Mwanafunzi Anasoma Kwa Mkopo Wa Serikali; Je, Anaweza Kwenda Hajj Na Hali Ana Deni Hilo?

 

Mwanafunzi Anasoma Kwa Mkopo Wa Serikali; Je,

Anaweza Kwenda Hajj Na Hali Ana Deni Hilo?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Assalaam aleykum,

 

Mimi ni mwanafunzi niliepewa mkopo na serikali. Mkataba wangu na serikali ni kurudi nikawatumikie na niwalipe pesa waliyonipa. Niko nje ya nyumbani; na huku Alhamdulillah kuna waislam hutokezea wakanigiya pesa au kuninunulia vitu ambavo nahitaji alhmadulillah. Likizo hii nimebahatika kupata kazi ya halali na nahisi nitabarruk kwa kuwaangalia wazee kidogo, nitoe sadaka na nijaribu kumsaidia mwanafunzi mmoja ambae ni yatima huko nyumbani. Suala langu ni: je natakiwa nisitoe pesa nilionayo mpaka nimalize deni? Na hata nikitaka kuhijji baadae hili deni litanizuia? Nasikia uchungu kua deni si dogo na mimi nataka kusaidia na nikipata nafasi nikahiji kwa pesa za halali nitazopata.

 

Natanguliza shukrani,

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika ni kuwa pindi unapokopeshwa na taasisi au mtu binafsi huwa mnaandikiana au mnakubaliana jinsi ya kulipa deni hilo. Baada ya makubaliano hayo inabidi ufanye juhudi ya kuweza kutimiza ahadi hiyo kila mwaka au mwezi au kama mlivyoagana na kukubaliana.

 

Ikiwa baada ya kulipa hilo deni utaweza kuwa na akiba ambayo itakuwa ni halali yako unaweza kufanya lolote. Kwa akiba hiyo unaweza ukawa unaweka kila mwezi kwa ajili ya kwenda Hijjah, kuwasaidia wazazi au yatima au kufanya shughuli yoyote nyingine ya halali bila tatizo lolote.

 

Jambo ambalo lililokatazwa ni wewe kuchukua mkopo kwa ajili ya kwenda Hijjah.

 

Ama ikiwa yule anayekudai deni lake akakubali kuwa ulicheleweshe kwa sababu kama hizo na akaridhia wewe badala ya kumlipa deni lake, uende kufanya Hijjah kwanza, basi kwa makubaliano hayo hakuna neno kufanya hivyo.

 

Na kwa faida yako, mikopo mingi wanayopewa wanafunzi na serikali mbalimbali huwa ina ribaa, na kwa hali hiyo ni haraam mtu kujiingiza kwenye mikopo ya namna hiyo.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share