Kuwatii Viongozi Wasio Waislamu Ikiwa Anaishi Nchi Za Kikafiri Inajuzu?

SWALI:

 

Salaam alykum,

 

Je, ni nini nafasi ya asiekua Muislamu katika jamii ya Kiislam? Je na katika ile aya isemayo mtiini MWENYEZI MUNGU na MTUME WAKE na waliono madarakani, je kama hao walio madarakani si Waislam inakuaje? Ahsante

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuwatii wasio Waislamu walio madarakani. Asli ya utii ni kwa viongozi ambao ni Waislamu kwani Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

"Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye mamlaka juu yenu, walio katika nyie (Waislamu)" (4: 59).

 

Hapa tunaelezewa kuwa wenye kutiiwa ni Waislamu wanaosimama imara katika kutekeleza sheria za Allaah Aliyetukuka hapa duniani. Hakika ni kuwa Waumini wamepatiwa dhamana kuwa watatawala dunia. Lakini endapo tutakuwa tuko kinyume na dhamana hiyo ni kuwa bado hatujafikia daraja ya Imani ya kuweza kufikia hilo.

 

Katika hali hiyo inakuwa ni dharura walio katika madaraka kutiiwa kwa sababu ya udhaifu wetu. Hivyo, inatakiwa tujiandae kwa ‘Ibaadah na kukuuza Imani zetu ili tufikie katika daraja hiyo inayohitajika. Hata hivyo, inatakiwa kila Muislamu afahamu kuwa utiifu kwa yeyote hasa kiongozi akiwa Muislamu au asiye Muislamu una mipaka. Hiyo ni kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam):

"Hakika utiifu ni katika wema". (Al-Bukhaariy na Muslim).

 

Na pia, "Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba". (Ahmad).

 

Ikiwa amri inayotolewa ni katika maasi hapo hafai kutiiwa kwa hali yoyote ile. Na ikiwa ni kutii katika sheria za nchi ambazo umechukua agano nao ambazo haziendi kinyume na sheria ya Kiislamu basi ni wajib wako kutii na kutimiza ahadi, kwani haya ni mafunzo katika Qur-aan na Sunnah kutimiza ahadi hata kwa asiye Muislamu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share