Zingatio: Shindaneni Katika Kheri

 

Zingatio: Shindaneni Katika Kheri

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Ndani ya darasa lenye wanafunzi mchanganyiko, wenye ufahamu wa hali ya juu na wale wasiofahamu mara moja, matokeo ya darasa kama hili ni kundi moja kuliathiri jengine, na mara nyingi hao wenye ufahamu wa chini watawaathiri hao waliojaliwa kuwa na vipaji vya akili.

 

Ili kupata ufundishaji utakaowasaidia wanafunzi na walimu wao, madarasa mawili yanagaiwa baina ya wenye vipaji na wale wenye ufahamu wa kawaida. Miongoni mwa madhumuni ya kuwatenganisha ni kuwafanya wanafunzi wawe ni wenye kushindana kimasomo.

 

Halikadhalika kwa Uislamu, ili Muislamu awe ni mtenda mema na mwenye kuachana na maovu, yatakikana kuwa karibu na watenda mema. Kundi hili ni lile la Waumini wanaoshikamana katika subira, wakausiana haki na wakakatazana batili.

 

Kwa Waumini hawa ndio kunapatikana ladha ya ibada kwani kila mmoja hujifunza kwa mwengine na kujitahidi kumpita mwenziwe. Kama mmoja ataamka usiku kuswali rakaa tano, mwengine ataswali rakaa saba, na mwengine kumi na moja. Kama mmoja wao atafunga siku tatu kwa mwezi, mwengine atafunga kila wiki mara mbili na mwengine atafunga siku moja na kuacha siku moja. Hiyo ndio hali ya wenye kushindana katika kheri.

 

Hao ndio ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amewasifu ndani ya Qur-aan kwa kuwa wapo mbele katika kheri: 

 

ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ وَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ ﴿٣٢﴾

Kisha Tukawarithisha Kitabu wale Tuliowakhitari miongoni mwa waja Wetu. Basi miongoni mwao ni mwenye kudhulumu nafsi yake na miongoni mwao aliyekuwa wastani na miongoni mwao aliyesabiki kwa mambo mengi ya kheri kwa idhini ya Allaah. Hiyo ndio fadhila kubwa. [Al-Faatwir: 32]

 

Kwa masikitiko makubwa, Waislamu walio wengi wanashindana kuangalia DVD zenye kupotosha dira nzima ya Uislamu. Wapo wasichana wanaoshindana kutembea utupu hadi kuzawadiwa mamilioni ya fedha. Wengine wanaoneshana orodha ya wazinifu, unywaji wa pombe na mengi mengineo yasiyofaa kabisa. Hili ndio kundi lililoshindwa kuelewa lengo la kuumbwa kwao hapa duniani.

 

Tujifunze kutokana na Siyrah za Swahaba waongofu. Swahaba ambao walikuwa wakitoka usiku wa manane kutafuta ‘amali njema za kufanya bila ya kuonekana. Sayyidna Abu Bakr na Sayyidna 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhuma) walikuwa ni wenye kushindana mno katika matendo mema. Hadi ilifikia kwamba Sayyidna 'Umar alipotoka kumsaidia kazi za ndani mama mtu mzima, alielezwa ya kwamba kishakutangulia kabla yako ambaye ameshayafanya yote. Sayyidna 'Umar hakukubaliana tu na hilo kwani alifanya juu chini hadi kutambua kwamba ni Sayyidna Abu Bakr anayemtangulia kabla ya kufika kwake.

 

Hiyo ndio hali waliyokuwa nayo Swahaba na wema waliotutangulia. Tujichungue na tujiangalie sisi tupo wapi na wapi tunaelekea?!

 

Share