Bilaal Bin Rabaah (رضي الله عنه)

Bilaal Bin Rabaah (Radhwiya Allaahu 'Anhu)

 

Muhammad Faraj Salim As-Sa’ay (Rahimahu-Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa kila linapotajwa jina la Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akisema;

 

"Bwana wetu aliyemkomboa Bwana wetu". Akimkusudia Bilaal bin Rabaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Wanasema wanavyuoni kuwa; Unapomsikia ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akimwita mtu 'Bwana wetu', basi tambua ya kuwa huyo ni mtu adhimu.

Imeandikwa katika Siyar al-A’alaam an-Nubalaa kuwa Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye asili yake ni Mhabeshi (mu-Ethiopia), alikuwa mweusi sana, mwembamba, mrefu na mwenye nywele ndefu.

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mtumwa wa kabila la Bani Jumhi, na maisha yake yalikuwa kama mtumwa yeyote wa kawaida pale Makkah, hakuwa na uwezo wala uhuru wowote isipokuwa kuwatumikia mabwana zake watu wa kabila la Al-Jumhi. Baadaye alimilikiwa na Umayyah bin Khalaf peke yake ambaye pia anatokana na kabila hilo la Al-Jumhiy, na mama yake Bilaal na jina lake lilikuwa Hamaamah, naye pia alikuwa mtumwa wa kabila hilo la Al-Jumhi.

 

Mara baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuanza kuwalingania watu katika dini ya Kiislam kwa jahari, Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akawa anasikia habari za dini hii mpya na habari za Rasuli huyu mpya (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na habari hizo zilikuwa zikimfurahisha sana kila anapozisikia hasa kutoka kwa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa kila anapopata fursa akimwendea Bilaal na watu wengine pia na kuwahadithia juu ya dini hii.

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasilimu mikononi mwa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akifanya kazi kubwa sana tokea siku ya mwanzo katika kuwalingania watu katika dini hii tukufu.

 

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiwalingania watu waliokuwa huru na akafanikiwa kuwasilimisha watu watukufu wakiwemo watano katika wale kumi waliobashiriwa Pepo nao ni ‘Uthmaan bin ‘Affaan, Az-Zubayr bin ‘Awaam, ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf, Sa’ad bin Abi Waqaas na Twalhah bin ‘Ubaydullaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na wengi wengineo, na alikuwa pia akiwalingania watu wasiokuwa huru kama vile Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa rafiki yake Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) tokea hata kabla ya Uislam, na wengineo pia.

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alifuatana na Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mpaka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuzitamka shahada mbili mbele yake, na kwa ajili hiyo akawa miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika dini hii tukufu.

 

 

Ahadun Ahadun

 

Uislam ulipoanza kuenea katika mji wa Makkah, na baadhi ya Ma-Quraysh kutambua kuwa watumwa wao walikuwa wakiingia katika dini hii mpya kwa siri tena kwa wingi, wakaanza kuwatesa kwa kuwaonjesha kila aina ya adhabu.

Miongoni mwa Waislam wa mwanzo waliokuwa watumwa na wakapata adhabu kubwa kutoka kwa washirikina wa Makkah, ni Sumayyah, mama yake ‘Ammaar aliyekuwa mke wa Yaasir (Radhwiya Allaahu ‘anhum) waliokuwa na asili ya Ki-Yemen.

Walikuwa wakiadhibishwa sana, na kila Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapopita nje ya nyumba yao alikuwa akiwaambia;

"Kuweni na subira enyi watu wa nyumba ya Yaasir, kwani hakika waadi wenu ni Jannah (Pepo)".

Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alifariki akiwa anateswa na akapata bahati ya kuwa Shahid wa mwanzo katika dini ya Kiislam.

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) naye alipata sehemu kubwa ya adhabu, kwani bwana wake Umayyah bin Khalaf aliyekuwa mtu khabithi sana, alikuwa akimtoa nje wakati wa jua kali linalounguza mwili na kumvua nguo zake kisha anamlaza juu ya mchanga wa jangwani unaounguza na kumwekea jiwe kubwa sana juu ya kifua chake huku akimwambia;

"Utabaki hivyo hivyo mpaka ufe isipokuwa kama utamkanusha Muhammad na kumtukana kisha urudi tena kuiabudu miungu yako Lata na Uzza".

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akimjibu kwa kusema;

"Ahadun Ahadun".(Mmoja tu, mmoja tu)

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliwahi kuulizwa;

"Kwa nini ulikuwa ukiendelea kusema hivyo "Ahadun Ahad".(Mmoja tu, mmoja tu), na hali unajua kuwa maneno hayo yanawaghadhibisha na kwa ajili hiyo wao wataendelea kukuadhibu?"

Akajibu;

"Wa-Allaahi kama ningekuwa nalijuwa neno jingine linaloweza kuwakasirisha zaidi kuliko hilo, basi ningelilitamka".

Hakika neno; "Ahadun ahad", lilikuwa likimkera sana Umayyah na kila anapolisikia alikuwa ghadhabu zinampanda na akawa anampiga Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kama mwendawazimu.

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akawa anaendelea kuadhibishwa na yeye alikuwa akiendelea kustahamili huku akiendelea kulitamka neno lake hilo 'Ahadun ahad', mpaka Umayyah mwenyewe akashindwa, kwani kila siku baada ya kumtesa wakati wa mchana, alikuwa akimfunga kamba shingoni na kuwakabidhi watoto wadogo na wendawazimu waliokuwa wakimburura Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kuzunguka naye mjini Makkah, huku wakimzomea na kumpiga, na yeye alikuwa akiendelea kusema'

"Ahadun ahad" (Mmoja peke yake mmoja peke yake).

 

 

Na Amchae Allaah

 

Siku moja Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa akipita akamuona Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika hali ile, akamwambia Umayyah;

"Humuogopi Allaah wewe, unamtesa namna hii maskini huyu, mpaka lini utaendelea hivi?'

Umayyah akamwambia;

"Wewe ndiye uliyemharibu huyu, kwa hivyo sasa muokoe wewe kama unaweza".

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamnunua kwa wakia tano na akamuacha huru kwa ajili ya kutaka Radhi za Allaah, na kabla ya hapo Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa keshawanunua watumwa sita na kuwaacha huru, na Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa wa saba.

Bilaal akaepukana na adhabu, na Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) bila shaka akapata ujira mkubwa kutoka kwa Mola wake (Subhanahu wa Ta’ala).

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliendelea na kazi hiyo ya kuwanunua watumwa na kuwaacha huru, na ‘Ulamaa wa tafsiri wamekubaliana kuwa Allaah Alimsifia Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika Aya ya 17 katika Suratul Layl pale Aliposema;

 

 وَسَيُجَنَّبُهَا الْأَتْقَى ﴿١٧﴾

Na ataepushwa nao mwenye taqwa kabisa.

 

 

الَّذِي يُؤْتِي مَالَهُ يَتَزَكَّىٰ ﴿١٨﴾

Ambaye anatoa mali yake kujitakasa.

 

 

وَمَا لِأَحَدٍ عِندَهُ مِن نِّعْمَةٍ تُجْزَىٰ ﴿١٩﴾

Na hali hakuna mmoja yeyote aliyemfanyia fadhila yoyote hata amlipe.

 

 

إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٠﴾

Isipokuwa kutaka Wajihi wa Rabb wake Aliyetukuka.

 

 

وَلَسَوْفَ يَرْضَىٰ ﴿٢١﴾

Na bila shaka atakuja kuridhika.  [Al-Layl: 17-21]

 

 

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akaondoka hapo pamoja na Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kwenda mpaka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na alipokuwa akiondoka naye, Umayyah akamwambia;

"Ondoka naye hapa, Naapa kwa Laata na Uzza, kuwa ungekataa kumnunua kwa wakia tano, basi hata kwa wakia moja tu ningekuuzia".

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamjibu;

"Wal-Allaahi lau kama ungetaka nimnunue kwa wakia mia basi ningekupa.”

 

 

Muadhini Wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Wa Mwanzo

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifurahi kupita kiasi alipomuona Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akiwa huru, na akawabashiria Waislam juu yake na akamfanya baadaye kuwa ni Muadhini wake wa mwanzo katika Uislam, kwani Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa na sauti nzuri sana na Allaah Akaijaalia sauti hiyo iwe yenye kuleta taathira ndani ya nyoyo za kila mwenye kuisikia.

 

Mji wa Madiynah ulikuwa ukitulia pale anapoadhini Bilaal, na watu walikuwa wakikimbilia Msikitini mara baada ya kuisikia sauti yake (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia alikuwa akimpenda sana Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na akistarehe sana kila anapoisikia sauti yake, na hasa anapoadhini, na alikuwa akiwatanguliza Bilaal na watu masikini miongoni mwa Waislam kabla ya matajiri na alikuwa akikaa nao muda mrefu zaidi na alikuwa akiwakirimu.

 

Siku ile Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoingia na majeshi yake kuuteka mji wa Makkah, na baada ya kusafishwa Msikiti wa Makkah kutokana na masanamu yaliyokuwa yamejaa humo, aliingia Msikitini na kuufunga mlango nyuma yake akiwa yeye na Bilaal na ‘Usaamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) peke yao ndani ya Msikiti na katika riwaya nyingine aliingia pia na ‘Uthmaan bin Twalha (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na kuwaacha watu wa kabila lake na watu wa nyumba yake pamoja na Maswahaba wakubwa wakubwa kama vile Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhum) nje ya Msikiti.

 

 

Nabiy  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamtaka Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) apande juu ya Al-Ka’abah na kuadhini, na Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akafanya kama alivyoamrishwa, na jambo hili liliwakasirisha sana baadhi ya Ma-Quraysh, akasema Itab bin Usayd;

"Nashukukru baba yangu hajaishi mpaka akaweza kuyaona haya! Hivyo Muhammad hajapata mwengine wa kutuadhinia isipokuwa kunguru huyu mweusi?"

 

Bilaal na ‘Usaamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wote walikuwa watumwa kabla ya Uislam.

 

Na katika Hadiyth, siku moja Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu);

"Nielezee juu ya ‘amali njema kabisa unayoitenda, kwani nimesikia sauti ya viatu vyako vikiwa mbele yangu Peponi?"

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akajibu;

"Ee Rasuli wa Allaah sijafanya ‘amali yoyote niliyoiona kuwa ni bora kwangu isipokuwa kawaida yangu mimi kila nikitawadha huswali kadiri ninavyojaaliwa kuswali”.

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;

“Hilo ndilo lililokufikisha”.

[Al-Bukhaariy]

 

 

 

Baadhi Ya Sifa Zake

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakuwa akimiliki sauti nzuri tu, bali alikuwa pia shujaa na alishiriki katika vita vyote walivyopigana Waislam, vile alivyoshiriki Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndani yake na pia vile asivyoshiriki, na alikuwa mpiganaji mzuri sana. Alishiriki katika vita vya Badr na kupigana kwa ushujaa mkubwa, na yeye ndiye aliyemuua Umayyah bin Khalaf baada ya kutekwa na Waislam katika vita hivyo.

Ingawaje daraja yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mbele ya Maswahaba wake (Radhwiya Allaahu ‘anhu), lakini Bilaal hakuwa mtu mwenye kujiona wala kujivuna wala mwenye kutakabari, bali alikuwa mnyenyekevu kwa Waislam wenzake, huku akiichunga nafsi yake, jambo lililomfanya aheshimiwe zaidi na Maswahaba wenzake (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

 

Kuposa Kwake

 

Katika kitabu cha Siyar Al-A’alaam An-Nubalaa cha Imaam Adh-Dhahabiy na katika Al-Bidaayah wan-Nihaayah cha Ibn Kathiyr imeandikwa kuwa; Siku ile alipokwenda yeye na ndugu yake kuposa katika nyumba moja ya watu wa kabila la Ki-Yemen, aliwaambia;

"Mimi ni Bilaal na huyu ni ndugu yangu Abshan, sisi ni watu wa Uhabeshi, tulikuwa tumepotoka na Allaah Akatuongoza, na tulikuwa watumwa na Allaah Akatukomboa. Kama mtakubali kutuozesha watoto wenu, 'AlhamduliLlaah' tunamshukuru Allaah, na kama mtatukatalia basi 'Allaahu Akbar' Allaah ni Mkubwa".

Bilaal na ndugu yake waliowa katika nyumba hiyo.

 

 

Siku Aliyofariki Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

Maisha yake yote Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tena karibu naye. Kila siku akimuadhinia huku Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akifurahishwa na sauti yake na yeye kwa upande wake alibahatika kuweza kuyatia nuru macho yake kila siku kwa kumuona kipenzi cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) asubuhi na jioni, mchana na usiku, mpaka siku ile Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoisalimisha roho yake kwa Mola wake.

 

Siku ile, Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliingia chumbani kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya kumtizama kipenzi chake kwa mara ya mwisho, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amefunikwa na kulazwa juu ya tandiko lake, na Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akawa anamtizama huku machozi yakimlenga. Aliposhindwa kuimiliki nafsi yake akaanza kulia kwa kwikwi.na baada ya muda akatulia, kisha akasogea mbele yake na kumswalia. Baada ya kumswalia akatoka chumbani huku machozi yakiwa yanaendela kumiminika.

 

Usiku uliofuata Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakuweza kupata usingizi hata kidogo kutokana na huzuni iliyomjaa moyoni mwake, na hasa kila anapokumbuka kuwa hatoweza kumuona tena Swahibu yake kama alivyokuwa akimuona kila siku mbele ya macho yake. Akawa katika hali hiyo usiku kucha mpaka ulipokaribia wakati wa Swalah ya Alfajiri alipotoka na kuelekea Msikitini kama kawaida yake kwa ajili ya kuadhini, na ulipoingia wakati wa adhana akaanza kuadhini;

"Allaahu Akbar, Allaahu Akbar, Allaahu Akbar Allaahu Akbar. Ash-hadu an laa ilaaha illa-Allaah, Ash-hadu an laa ilaaha illa-Allaah…" Alipotaka kutamka;

"Ash-hadu anna Muhammadan Rasuulu-LLaah", Akashindwa, - pumzi zilimkaba, sauti ikashindwa kutoka, na aliposhindwa kuimiliki nafsi yake, machozi yakaanza kummiminika, na watu waliposikia kukatika kwa adhana na kilio cha Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wote waliokuwepo Msikitini nao pia wakaanza kulia. Na baada ya kuweza kuimiliki nafsi yake, Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akaikamilisha adhana kwa sauti ndogo na hakuweza kuinyanyua sauti yake.

 

Baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuzikwa, Bilaal akaondoka na kujitenga mbali kidogo na watu huku akilia kwa huzuni. Ulipoingia wakati wa Swalaah, watu wakawa wanamsubiri Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) awastareheshe kwa kuwaadhinia kwa sauti yake nzuri. Lakini Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakuadhini. Watu wakamkumbusha kwa kumwambia;

"Wakati wa adhana ushaingia ee Bilaal".

Akasema huku machozi yakimlenga;

"Sitoadhini tena baada ya leo, bora aadhini mwengine badala yangu."

 

 

Sitoadhini Tena Baada Ya Kufa Kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Wakati wa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa Khalifa wa Waislam, alimtaka Bilaal aadhini akamwambia;

"Adhini".

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikataa, akamwambia;

"Ikiwa ulinikomboa kwa ajili ya nafsi yako basi nikamate, ama ikiwa kwa ajili ya kutaka radhi za Allaah, basi niache na Allaah wangu."

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamwambia;

"Nilikukomboa kwa ajili ya kutaka radhi za Allaah Peke Yake".

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamjibu kwa huzuni;

"Basi mimi sitoadhini tena baada ya kufa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)".

Baada ya kufariki Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akataka kwenda kupigana Jihaad, lakini Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimkatalia, akamwambia;

"Nakuomba kwa ajili ya Allaah ee Bilaal, kwa hisani yako, umri wangu ushakuwa mkubwa na siha yangu ishadhoofika na ajali yangu ishakaribia, tafadhali baki hapa pamoja na mimi".

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akakubali kuwa pamoja naye mpaka Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipofariki dunia.

 

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) Anakwenda Kupigana Jihaad

 

Alipotawala ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu), naye pia alimtaka Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aadhini, naye akamkatalia pia ombi lake hilo, kisha ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamuuliza;

"Yupi unaona nimpe kazi ya kuadhini?"

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Sa’ad, kwani yeye aliwahi kuadhini wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)".

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamwendea ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kumuomba amruhusu kwenda kupigana Jihaad.

‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamwambia;

"Ee Bilaal, hutaki kubaki pamoja nami kama ulivyokuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha pamoja na Abu Bakr?"

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Natamani kwenda kupigana Jihaad ewe Amiri wa Waislam, na naona kuwa Jihaad ni miongoni mwa ‘amali bora kupita zote".

‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamwambia;

"Fanya kama unavyotaka ewe Bilaal."

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasafiri kuelekea nchi ya Shaam na kujiunga na jeshi lililokuwa likiongozwa na Abu ‘Ubaydah ‘Aamir bin Jarraah (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) Anaadhini Tena

 

Alipoitembelea nchi ya Shaam wakati wa Ukhalifa wake, ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alionana tena na Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na Waislam wakamuomba ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) awaombee kwa Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ili awaadhinie angalau mara moja tu ili wapate kuisikia sauti yake ‘adhimu aliyokuwa akiinyanyua kila siku mara tano wakati wa uhai wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Ulipoingia wakati wa Swalah, ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamuomba Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aadhini na Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akalikubali ombi lake, akapanda juu ya mlmbari na kuanza kuadhini. Nyoyo za watu zilikuwa zikipiga kwa nguvu huku wakiisikiliza sauti ya Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akiadhini kwa mara ya mwanzo tokea alipofariki Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Imeandikwa katika kitabu cha Siyar A’alaam An-Nubalaa kuwa;

"Watu hawakupata kulia kama siku hiyo kwa ajili ya kukumbuka uhai wa Nabiy wao (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)".

 

 

Kifo Chake (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)

 

Haya kwa ufupi ni maisha ya Swahaba huyu mtukufu (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyejitolea nafsi yake kwa ajili ya kuipigania dini ya Allaah.

Alifariki katika mji wa Damascus mwaka wa ishirini baada ya Hijrah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa ana umri uliopindukia miaka sitini kwa maradhi ya tauni yaliyowaua watu wengi sana katika nchi ya Shaam.

Inasemekana kuwa roho yake ilipokuwa ikimtoka, mkewe alikuwa akimwambia;

"Huzuni iliyoje, huzuni iliyoje."

Lakini Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiyafumbua macho yake akasema;

"Bali furaha iliyoje, kesho nitaonana na wapenzi, Muhammad na Maswahaba."

 

Share