Nabiy 'Iysaa (عَلَيْهِ السَّلام) Ametabiriwa Katika Qur-aan Kuja Kwa Nabiy Muhammad (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم)?

 

SWALI:

 

 

 

Mimi naitwa *********** wa mbweni Zanzibar napenda kuuliza swali langu kwamba hivi kuna ukweli wowote kwamba yesu (nabii Issa) alibashiria (alitabiri) juu ya ujaji wa nabii Muhammad s.w.a kupitia Biblia na Quran na kama upo naomba mnifafanulie.

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu utabiri wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Nabii 'Iysa (‘alayhis Salaam) katika Qur-aan na Biblia. Tufahamu kuwa utabiri huu hautoki kwa Nabii 'Iysa (‘alayhis Salaam) bali ni wahyi kutoka kwa Allaah Aliyetukuka. Hilo si la ajabu kwani Mitume waliokuja baada ya wengine walitabiri ujio wao. Ama Qur-aan iko wazi kabisa kuhusu hilo na Biblia nayo mbali ya kuwa ni mchanganyiko wa vitabu vingi lakini baadhi ya maneno ya Allaah Aliyetukuka yamebaki.

 

Ama Qur-aan inatuambia:

"Na wakumbushe aliposema 'Iysa bin Maryam (kuwaambia Mayahudi): Enyi wana wa Israili! Mimi ni Mtume wa Allaah kweni, nisadikishaye yaliyokuwa kabla yangu katika taurati, na kutoa habari njema ya Mtume atakayekuja nyuma yangu ambaye jina lake Ahmad. Lakini alipowajia kwa hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni udanganyifu ulio dhahirini" (61: 6). Ahmad ni jina jingine la Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama iliyokuja katika Hadiyth sahihi.

 

 

Ama mabaki ya Biblia kuna utabiri mwingi wa hilo. Hilo ni lazima liwe hivyo kwani Allaah Aliyetukuka Anatuambia: "Ambao wanamfuata Mtume, Nabii aliye ummiy (asiyejua kusoma wala kuandika), ambaye wamemuona ameandikwa kwao katika Taurati na Injili…" (7: 157). Hakika ni kuwa si Nabii 'Iysa tu aliyetabiri ujio wake bali Mitume wengine wengi. Hebu tutizame vifungu vifuatavyo:

 

 

  1. "Mtawala wa ulimwengu huu anakuja" (Yohana 14: 30).

 

  1. "Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu atawafundisheni kila kitu na kukumbusheni yote niliyokuambieni" (Yohana 14: 26).

 

 

  1. "Yeye ni roho wa ukweli" (Yohana 14: 16).

 

  1. "Afadhali mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu" (Yohana 16: 7).

 

 

  1. "Atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu" (Yohana 16: 8).

 

  1. Atawaongozeni katika ukweli (Yohana 16: 12 – 13).

 

 

  1. Ufalme wa Mungu utachukuliwa kutoka kwa Mayahudi na kupatiwa taifa litakalozaa matunda (Mathayo 21: 43).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share