Mashairi: Twawapenda Aali Bayti

 

                    Muhammad Faraj Salim As-Sa’ay

                              

 

Ndugu yangu hebu keti

usikiye nisemayo

Andika kila ubeti

wa maneno ninenayo

Uchukuwe na sileti

na kalamu uwe nayo

Hikaya za Aali Bayti

nyumba ya tumwa Nabiya

 

 

Nyumba ya tumwa Nabia

nuru ilikochomoza

Ikaangaza  dunia

huku ikituongoza

Tukaifahamu njia

hako wa kutupotoza

Hikaya za Aali Bayti

nyumba ya tumwa Nabiya

 

 

Wao wametoka kwake

maimamu na Khalifa

Ni watu wa nyumba yake

walopata kila sifa

Waume kwa wanawake

hekima na maarifa

Hikaya za Aali Bayti

nyumba ya tumwa Nabiya

 

 

Isomeni Quruani

mupate kuyafahamu

Yote yamo humo ndani

maneno Yake Karimu

Kwa mapenzi na hisani

ataka tuwakirimu

Hikaya za Aali Bayti

nyumba ya tumwa Nabiya

 

 

Ali Hasani Huseni

Fatwima na dada zake

Muttalibi si wageni

wote ni aila yake

Hawa wote wa nyumbani

pamoja na wake zake

Hikaya za Aali Bayti

nyumba ya tumwa Nabiya

 

 

Wakeze ni wetu mama

hayo kasema Manani

Neno Lake kaditama

halifutwi asilani

Haishi ila na wema

Hamadi kwake nyumbani

Hikaya za Aali Bayti

nyumba ya tumwa Nabiya

 

 

Wakeze ni wetu mama

Aali Bayti nao piya

Sifa mbili zote njema

ni tunuku la Jaliya

Ni daraja na rehema

za akhera na duniya

Hikaya za Aali Bayti

nyumba ya tumwa Nabiya

 

 

Wote sisi twawapenda

Rabbi Mola Shuhudiya

Kwa maneno na kutenda

Uloridhi twaridhiya

Sisi hatufanyi inda

huyu towa huyu tiya

Hikaya za Aali Bayti

nyumba ya tumwa Nabiya

 

 

Swala baraka salamu

mfikishie Nabiya

Mbora wa wanadamu

mola Ulomswaliya

Na Aali Bayti kiramu

na Swahaba zake piya

Hikaya za Aali Bayti

nyumba ya tumwa Nabiya

 

Share