Kwa Nini Waislamu Tukiswali Tunaelekea Qiblah?

 

Kwa Nini Waislamu Tukiswali Tunaelekea Qiblah?

 

Alhidaaya.com

 

 

 SWALI:

 

Mimi swali langu; Kwa nini waislamu tunaelekea kibla wakati wa ibada zote?

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Mwanzo tunapenda kurekebisha kauli yako kuhusu ibara inayosema, “Waislamu tunaelekea Qiblah wakati wa ‘Ibaadah zote”. Ibara hii si kweli kwani Ibaadah ambayo Waislamu wanaelekea Qiblah ni Swaalah peke yake. Ama zipo ‘Ibaadah nyengine ambazo hazipaswi kuelekea Qiblah unapozitekeleza; mfano:

 

Kukidhi haja ndogo au kubwa kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuongoza hayo kama ilivyothibiti katika Hadiyth zifuatazo:

 

عَنْ سَلْمَانَ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: {لَقَدْ نَهَانَا رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏ "أَنْ نَسْتَقْبِلَ اَلْقِبْلَةَ بِغَائِطٍ أَوْ بَوْلٍ، أَوْ أَنْ نَسْتَنْجِيَ بِالْيَمِينِ، أَوْ أَنْ نَسْتَنْجِيَ بِأَقَلَّ مِنْ ثَلَاثَةِ أَحْجَارٍ، أَوْ أَنْ نَسْتَنْجِيَ بِرَجِيعٍ أَوْ عَظْمٍ"} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Salmaan (Radhwiya Allaahu 'anhu)  amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alitukataza kuelekea Qiblah wakati wa kwenda haja kubwa au ndogo, wala tusijisafishe kwa mkono wa kulia, au kujisafisha kwa mawe yasiyotimia matatu, au kujisafisha kwa kinyesi cha wanyama au mfupa.” [Imetolewa na Muslim]

 Na pia,

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 لَا تَسْتَقْبِلُوا اَلْقِبْلَةَ بِغَائِطٍ وَلَا بَوْلٍ، وَلَكِنْ شَرِّقُوا أَوْ غَرِّبُوا}

“Usielekee Qiblah wakati unakwenda haja kubwa au ndogo, lakini geukia Mashariki au Mgharibi.” [Hadiyth ya Abuu Ayyuwb imekharijiwa na imaam Saba]

 

 

‘Ibaadah ya Swawm, Zakaah, Hijjah, Jihaad, kufanya kazi, kusoma si lazima uelekee Qiblah.

 

 

Lakini ufahamu na ibara hii imekuja kwa ule muono wetu finyu kuwa Ibaadah ni Swalaah peke yake. Ifahamike kuwa ‘Ibaadah katika Uislamu ni kila jambo la halaal unalolifanya ili kupata Radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa). Ukifanya jambo hilo unapata thawabu. Hivyo, zimekuja Hadiyth kutufahamisha kuwa hata kustarehe na mkeo ni aina ya ‘Ibaadah na unapata thawabu kwayo [Muslim].

 

 

Sasa labla tukija katika mas-ala ya Swalaah na kuelekea Qiblah ni kuwa hili ni agizo kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na mtihani kwetu. Je, katika amri hii tutakuwa ni wenye kusitasita au vipi? Muislamu ni yule ambaye amejisalimisha kabisa kwa Allaah ('Azza wa Jalla)  na pindi anapopatiwa amri anakuwa ni mwenye kuitii bila ya wasiwasi wa aina yoyote.

 

 

Hakika ni kuwa kuelekea sehemu fulani katika maombi au ‘Ibaadah fulani au zote ni jambo ambalo linaeleweka sana na Waislamu na wale waliokuwa Waislamu lakini wakapotosha vitabu vyao kama Mayahudi na Manaswara. Hili lipo wazi katika maandiko na halina utata. Hebu tutazame baadhi ya Aayah za Qur-aan zinazozungumzia jambo hilo.

 

 

Waislamu walikuwa wanaelekea Al-Quds kabla ya kuhamia Madiynah na baada ya hapo waliendelea kuelekea huko kwa muda wa miezi 16 au 18 kabla ya kubadilishwa Qiblah na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) kuelekea al-Ka‘bah au Msikiti Mtukufu wa Makkah. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

 

قَدْ نَرَىٰ تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاءِ ۖ فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْلَةً تَرْضَاهَا ۚ فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِۚ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّوا وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ ۗ وَإِنَّ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ لَيَعْلَمُونَ أَنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ ۗ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا يَعْمَلُونَ ﴿١٤٤﴾

Kwa yakini Tumeona (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) unavyogeuza geuza uso wako mbinguni. Basi Tutakuelekeza Qiblah unachokiridhia. Basi elekeza uso wako upande wa Al-Masjidil-Haraam. Na popote mtakapokuwepo (mkataka kuswali), basi elekezeni nyuso zenu upande wake. Na hakika wale waliopewa Kitabu bila shaka wanajua kwamba hivyo ni haki kutoka kwa Rabb wao. Na Allaah si Mwenye kughafilika kwa wayatendayo. [Al-Baqarah; 144]

 

 

Anasema tena Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa):

 

وَمِنْ حَيْثُ خَرَجْتَ فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ ۚ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّوا وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ  

Na popote utokako (ili kuswali) basi elekeza uso wako upande wa Al-Masjidil-Haraam. Na popote mtakapokuwa basi elekezeni nyuso zenu upande wake.  [Al-Baqarah: 150]

 

 

Mayahudi waliokuwa Madiynah walipiga makelele sana kuhusu kubadilishwa Qiblah. Qur-aan iliwarudi kuwa sehemu zote ni za Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa), Naye ndiye pekee Mwenye kuweka Qiblah kwa mtu mwenye kuswali. Tafadhali tazama Suwrah Al-Baqarah (2: Aayah 142 – 143)

 

 

Hao wajinga walisema: “Bila shaka, Swalah za Waislamu kwa miaka yote iliyopita zimepotea na hawatapata thawabu zozote, kwani hazikufanywa kwa kuelekea katika Qiblah kilicho sahihi”. Akajibu Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa):

 

وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُضِيعَ إِيمَانَكُمْ ۚ

Na Allaah Hakuwa Mwenye kupoteza iymaan yenu (Swalaah) [Al-Baqarah: 143]

 

Kumaanisha Swalaah zenu zilifanywa katika Qiblah kilicho kuwa sahihi kilichoridhiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa).

 

Ibara hii hapa ni muhimu sana, Anaposema Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa):

 

وَإِنَّ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ لَيَعْلَمُونَ أَنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ ۗ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا يَعْمَلُونَ ﴿١٤٤﴾

Na hakika wale waliopewa Kitabu bila shaka wanajua kwamba hivyo ni haki kutoka kwa Rabb wao. Na Allaah si Mwenye kughafilika kuhusu wayatendayo. [Al-Baqarah: 144]

 

 

Nao pia walikuwa wakielekea sehemu fulani walipokuwa katika maombi yao lakini baada ya kubadilishwa Qiblah walikataa hilo japokuwa wanaelewa vyema kuwa hiyo ni haki.

 

 

Jambo hili la kuelekea sehemu fulani katika maombi linatekelezwa hata na baadhi ya makabila yanayofuata dini za kitamaduni. Mfano hai ni Wakikuyu wanaoishi Kenya ambao wanaelekea mlima Kenya. Huzuni ni kuwa waliopewa Vitabu walibadilisha maandiko ili kukidhi maslahi na matashi ya binafsi, lakini hakika hii wanaijua zaidi ya watoto wao.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share