Kumlipia Gharama Za Hijjah Mwanamke Aliyekuwa Na Mahusiano Naye Yasiyo Halali

 

Kumlipia Gharama Za Hijjah Mwanamke Aliyekuwa Na Mahusiano Naye Yasiyo Halali

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Kuna mwanamke ambaye aliwahi kuwa rafiki yangu wa kimapenzi zaidi ya miaka 20 iliyopita ambaye nimeonana nae hivi karibuni. Mwanamke huyu kwa sasa ameolewa na msalihina (saalihiina) na khamsa salawatu. Kwa sasa hatuna mahusiano yoyote zaidi ya yaliyopita na wala hatuna nia ya kuanzisha mengine kwani sote sasa ni watu wazima na tunafata maaelekezo ya dini na tumetubia kwa yaliyotokea hapo nyuma. Shida yake ni kwenda Hija atimize.

 

Nguzo hii muhim ya dini. Mimi kwa nia moja na bila ya tarajio lolote zaidi ya thawabu kutoka kwa Allah nimeweka nia ya kumlipia gharama za kwenda Hija. Jee nikimlipia hija yake itasihi? Jee mimi sitokuwa nimetenda dhambi nikifanya hivyo?

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kuwapa uongofu ndugu zetu walioingia katika makosa Akawaajalia ni wenye kupenda kutenda mema badala yake kama ndugu yetu muulizaji. Na kutukabili kuuliza jambo lenye utata ni ishara kuwa mna khofu kubwa ya kuingia katika makosa mara nyingine. Hii ni Neema kwenu  hivyo inapasa kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa kukuonyesheni njia ya kuzidi kupata uongofu  ili msiwe mnafanya yale yasiyomridhisha.

 

Swala lako ni lenye utata kwa sababu kadhaa zifuatazo ambazo nyingine tunaziweka kwa mfumo wa maswali.

 

Kwanza: Msaada wenyewe una uhusiano wa historia yenu ya urafiki wa kimapenzi ambao sio urafiki wa halali kwani bila ya shaka utakuwa ulihusiana na maasi. Na kama tunavyojua kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hapokei jambo ila lililo zuri kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((إنَ الله تعالى طَيِّبٌ لا يَقْبَلُ إلا طَيِّباً)) رَوَاهُ مُسْلِمٌ

((Allaah ni Mwema na Hakubali ila kilicho chema tu)) [Muslim]

 

Pili:

 

Japokuwa mmeshaacha urafiki huo na wote mmeshatubu, lakini kuwasiliana naye kwa njia yeyote ile bila ya kujua mumewe na kuwa naye faraagha ni makosa makubwa:  

 

قال صلى الله عليه سلم : ((لا يخلوّنّ أحدكم بامرأة إلا مع ذى محرم )) متفق عليه

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hawi faraagha mmoja wenu pamoja na mwanamke ila awepo Mahram wake)) [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

 

Hivyo haitokuwa ni kutubu kikweli ipasavyo, kwani uhusiano baina yako na huyo mwanamke unaendelea japokuwa unahisi kuwa hakuna chochote lakini uhusiano huo unaweza kurudisha ushetani uliokuweko kabla. Tambueni kwamba hizo ni hila na njia za Shaytwaan kukuvutieni katika maasi: 

 

Ametuonya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ وَمَن يَتَّبِعْ خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ فَإِنَّهُ يَأْمُرُ بِالْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ ۚ 

Enyi walioamini! Msifuate nyayo za shaytwaan; na yeyote yule atakayefuata nyao za shaytwaan basi hakika yeye anaamrisha machafu na munkari. [An-Nuwr: 21]

 

Tatu: 

 

Je, umemjulisha mumewe kwamba unataka kumfanyia jambo la kheri mkewe? Na je, mumewe anajua kuwa nyinyi mlikuwa marafiki wa kimapenzi kabla ya kumuoa yeye huyo mke? Tuna shaka kama anajua hivyo kwani hatudhani kama atakubali baada ya kujua historia yenu. Kwa hivyo, hapo hapo utakuwa umepata jibu kuwa mnayofanya ni ya siri kwa sababu si sahihi na si halali. Hilo tu latosha kukuonyesha kuwa hamjaelewa maana halisi ya tawbah.

 

Nne:

 

Kwanini asiende na mumewe? Atakwendaje Hijjah bila ya Mahram wake? Ikiwa mume wake haendi kwani kama angekuwa anakwenda basi angemlipia na mkewe, na ikiwa ni mke pekee anataka kwenda na hana uwezo basi fahamuni kuwa mume anastahiki kujua njia za kumwezesha mkewe kwenda huko, na pia rukhusa ya mume ni muhimu, na kwenda mwanamke peke yake bila Maharimu ni makosa, na kuwa na Maharimu ni uwezo wa kwenda Hijjah, na akikosa Maharimu wa kusafiri naye, basi mjue kuwa haikumpasa bado nguzo ya Hijjah kwake kwani kuwa na Maharimu (Mahram) ni sharti mojawapo ya kuwa uwezo wa njia ya kwenda kutekeleza fardhi hiyo kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

 

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ 

Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. [Al-'Imraan: 96]

 

Na pia makatazo ya mwanamke kusafiri peke yake bila Mahram wake yameshawekwa wazi kwenye Sunnah kama anavyotujulisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((لا يحل لامرأة مسلمة تسافر مسيرة اليوم وليلة إلا مع ذي حرمة منها))

((Haimpasi mwanamke Muislamu kusafiri msafara wa mchana na usiku ila awe na Mahram)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Naye huyo mwanamke, madamu hana uwezo wa njia basi asitake kushikilia sana kutekeleza ibada kwa kuasi amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na Nabiy Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), bali nia yake inamtosheleza kulipwa na Rabb Mtukufu. Tunafahamu kuwa bila ya shaka atakuwa na hamu kubwa ya kutaka kutekeleza ibada hiyo labda awe na matumaini kuwa atafutiwa madhambi yake yote. Lakini itambulike kuwa mja hufutiwa madhambi yake yote ya maasi anapotubu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hata kama hakwenda Hajj.   

 

Kwa hiyo mas-alah haya sio ya kwamba utapata dhambi kumlipia gharama za Hajj, bali ni mashaka ya kutokukubaliwa Hijjah yake kutokana na sababu hizo. Na kuacha yale yenye mashaka ni bora kuliko kufanya yenye mashaka kama ambayo wewe unataka kuyafanya.

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anatuonya hayo:

   

عَنْ أَبي مُحمَّدٍ الحسَنِ بْنِ عليّ بْنِ أبي طَالِب، سِبْطِ رَسُولِ اللهِ صلى الله عليه وسلم وَرَيْحَانَتِهِ رضيَ اللهُ عنهُما، قالَ: حَفِظْتُ مِنْ رَسُولِ الله صلى الله عليه وسلم: ((دَعْ ما يَرِيبُكَ إلى مَا لاَ يَرِيُبكَ )) رَوَاهُ التِّرْمِذِيُّ وَالنَّسَائِيُّ وَقَالَ التِّرْمِذِيُّ: حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ. 

Kutoka kwa Abu Muhammad Al-Hasan bin ‘Aliy bin Abi Twaalib mjukuu wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kipenzi chake (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) alisema: ((Nilihifadhi kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) maneno haya: ((Acha kile kinachokutia shaka ufuate kile kisichokutia shaka)) [At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy, At-Tirmidhiy akisema kuwa ni Hadiyth Hasan na Swahiyh]

 

Tunakunasihi ukate mawasiliano na mahusiano yote baina yako wewe na huyo mwanamke ambaye si Mahram yako na haipasi kisheria  kuwasiliana na mke wa mtu. Lazima ujue kuwa Tawbah ya kweli ni kujuta kikamilifu kwa yale uliyoyatenda na kutolirejea tendo hilo kwa njia yoyote ile hata kama ni kwa fikra njema ya kutaka kumlipia gharama za Hajj.

 

Tunakushauri  kuwa ikiwa wewe bado hukutekeleza nguzo hiyo, basi utumie gharama hizo kwenda kuifanya Hajj.  Na ikiwa umeshafanya Hajj, basi nenda kamhijie mzazi wako ikiwa ameshafariki. Na kama bado wazazi wako wangali hai, basi msaidie ndugu yako ambaye hajakwenda. Au vilevile unaweza kuwasaidia mayatima kwa gharama hizo. Na mengi yako ya kufanya yatakayokuingizia thawabu au Sadaka yenye kuendelea kuliko kumlipia mke wa mtu kwenda Hajj.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Azidi kuwaonyesha uongofu, Awazdishie taqwa, Awaghufurie nyinyi na sisi na Waislam wote na Atuongoze sote kwenye njia ya sawa; njia iliyonyooka; njia ya Rusuli, Mashahidi, wema waliopita na wasema kweli. Aamiyn

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share