Inafaa Kwenda Kwa Shaykh Amuombee Du’aa Ya Kupata Mume?

 

Inafaa Kwenda Kwa Shaykh Amuombee Du’aa Ya Kupata Mume?

 

 

 

 

SWALI:

 

Salam aleikum, ndugu zangu waislamu mimi ni mschana wa kiislam na napenda kuolewa, je nikienda kwa sheikh kuombewa dua ili Allah anifungulie rizki yangu, ntakua nimemshirikisha Allah. Tafadhali naomba mnisaidie nifanye nini

 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho 

 

 

Du’aa ni ‘Ibaadah kama anavyotueleza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyonukuliwa na at-Tirmidhiy. Kwa kuwa Du’aa ni ‘Ibaadah ni vyema kila mmoja ajiombee mwenyewe kwani mtu mwenyewe ndiye mwenye kujijua. Na kuna wakati ambapo Muislamu akiomba Du’aa anakuwa ni mwenye kujibiwa. Nyakati zenyewe ni kama:

 

  1. Wakati mtu yuko katika Swawm.
  2. Wakati wa kufungua Swawm.
  3. Mmoja anapokuwa amesafiri.
  4. Baina ya Adhaana na Iqaamah.
  5. Unapoinuka usiku kwa ajili ya kuswali.
  6. Unapokuwa katika Sijdah.
  7. Kwenye kikao cha tahiyyaatu kabla ya kutoa salaam.
  8. Siku ya Ijumaa kuna saa ya kujibiwa nyakati za Al-‘Aswr.

 

Kwa faida ziada bonyeza kuingo kifuatacho:

 

11-Wewe Pekee Tunakuabudu: Nyakati, Mahali Na Hali Za Kutakabaliwa Du'aa

 

Na pia haikatazwi kuwa unapokuwa na rafiki, jamaa au wazazi kuwaomba hasa wanapokuwa wanasafiri wakuombee. Hilo lilifanywa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa anasafiri, akamwambia ewe ndugu yetu: “Usitusahau kwa Du’aa.”

 

Kwa muhtasari, ni vyema uwe unaomba mwenyewe kwa lile unalotaka na bila shaka Allaah ('Azza wa Jalla)     Anasikia Du’aa ya kila mmoja wetu na yako pia ataisikia na kukujibu kama Anavyosema:

 

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share