Nani Muhimu Kumhudumia Katika Ugonjwa Mama Au Mke?

 

SWALI:

 

Asalam aleikum, kuna ndugietuwa na muislam ametokezewa na matatizo ya maradhi ambayo imembidi kupelekwa hospitali kubwa na kufanyiwa operation.

Suala langu ni kua huyu bwana kutokezewa na tatizo kama hili nani ni muhimu wa kuanae karibu na kumshughulika akiwa hapo hospitali wakati wa matibabu. Ikiwa anae mkewe na watoto wake ambao ndio wanaishi pamoja. na pia maana yakutaka kujua nani muhimu baina ya mama au mke katika hali kama hii ni kua mamake mume alimwambia mkewe huyu bwana kua hana umuhimu wa kua hapo hospital muhimu ni yeye (mama). Basi nakuomba unijibu suala hili kwa uwezo wa ALLAAH namna kwamba na watu wengine wafahamu umuhimu wa mume na mke na pia mama juu ya mtoto wake akiwa ashaolewa au ashaowa.

 

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu huduma anayohitajia mume katika ugonjwa wake. Uislamu haukuacha jambo lolote ila umetuelezea ili tusipate utata aina yoyote tunapokabiliana na tatizo au shida yoyote ile.

 

Ama kuhusu swali lako kila mmoja kati ya mama na mke wana jukumu kwa mgonjwa wao. Na hili si suala la kuteta wala kubishana kati ya hao wawili bali wanaweza kushirikiana kwa njia nzuri kwa wepesi wa mgonjwa. Kila mmoja kati yao ana hiswa yake. Bila shaka mume na mke wanaingiliana kwa kiasi kikubwa zaidi hata kuliko mama. Yapo mambo kijana wa kiume atakuwa anaona hayaa kufanyiwa na mama baada ya kubaleghe. Lakini mke huwa ana ruhusa ya sheria ya kuona kila kitu cha mumewe hivyo kumfanya yeye iwe ni rahisi kumhudumikia.

 

Hata baada ya hayo tuliyoyasema, Uislamu pia unatazama maslahi ya kila mmoja katika wanaadamu. Hapa hivyo, tunatazama maslahi ya mgonjwa. Haitakuwa maslahi ikiwa mama na mke watakuwa wanashindana au kuzozana, hivyo itakuwa afadhali kila mmoja wao amhudumie mgonjwa kwa mpangilio fulani. Kwa mfano, mke atamhudumia usiku na mama asubuhi au kinyume chake ili mwanzo kila mmoja apate hisia ya kuwa amemsaidia mgonjwa na mgonjwa naye apate kupona kwa njia nzuri zaidi kwa ushirikiano huo.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Ampe shifaa mgonjwa na kuwepo uelewano baina ya mama na mke katika kumhudumia mgonjwa wao.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share