Skip to main content

Mashairi: Ya Habibi Ya Nabiya

Yaa Habibi Yaa Nabiya

Muhammad Faraj Salim As-Sa’ay (Rahimahu Allaah)

Maka ulikozaliwa, Madina ukapokewa

Kwa mashada ya mauwa, Yaa Habibi ya Nabiya

Maka ilikochomoza, Nuru ya Mola Muweza

Madina ikaangaza  kisha kote kueneya

Ulikuja na Risala, kutoka Kwake Ta’alaa

isomwe kila mahala, kila pembe ya duniya




 

Ni Risala kamilifu, Yake Mola Mtukufu

aso mwana wala kufu, yenye kunawiri njiya

Yote ukayatimiza, hapana ulichosaza

tena bila kupunguza, kamili kutufikiya

Ukatufunza Shahada,akhlaqi na ibaada

na kutoa misaada, kwa wenye kuhitajiya



Allahu katakasika, Mola Aso mshirika

ni Shahada ya hakika, na wewe wake Nabiya


 


Hiyo ndiyo ya awali, alotufunza Rasuli

ni nguzo iliyo ghali, nyoyoni mwetu jamiya


 


Swala akatufundisha, Asubuhi hadi Isha

zote twazikamilisha, nyakati zikiingiya



Twaziswali kwa wakati, kwa ikhilasi na dhati

tena bila hatihati, Ya Rabbi takabaliya



Kisha tutowe na Zaka, wakati unapofika

kwa hesabu kila mwaka, nisabu ikitimiya



Ilitiliwa mkazo, tajiri na walo nazo

tugawe bila vikwazo, tuwape wahitajiya





Kisha kutoa sadaka, hiyo kama tukitaka

mali inatakasika, na kurudisha afiya



Kuhiji Maka ni nguzo, kwa kila mwenye uwezo

hiyo haina mchezo, yataka kuipaniya



Kaaba nyumba tukufu, nyumba kongwe takatifu

hapo lazima utufu, shoti saba kutimiya



Nyumba hiyo ipo Maka, ni mji wenye baraka

Dhambi hapo hufutika, Mola Ametuambiya

Arafati ndiyo Hija, huko nako kwakungoja

kwake aliye Mmoja, dua zinaelekeya

Siku hiyo ikifika,  watu tena patashika

machozi yamiminika, wakiomba na kuliya



Labeka Rabi labeka,  Mola Uso mshirika

Arafati tumefika,  Nawe watushuhudiya

Mwenye Sifa ya Uluwa, La ilaaha illa Huwa

ziwe zitakavyokuwa,  dhambi utatufutiya

Uturudishe tukiwa,  kama tulivyozaliwa

ndivyo tulivyoambiwa, na Muhammadi Nabiya



Kisha Mina siku tatu, wanakusanyika watu

wanapiga Jamaratu,  na kuchinja Adhuhiya


Yabaki shughuli moja, hiyo pia yakungoja

ni shoti saba za Hija, Tawafu na Sayi piya

Safari ikishafika,  ukataka kuondoka

usibaki hapo Maka Widaa itabakiya

Hiyo ni tawafu moja, ukesha moja kwa moja

Hapana tena kungoja Garini utaingiya

 



Hizo ndizo nguzo zake, na hiyo Risala yake

kutoka kwa Mola wake, ni amana ya Jaliya



Ni nzito kweli kweli, Ilikataa jabali

wewe ukaikubali, kubeba ukairidhiya





Mola Amekuhitari,  mbele ya wote bashari

uifikishe habari, kwa jini na insiya

Anachokitaka huwa, Mwenyewe kakuchaguwa

kwa sababu akujuwa,  kipenzi chake Nabiya

 



Mwenye khuluqa adhimu, mpole tena karimu

kwa uma wake rahimu, kuliko kila Nabiya

Ni mwenendo mtukufu, ulotimu kamilifu

mkweli muaminifu mwenye sifa maridhiya



Mfano wa Quruani,  inotembea njiani

kakufundisha Manani, utukufu wa tabiya