Historia Ya Salaf Wa Ummah Kwa Kifupi - Karne Ya Kwanza

 

Historia Ya Salaf Wa Ummah Kwa Kifupi

Karne Ya Kwanza (1H - 99H)

Imefasiriwa Na: Abu Sumayyah

Alhidaaya.com

 

 

‘Abdullaah Abu Jaabir (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

‘Abdullaah Abu Jaabir bin ‘Amr bin Hazzam bin Tha’labah al-Answaariy al-Khazrajiy as-Sulamiy, ni miongoni mwa waliotoa ahadi ya ‘Uqbah. Alihudhuria vita vya Badr na alikufa shahidi katika vita vya Uhud.

 

 

 

‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

‘Abdullaah bin ‘Abbaas bin ‘Abdul-Muttwalib bin Haashim bin ‘Abd Manaaf al-Qurashiy al-Haashimiy, alikuwa ni binamu yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na alikuwa mfasiri wa Qur-aan. Alizaliwa miaka mitatu baada ya Hijrah na alikuwa anaitwa ‘Bahari ya Elimu.’ Alishiriki katika Jihaad kule Kaskazini mwa Afrika kwenye mwaka 27H na alikufa mwaka 68H.

 

 

 

‘Abdullaah bin ‘Amr (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

‘Abdullaah bin ‘Amr bin al-’Aasw bin Waail bin Haashim bin Su’ayd bin Sa’d bin Sahm as-Sahmi. Yeye na baba yake walikuwa ni Maswahaba. Alikuwa anajua kusoma na kuandika na alipata ruhusa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuandika yote yale aliyokuwa akiyazungumza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikufa katika mwaka 65H.

 

 

 

‘Abdullaah bin Mas’uwd (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Alikuwa Swahaba mkubwa wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ‘Abdullaah bin Mas’uwd bin Ghaafil bin Habiyb (Radhiya Allaahu ‘Anhu), alikufa katika mwaka 32H huko Madiynah. Az-Zubayr aliongoza Swalah ya Janaazah lake na kuzikwa Baqiy’.

Alikuwa ni mtu wa sita kusilimu hata kabla ya ‘Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimbashiria makazi yake Peponi. ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alitaja jambo hii kusema ya kwamba Mtume alimuamuru Ibn Mas’uwd kupanda mti kuchuma kitu fulani na kuleta chini. Maswahaba walikuwa wakiangalia miundi ya Ibn Mas’uwd wakati akipanda mti na waliaanza kumcheka kutokana na uwembamba wa miundi yake. Mjumbe wa Allaah alisema: “Ni kitu gani kinachowachekesha? Miguu ya Ibn Mas’uwd ni mizito kwenye mizani siku ya Qiyaamah kuliko Mlima Uhud.”

[Imesimuliwa na Imaam Ahmad katika Musnad yake na kuthibitishwa na Shaykh Ahmad Shaakir (920)].

‘Abdullaah bin Mas’uwd alikuwa msomaji mkubwa wa Qur-aan. Inasemekana alikuwa ni mmoja wa watu wenye kufuata kwa karibu sana muongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Imekusanywa kutoka kwenye kitabu cha Siyaar A‘laam an-Nubalaa - cha Adh-Dhahabiy na Tahdhiyb At-Tahdhiyb cha Ibn Hajr.

 

 

 

Abu ad-Dardaa (Radhiya Allaahu ‘Ahnu)

Abu ad-Dardaa Uwaymir bin Maalik bin Zayd bin Qays al-Khazrajiy al-Answaariy. Kuna maoni tofauti kuhusu jina lake. Alisilimu wakati wa vita vya Badr na alishuhudia vita vya Uhud. Alikuwa ni Mwanachuoni wa Shari’ah. Mchaji Allaah miongoni mwa Swahaba. Alikufa katika mwaka 32H.

 

 

 

Abu Dharr al-Ghifaariy (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Abu Dharr al-Ghifaariy Jundub bin Junaadah bin Sakn alikuwa ni miongoni waliosimu mwanzoni lakini alichelewa kufanya Hijrah hivyo hakushiriki vita vya Badr. Fadhila zake ni nyingi na alikufa mwaka 32H.

 

 

 

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Abu Hurayrah, ‘Abdur-Rahmaan bin Swakhr ad-Dawsiy alikwenda kwa  Mtume kama Muhaajir wakati wa vita vya Khaybar. Alihifadhi idadi kubwa ya Hadiyth. Zaidi ya Hadiyth elfu nane zilisimuliwa kutoka kwake. Alikufa katika mwaka 58H.

Mtume Alimuombea du’aa yeye na mama yake kwa kusema: “Ee Allaah! Wajaalie hawa waja wako (wawili) ni wenye kupendwa na Waumini na wafanye Waumini ni wenye kuwapenda.” [Imesimuliwa na Muslim].

 

 

 

Abu Muwsaa al-Asha’riy (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Abu Muwsaa al-Ash’ariy ‘Abdullah bin Qays bin Saalim alikuwa ni mwenye sauti nzuri wakati wa kusoma Qur-aan na ni mmoja wa Wanachuoni  miongoni mwa Maswahaba. Inasemekana alikufa mwaka wa 42H au 44H.

 

 

 

Abu Sa’iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Abu Sa’iyd al-Khudriy Sa’ad bin Maalik bin Sinaan bin ‘Ubayd al-Answaariy al-Khazrajiy. Yeye na baba yake wote walikuwa ni Maswahaba na alishuhudia vita vyote vilivyofuata baada ya vita vya Uhud. Alikuwa ni mmojawapo wa Wanachuoni miongoni mwa Maswahaba na alisimulia Hadiyth nyingi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikufa katika mwaka 74H.

 

 

 

‘Adiy Bin Haatim (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

‘Adiy bin Haatim bin ‘Abdillaah bin Saa’d bin al-Hashraj bin ‘Aamr al-Qays at-Twaaiy, Abu Tarif. Alikuwa Mkristo aliyesilimu na kuhudhuria vita vya Jamal, Swiffiyn na an-Nahrawaan pamoja na ‘Aliy. Alikufa katika mwaka 68H.

 

 

 

Al-Bara’a bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Al-Bara’a bin Maalik bin an-Nadr al-Answaariy.Alihudhuria vita vya Uhud na alitoa ahadi ya utii chini ya mti. Alikufa shahidi katika mwaka wa 20H kwenye siku Tustar.

 

 

 

Al-Mughiyrah Bin Shu’bah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Al-Mughiyrah bin Shu’bah bin Abi ‘Aamir bin Mas’uwd ath-Thaqafiy, Abu ‘Abdillaah. Alihudhuria vita vya Hudaybiyah, Al-Yamaamah na alipata ushindi kule Syria na Iraq. Alikufa katika mwaka 50H.

 

 

 

‘Amr Bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

‘Amr bin al-’Aasw bin Wa’il al-Qurashiy as-Sahmiy Alisilimu katika mwaka wa Sulhu Hudaybiyah na alikuwa ni mmoja wapo kati ya wale walioshinda  kule Misr. Alifariki katika mwaka 43H.

 

 

 

Anas Bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Anas bin Maalik bin an-Nadr, Abu Hamzah, al-Answaariy, an-Najjaariy. Alikuwa mfanyakazi wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). ambaye alikaa nae karibu kwa takriban miaka kumi tangu alipohama mpaka kifo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa ni miongoni mwa Maswahaba wa mwisho kufariki. Alifariki akiwa na miaka 93H kule Baswrah akiwa na miaka 103.

 

 

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alimuombea du’aa kwa kusema: “Ee Allaah Mjalie utajiri na watoto na Vibariki vile ulivyomruzuku.” [Muslim].

Na katika mapokezi mengine Anas Aliongezea kwa kusema: “Na (kutoka kwa) Allaah fungu langu imekuwa kubwa watoto wangu na wajukuu wameongezeka kiasi cha kufikia mia moja kwa kuwahesabu.” [Muslim].

 

 

 

‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘Anha)

‘Aaishah bint Abi Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhuma). Mke wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Baada ya Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘Anha) kufariki, Malaika Jibriyl alimuonyesha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye ndoto kabla ya kumuoa na alikuwa na miaka kumi na nane wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipofariki.

Alifariki katika mwaka 59H kwenye tarehe kumi na saba ya mwezi wa Ramadhwaan. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alimzika.

Alikuwa Mama wa Waumini Asw-Swiddiyqah (Radhiya Allaahu ‘Anha). ‘Umar alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Ni nani unayempenda zaidi miongoni mwa watu? Akajibu: ‘Aaishah’. Kisha, akamuuliza miongoni mwa wanaume (ni nani unayempenda zaidi)? Akajibu: Baba yake.”

 

Ash-Sha’abiy alisema: Wakati Masruwuq anatusimulia kuhusu ‘Aaishah, alisema: ‘Niliambiwa na mkweli, bint wa mkweli, mpendwa miongoni mwa vipenzi vya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Asiye na hatia ambaye ndoa yake ilianzishwa kutoka mbingu ya saba.

Az-Zuhriy alisema: “Iwapo elimu ya Mama ‘Aaishah itakusanywa na kulinganishwa na elimu ya wakeze wengine Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wanawake wengine wote basi elimu ya Mama ‘Aaishah ingelibakia kuwa isiyo na kifani.”

 

 

 

‘Imran Bin Huswayn (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Imran bin Huswayn al-Khuza’iy al-Ka’biy, Abu Nujayd. Alisilimu mwaka wa vita vya Khaybar na aliripoti baadhi ya Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikufa katika mwaka 52H.

 

 

 

Jaabir Bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Jaabir bin ‘Abdillaah bin ‘Amr bin Harram al-Answaariy as-Sulamiy. Alishuhudia ‘Uqbah wakati wa pili huku akiwa mtoto. Inasemekana alihudhuria vita vya Badr na Uhud na kuripoti Hadiyth nyingi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alifariki katika Mwaka wa 74H.

 

Share