Mwanamke Kumfanyia Hijjah Mtu Mwengine Bila Yeye Kuwa Na Mahram Haifai

 

Mwanamke Kumfanyia Hijjah Mtu Mwengine Bila Yeye Kuwa Na Mahram Haifai

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Assalam Aleikum,

 

Nina suali moja ntafurahi sana mukinijibu haraha kabla sijachukua hatua zangu. Mimi ni Mwanamke ambae nimeshafanya hajj mara kadha sasa ninataka kwenda kumfania mtu Hajj na huyo mtu hajawahi kwenda na mimi sina mahrim wangu kufuatana nae jee hi hajj itafaa? Na nitaweza kwenda bila ya mahrim.

 

Shukran Jazakalahu Kheri.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Mwanamke haimpasi kusafiri bila ya Mahram wake, na hata katika kutekeleza ibada ya Hijjah, baadhi ya Maulamaa wameweka sharti kuwa lazima mwanamke awe ana Mahram wake ndio aweze kwenda kutekeleza fardhi hii. Kwa hiyo ikiwa kuna sharti ya kuwa na mahram katika ibada ya fardhi anayojitendea binafsi mwanamke, seuze iwe ni ibada kwa ajili ya kumfanyia mtu mwingine. Hadiyth ifuatayo imeelezea kuhusu makatazo hayo:

 

 قالَ صلى الله عليه وسلم  : (( لا تُسافِرِ المرأةُ إلاَّ معَ ذي مَحْرَمٍ)) رواه البخاري ومسلم

Amesema Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwanamke asisafiri ila awe na mahram wake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kutokana na Hadiyth hiyo ambayo inaonyesha kuwa ni haraam kwa mwanamke kusafiri bila ya mahram, Maulamaa wengi wametoa rai kuwa kuwa na mahram ni moja ya sharti ya kuifanya Hajj kuwa imewajibika kwa mwanamke. Na mwanamke mwenye nia ya kutekeleza Hajj lakini ameshindwa kwa sababu hiyo hupata thawabu kutokana na nia yake In shaa Allaah.

 

Vile vile:

 

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhuma) amesema amemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Asikae faragha mwanamme na mwanamke isipokuwa awe na mahram yake wala asisafiri mwanamke ila awe na mahram wake pia”. Akasimama mtu mmoja na kuuliza: “Ee Rasuli wa Allaah! Mke wangu ametoka kwenda kuhiji nami nimejiandikisha kwenda kwenye vita vya Jihaad kadhaa”. Akajibu: “Nenda ukahiji pamoja na mke wako” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) Aliulizwa kama iliwajibika Hajj kwa mwanamke aliyekuwa tajiri ambaye hakuwa na mahram. Alijibu: "Hapana". [Al-Mughniy 3/97] 

 

Kwa hiyo haifai kwenda kufanya kwa ajili ya mtu mwingine ila kama utakwenda na mahram wako. Ukitaka kupata thawabu sawa na hizo madam unao uwezo, basi ni vizuri kumlipia gharama hizo Muislamu mwanaume aliyekwishafanya Hajj kabla ili akamtimizie fardhi hiyo ya huyo unayetaka kumfanyia, na hilo ni jambo jema litakalokupatia thawabu vilevile In shaa Allaah.  

 

Bonyeza hapa kusoma jibu la maudhui kama hiyo:

 

Hijja Yake Imekubaliwa Ikiwa Amekwenda Bila Ya Mahram?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share