Mashairi: Shisha Imekuwa Mtindo

 

 Shisha Imekuwa Mtindo

 

              ‘Abdallah Bin Eifan

              (Jeddah, Saudi Arabia)

 

 

Salamu kwa Waumini, zifike kila makani,

Natoa yangu maoni, nikikosa samahani,

Huku ndugu Arabuni, madhara hawaioni,

Shisha(1) sasa ni mtindo, nchi zote Arabuni.

 

Zunguka kila pahali, zunguka mikahawani,

Hata hupati mahali, wamejazana vitini,

Kusogea hakubali, ameshatanda mezani.

Shisha sasa ni mtindo, nchi zote Arabuni.

 

Hata upige kinanda, ataesikia nani?

Wamechacha kina dada, wamejaza majumbani,

Wengine juu ya vitanda, shisha ipo mdomoni,

Shisha sasa ni mtindo, nchi zote Arabuni.

 

Kuna shisha ya matunda, na tumbaku huchanganywa,

Eti ni yenye faida, ona wanavyodanganywa,

Ni kitu cha kawaida, wajinga wanaambiwa,

Shisha sasa ni mtindo, nchi zote Arabuni.

 

Tena kwa mamilioni, pesa nyingi zinatupwa,

Hatua hatuzioni, hakuna kinachofanywa,

Hata watoto shuleni, huwaoni wakikanywa,

Shisha sasa ni mtindo, nchi zote Arabuni.

 

Faida kwa mabepari, pesa wanazikusanya,

Viwanda vya makafiri, vinashamiri Ulaya,

Mashekhe wanahubiri, hakuna wa kusikiya,

Shisha sasa ni mtindo, nchi zote Arabuni.

 

Na tena wanatangaza, tazama magazetini,

Watu wanawapoteza, matangazo redioni,

Na picha wanasambaza, kila pembe madukani,

Shisha sasa ni mtindo, nchi zote Arabuni.

 

Ulaya wamegutuka, watu wameerevuka,

Wengi wanaiepuka, wavutaji hupunguka,

Huku kwetu wamedaka, idadi huongezeka,

Shisha sasa ni mtindo, nchi zote Arabuni.

 

Hata kule Afrika, tumbaku wanatumia,

Ugoro umesifika, ananusa anabwia,

Mashamba yanalimika, tumbaku kupalilia,(2)

Ugoro(3) umetajika, nchi nyingi Afrika.

 

Kiko(4) pia inavutwa, khasa wale Mabwanyenye,

Hapo ni “Bwana Mkubwa”, anavyoringa mwenyewe,

Ona meno yanabanwa, anapozungumza yeye,

Kiko kimesimuliwa, ni tabia za Wazungu.

 

Karafuu wanaweka, na tumbaku Indonesia,(5)

Harufu utatoroka, anapo kupulizia,

Karafuu hutumika, madhara ya jumuia,

Sigara za karafuu, Asia wanaumia.

 

Cigar(6) kutoka Cuba, zimeingia mjini,
Utaona wamebeba, mapaketi mikononi,
Wakivuta pua ziba, harufu kama chooni,

Cigar ni kubwa sana, na madhara kadhalika.

 

Ni silaha ya adui, nia kutuangamiza,
Makafiri zao rai, dini yetu kupoteza,
Wengi watu hawajui, bado wapo kwenye giza,

Tumbaku ni sumu kali, tazama wanaokufa.

 

Viwanda vya Mayahudi, vinazidi kupanuka,
Njama zao zinazidi, bajeti wameshaweka,
Na sisi tupo baridi, tumezorota hakika,

Tumbaku sababu kubwa, ya vifo ulimwenguni.

 

Na wapige marufuku, kuiingiza nchini,

Pesa hizi za tumbaku, wangepewa masikini,

Mungu Ataturuzuku, nawaaga ikhwani,

Tumbaku hatutashuku, ni mmea wa mashetani.

 

 

                    

            

 

 (1) Shisha                      (2) Shamba la tumbaku

                     

                  

 (3) Ugoro                       (4) Kiko

 

      

        

 

 (5) Gudang Garam   (6) Cigar   

     (KRETEK)   

 

 

Share