiyo mipaka ya Allaah. Na kwa makafiri iko adhabu chungu))

Al-Mujaadalah :1-4

 

Wa Allaahu A'alam

 

 


Share