Du’aa Gani Asome Ili Apate Mume Wa Kheri?

Du’aa Gani Asome Ili Apate Mume Wa Kheri?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalam Aleikum,

 

Kwanza nawapongeza sana kwa website yenu, ni nzuri sana na inatusaidia sana kwa sisi vijana tuliokuwa mda mwingi kazini. Inanipa faraja sana kujua kuwa kila nnapotaka kusoma dua yoyote au kusikiliza naweza kuingia humu.

 

Lakini naomba niwaulize swali moja linalonisumbua siku nyingi sana. Sasa najiuliza, hivi kuna dua yoyote kubwa inayopaswa kuisoma kama mwanamke anaetafuta mume ambae ni wa kheri kwake?

 

Asante sana

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika ni kuwa hatujapata kuona wala kusikia Du’aa kama hiyo. Hata hivyo, kukosekana Du’aa ya moja kwa moja haimanishi kuwa ndio basi, bali zipo njia nyingi za kufanikisha hilo.

 

 

Swali linaweza kuja kwa nini basi hakuna Du’aa ya kupata mume wa kheri? Jibu kwa swali hili ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuambia:

 

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye ametuelezea nyakati ambayo Du’aa inakuwa ni yenye kukubaliwa kwa urahisi kabisa. Hivyo, inabidi ujitume ili kufikia hilo kwa kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Akufanikishie hilo. Katika baadhi ya nyakati ambamo Du’aa zinakubaliwa ni:

 

  1. Baina ya Adhaana na Iqaamah.
  2. Thuluthi ya mwisho ya usiku ambamo utainuka uswali Tahajjud, na humo uombe.
  3. Ukiwa katika sijdah ndani ya Swalaah.
  4. Siku ya Ijumaa baina ya Khutbah mbili.
  5. Baada ya Alasiri siku ya Ijumaa na kabla kuchwa jua.
  6. Uwe ni mwenye kula, kunywa, kuvaa vya halaal na uwe ni mwenye kumridhisha Allaah ('Azza wa Jalla).  
  7. Wakati unapokuwa safarini.
  8. Wakati unapokuwa uko katika Swawm ya  faradhi (Ramadhaan) au ya Sunnah. Hivyo, jaribu kujikurubisha kwa Allaah kwa kufunga Jumatatu na Alkhamiys na uombe du’aa ukiwa katika hali hiyo ya Swawm.
  9. Kabla hujatoa Salaam ndani ya Swalaah.

 

Bonyeza pia kiungo kifuatacho upate faida nyenginezo tele:

 

يَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ - Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

Fanya bidii usome hizo Makala ufaidike na ufuate mwongozo huo wa Du’aa za kumuomba Allaah ('Azza wa Jalla) Naye Atakupa mwenye kheri na mswalihina kwa Uwezo Wake, wala usikate tamaa katika hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share