Kudanganya Kuogopa Ghadhabu Za Mkewe Kwa Ajili Ya Kuoa Mke Wa Pili Inafaa?

SWALI:

 

Asalaam alaykum,

 

Kuna ndugu yangu anataka kuolewa mke wa pili, ila huyo mwanaume kamuapia mkewe hatooa tena baada ya mkewe kujua ila kuzuia ugomvi katika nyumba yake, kwa kifupi kamdanganya maana bado anamwambia ndugu yangu  bado anampenda na atamuoa na anamwambia uwongo kama huo unaruhusiwa katika dini maana anataka kufanya jambo la kheir, na mkewe akijua kama bado anataka kuoa tamletea taabu, Je ni sawa kuapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kuwa hautaoa mke mwingine na wakati mtu anayo nia ya kuoa kafanya hivyo kwa kuepuka matatizo ya nyumbani kwake? Fiamanillah.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu udanganyifu. Uongo ni jambo ambalo limekatazwa sana kwa kiasi kuwa Allaah Aliyetukuka Ametuagizia tuseme ukweli na tuwe na wakweli. Anasema Aliyetukuka: “Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na kuweni pamoja na wakweli” (9: 119).

 

Uislamu umehimiza sana ukweli na kukataza uongo na udanganyifu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Mwenye kutudanganya si katika sisi” (Muslim).

 

Inafaa mtahadhari sana na mtu kama huyo kwani huenda akawaingiza katika janga ambalo litawatia taabu kutoka kwayo. Inafaa nawe umtahadharishe dadako asiwe ni mwenye kuingia katika mtego huo. Awe ni mwenye kusubiri na InshaAllaah atapata mwengine mwenye kheri naye. Leo kadanganywa mwenzake na kesho atadanganywa yeye.

 

Uongo unaruhusiwa tu katika hali maalum kama katika kusuluhisha watu waliokhasimiana au wanandoa wanaotaka kuachana, na si katika suala hilo ambalo halihitaji uongo katu. Vilevile kuapa kwa jina la Allaah katika mambo ya uongo au ya kipuuzi ni dhambi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share