Zingatio: Iogope Siku Hii

 

Zingatio: Iogope Siku Hii

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Ni ukosefu wetu wa kumbukumbu na dharau ndizo zinatupelekea kukosa nidhamu mbele ya Ukubwa wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) pamoja na vile Alivyoviumba. Yareti kama mwanaadamu atakaa kuzingatia Ukubwa wa Yule Muumbaji, katu hatakhasirika kwa kukosa rahma za Rabb Mlezi.

 

Allaah(Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametueleza kwa kina viumbe vyake vya Moto na Jannah ndani ya Qur-aan. Viumbe ambavyo vitashuhudiwa siku ya Qiyaamah macho kupe kupe. Watakaoingia Motoni watayaona mashaka yake na wale watakaorehemewa kuingia Jannah wataziona neema zake. Allaah Atujaalie miongoni mwa wenye kupata neema za Jannah.

 

Basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatutahadharisha kuhusu Siku hiyo:

 

 وَاتَّقُوا يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللَّـهِ ۖ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٢٨١﴾

Na iogopeni Siku mtakayorejeshwa ndani yake kwa Allaah, kisha kila nafsi italipwa kamilifu iliyoyachuma nao hawatodhulumiwa. [Al-Baqarah: 281]

 

Hiyo ndio Siku ambayo mimi na wewe sote tutaishuhudia, namna ambavyo mwanaadamu atashuhudia kifo chake. Jee umepata kufikiria hisabu yako itakavyokuwa Siku hiyo? Watakaonufaika na neema za Rabb wao ni wale waliomcha na kutenda mema hapa duniani kwa ikhlaasw ya hali ya juu. Ama wale ambao wamegeuka tumbili kwa kukosa muongozo, watakiona cha mtema kuni.

 

Basi ndugu yangu Muislamu kumbuka kwamba hapo awali hukuwa chochote. Unamuonesha nani kibri chako hali ya kuwa wewe utakufa. Ee nafsi... nafsi... Rudi kwa Rabb wako kabla ya muda kuisha. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

أَوَلَا يَذْكُرُ الْإِنسَانُ أَنَّا خَلَقْنَاهُ مِن قَبْلُ وَلَمْ يَكُ شَيْئًا ﴿٦٧﴾ فَوَرَبِّكَ لَنَحْشُرَنَّهُمْ وَالشَّيَاطِينَ ثُمَّ لَنُحْضِرَنَّهُمْ حَوْلَ جَهَنَّمَ جِثِيًّا ﴿٦٨﴾ ثُمَّ لَنَنزِعَنَّ مِن كُلِّ شِيعَةٍ أَيُّهُمْ أَشَدُّ عَلَى الرَّحْمَـٰنِ عِتِيًّا ﴿٦٩﴾

Je, hakumbuki insani kwamba Tulimuumba kabla, na hali hakuwa chochote? Basi Naapa kwa Rabb wako. Bila shaka Tutawakusanya wao na mashaytwaan, kisha Tutawahudhurisha pembezoni mwa Jahannam wapige magoti. Kisha bila shaka Tutawachomoa katika kila kundi wale ambao waliomuasi zaidi Ar-Rahmaan. [Maryam: 67-69]

 

Aayah zinazofuatia hapo ni nzito zaidi, kwani zinaeleza kwamba sote tutaingia Motoni:

 

وَإِن مِّنكُمْ إِلَّا وَارِدُهَا ۚ كَانَ عَلَىٰ رَبِّكَ حَتْمًا مَّقْضِيًّا ﴿٧١﴾ ثُمَّ نُنَجِّي الَّذِينَ اتَّقَوا وَّنَذَرُ الظَّالِمِينَ فِيهَا جِثِيًّا ﴿٧٢﴾

Na hakuna yeyote miongoni mwenu, isipokuwa ni mwenye kuufikia (moto). Hiyo ni hukumu ya Rabb wako; lazima itimizwe. Kisha Tutawaokoa wale waliokuwa na taqwa, na Tutawaacha madhalimu humo wamepiga magoti. [Maryam: 71-72]

 

Lakini rahma za Allaah ni kubwa na hakika Atawanusuru wale waliokuwa wakimukhofu hapa duniani kwa siri na dhahiri na Atawaacha waovu wakiwa wenye kukhasirika:

 

ثُمَّ نُنَجِّي الَّذِينَ اتَّقَوا وَّنَذَرُ الظَّالِمِينَ فِيهَا جِثِيًّا ﴿٧٢﴾

Kisha Tutawaokoa wale waliokuwa na taqwa, na Tutawaacha madhalimu humo wamepiga magoti. [Maryam: 72]

 

Wahenga walinena: ‘Ukimuona mwenzio ananyolewa, wewe tia maji’. Jitayarishe na Siku hiyo kwa kutenda mema sio kumuasi Rabb al-Jabbaari Ambaye adhabu na ghadhabu Zake Hazina mfano wa kitu chochote. Nakuusia usigeuke ngo’mbe aliyekata kamba, kwani kamba aliyofungiwa ilikuwa na maana na faida kwake. Halikadhalika kwako Muislamu, Qur-aan usiikimbie kwani ina faida na maana yake juu yako. Kuwa chini ya Shariah ya Rabb sio juu ya Shariah, utaangamia.

 

 

 

Share