Zingatio: Faida Ya Milele

 

Zingatio: Faida Ya Milele

 

 

 Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Mtumwa anapomtumikia bwana wake huwa hana budi kutekeleza amri zote. Juu ya hivyo, atakapoambiwa ya kwamba utumwa wake unamalizika baada ya kumtumikia bwana, basi atafanya juhudi zake kumridhisha matakwa yake ili apate uhuru wake.

 

 

Maisha yetu duniani yanahitaji kufuata kanuni zote za Muumba bila ya kuzibagua. Kwani faida ya kumtumikia Rabb Mlezi ni ya milele. Ni jambo la kuliweka ndani ya moyo. Hapo ndipo litakapotupa msukumo wa kutenda mema na kuepuka maovu.

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaaa) ni Mwenye Rehema hakuna zaidi yake. Kwa mama aliyepotelewa na mwana, furaha yake ipo chini ikilinganishwa na furaha Anayokuwa nayo Allaah pale mja wake anapoomba toba. Yeye Ndiye Mwenye kusamehe madhambi yetu.

 

 

Tupige hisabu ya umri tunaotumia hapa duniani. Baadaye tulinganishe na miaka ya wazee wetu waliotangulia mbele ya haki. Nani hapa aliyekula chumvi zaidi? Bila ya shaka yoyote kwamba waliotangulia mbele ya haki wameshatumia dahri za miaka na miaka.

 

 

Tuwe na uchungu wa mfanyabiashara. Ambaye huwa na bidii kuchuma mali bila ya kujali msimu wa biashara. Anakuwa ni mbunifu na laini mbele ya mteja wake. Wala hajiwekei dharura zisizo na msingi. Kwani anaelewa kuwa dharura hizi zitamsababishia kukosa faida.

 

 

Waswahili tuna msemo: "Hiari yashinda utumwa". Diyn yetu tukufu ni ya kunyenyekea kwa Muumba katika hali zote. Kuanzia kuzaliwa kwetu hadi mauti yanapotukuta. Na huo unyenyekevu wetu una malipo makubwa Siku ya Hisabu. Malipo ambayo yatapita juhudi ya mfanyabiashara.

 

 

Basi ni nani aliyekosa akili ya kuzaliwa kuielewa pesa? Hata aliye mtoto au asiye na akili anaelewa faida ya pesa. Basi tuelewe kwamba pesa haina thamani kuliko unyenyekevu wetu kwa Muumba. Kwani kuna malipo makubwa hapa duniani, wakati wa kukata roho, katika maisha ya barzakh, kisimamo cha Hisabu na hatimaye malipo ya Jannah:

 

تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ ۚ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١٣﴾

Hiyo ni mipaka ya Allaah. Na yeyote atakayemtii Allaah na Rasuli Wake Atamuingiza Jannaat zipitazo chini yake mito, watadumu humo, na huko ndiko kufuzu kukubwa. [An-Nisaa: 13]

 

Bia ya kusahau kwamba malipo ya Jannah yanatokana na kipindi kifupi cha maisha yetu hapa duniani. Sasa piga hesabu ya maisha ya miaka mia. Lakini faida ya kumnyenyekea Rabb ni mara nyingi zaidi! Kwani malipo yake ni zaidi ya miaka alfu, ni yenye kuendelea milele.

 

 

 

Share