Mashairi: Iblisi, Shetani, Jini

 

             ‘Abdallah Bin Eifan

           (Jeddah, Saudi Arabia)

 

Salaam kwa Wafuasi, wa yetu tukufu dini,

Naomba Mola Mkwasi, izidi yetu imani,

Atuepushe maasi, na balaa duniani,

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

Majini wapo na sisi, lakini hatuwaoni,

Hututia wasiwasi, hao ndio mashetani,

Mkubwa ni Iblisi, ameshika usukani,

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

Msujudie Adamu, kaambiwa na Manani, (Al-Baqarah: 34)

Kawa na kichwa kigumu, kagoma kuwa kundini,

Akamlaani Rahimu, iblisi maluuni,

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

Kaumbika iblisi, kwenye moto unawaka,
Na hapo atajilisi, motoni atachomeka,
Adui wetu halisi, lazima kumuepuka,

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

Kutoka kwenye udongo, binadamu kaumbika, (Twaahaa: 55)
Atarudia udongo, mauti yakimfika,
Atoke kwenye udongo, wakati wa kufufuka,

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

Adamu kahadaika, alipokuwa peponi,

Hakika kadanganyika, kawa hana shukurani,

Mwishowe akaokoka, aliomba samahani,

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

Wapo wanatuandama, njiani na majumbani,

Tuendapo wapo nyuma, hata tuende chooni,*

Wapo wametusakama, ardhini na angani,

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

Huwaoni wakichoka, daima wapo mbioni,

Wapo wanashughulika, watutie mtegoni,

Pale tukishaanguka, wanakuwa furahani,

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

Mabaya hufanya mema, hutupambia machoni,

Mpaka siku ya Qiyaama, sisi na wao vitani,

Tuone mwisho wa "drama," ataeshinda ni nani?

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

Tazama hii dunia, itakwisha karibuni,

Tupo tunapita njia, hapa tupo safarini,

Shetani katuwania, tupo kwenye mitihani,

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

Kwa hivyo tusome sana, kuna kinga vitabuni,**

Si usiku si mchana, tusisahau jamani,

Kuna dua utaona, uisome mlangoni,***

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

Usiku unapofika, ukipanda kitandani,

Kuna aya husomeka, uikariri kichwani,****

Ndipo utapookoka, salaama u salimini,

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

 

Na Tumuombe Jalali, shetani tukiwahisi, (Al-Muuminuun : 97-98)

Tuwe nao mbalimbali, kama kanga na mkasi,

Shairi hapa kamili, naichana karatasi,

Tupo nao mashetani, majini na iblisi.

 

 

Bonyeza Hapa Chini:

*Dua'a Ya Kuingia Chooni
   Dua'a Ya Kutoka Chooni

 

** Hiswnul Muslim
***Dua'a Ya Kuingia Nyumbani

       Dua'a Ya Kutoka Nyumbani

 

**** Nyiradi Za Kulala

 

 

Share