Kudhihirisha Kisomo Cha Baadhi Ya Aayah Kwa Sauti Kwenye Swalaah Zisizo Za Sauti

SWALI:

 

Nimeshuhudia Imaamu kwenye  Swalaa ya Adhuhuri na Al-'Asri akidhihirisha kisomo cha Aayaat kama mbili hivi, katika Rak'ah mbili za mwanzo.

Nini hukmu ya jambo hili Baaraka Allaahu fiykum.

 


JIBU:

 

بسم الله الرحمن الرحيم 

Sifa zote njema na za ukamilifu zinamstahiki Allaah Rabb wa walimwengu wote, Swalaah na Salaam zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) Na waliowafuata hao kwa wema mpaka siku ya mwisho.

 

Bila ya shaka inafaa katika Shariy'ah Imaam kuwasikilizisha Maamuma Aayah moja au mbili au sehemu ya Aayah katika baadhi ya nyakati katika Swalaah ya Adhuhuri na Al-'Asr kutokana na mapokezi yaliyothibiti juu ya hilo kupitia Hadiyth aliyoipokea Al-Imaam Al-Bukhaariy na Muslim katika Swahiyh zao mbili kutoka kwa Swahaba Abuu Qataadah Al-Haarith bin Rib'iy (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema:

“Alikuwa Nabii wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa 'alaa aalihi wa sallam) akisoma katika Rakaa mbili za mwanzo katika Swalaah ya Adhuhuri na Al-‘Asr Suwrat Al-Faatihah na Suwrah nyinginezo na alikuwa akitusikilizisha Aayah mara nyingine. [Swahiyh Al-Bukhariy (762) na Muslim (451).]

 

Kuhusu Neno (alikuwa akitusikilizisha Aayah mara nyingine), amesema Al-Imaam Mulla 'Aliy Al-Qaariy (Rahimahu Allaah):

“Amesema At-Twiybiy maana yake alikuwa akiinua sauti yake kwa kuyasoma baadhi ya maneno katika Suwrat Al-Faatihah na Suwrah nyingine kiasi kwamba anasikika kwa hicho akisomacho mpaka hufahamika ni Suwrah gani anaisoma.”

[Mirqaatul-Mafaatiyh, Juz. 2 uk. 688]

 

 

Amesema Ibn Hajar (Rahimahu Allaah):

“Kusikika katika baadhi ya maneno kwenye Rakaa mbili za mwanzo katika Swalaah ya Adhuhuri na Al-'Asr kumetokana na wingi wa mazingatio yake wakati anapoisoma Qur-aan akiwa katika Swalaah hadi anafikia kudhirisha baadhi ya maneno au Aayah bila kukusudia, au anafanya hivyo ili apate kubainisha kuwa inafaa kudhihirisha Aayah au baadhi ya maneno katika usomaji ndani ya rakaa hizo. Au anafanya hivyo ili awafahamishe watu kuwa huwa anasoma Suwrat Al-Faatihah na Suwrah nyingine katika Rakaa mbili hizo za mwanzo katika Adhuhuri na Al-'Asr pia kuwasikilizisha baadhi ya maneno na Aayah ili watu wamuige katika hilo.”

Mwisho wa kunukuu.

 

Amesema Al-Imaam Ibn Al-Jawziy (Rahimahu Allaah) akiizungumzia kauli (Na alikuwa akitusikilizisha Aayah mara nyingine):

“Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa 'alaa aalihi wa sallam) akifanya hivyo katika baadhi ya nyakati kwa kuwa ili iwe kufanya hivyo hakuitoi Swalaah katika asili yake kuwa ni ya siri na si ya Jahri.”

[Kashful-Mushkil, Juz. 2, uk. 142]

 

Aliulizwa Al-Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah):

 

Swali:

Hivi inafaa nikadhihirisha kisomo katika Swalaah isiyokuwa ya kudhihirisha?

 

Jibu:

Sunnah ni kusoma siri katika Swalaah ya siri lakini lau akidhirisha baadhi ya Aayaat si vibaya kwani alikuwa Mtume akiwasikilizisha Maswahaba Aayah  baadhi ya nyakati katika Swalaah ya Adhuhuri na Al-‘Asr lakini bora katika Adhuhuri na Al-'Asr ni kusoma kwa siri na katika Swalaah za usiku ni kusoma kwa kudhihitisha na katika Swalaah ya Alfajiri pia.

[Fataawa Nuurun 'Alaa Ad-Darb, Juz. 8, uk. 224-225]

 

 

Na amesema Al-Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu  Allaah) akielezea hikmah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa 'alaa aalihi wa sallam) kuwasikilizisha Swahaba baadhi ya maneno au Aayah katika Swalaah ya Adhuhuri na Al-‘Asr ima ili awafahamishe kuwa alikuwa akisoma Qur-aan baada ya Suwrat  Al-Faatihah, au awazindue kwa kwa namna fulani kwa sababu Imaam anapodhihirisha kisomo katika  Swalaah  ya  siri  basi watu huzinduka.

[Liqaau Al-Baabi Al-Maftuwh, juz. 6, uk. 101]

 

Tunatumai kwa Tawfiyq ya Allaah hapo tutakuwa tumejaribu kulijibu Swali lako.

 

Wa Allaahu A'lam.

 

Share