Alinitaka Kunioa Kisha Kabadlisha Rai Yake, Nimeambiwa Na Shaykh Kuwa Mkewe Kaniroga Nami Bado Nampenda

 

Alinitaka Kunioa Kisha Kabadlisha Rai Yake,

Nimeambiwa Na Shaykh Kuwa Mkewe

Kaniroga Nami Bado Nampenda

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Asalaam Alaykum,

 

Allaah awajilie kila la kheri kwa kazi ngum mnayoifanya.

mimi ni msichana nilikuwa na mchumba ambae alikuja nyumbani na kutoa maneno ya kunioa miaka 3 sasa, lakini ni mtu ambae ana mke na watoto wawili, alimweleza na mkewe na mara nyingine mkewe alikuwa hata anapiga simu na kutoa maneno machafu, Alhamdulilah namshukuru mola kwa ujasiri na rehma ya kuyaona yale ni yakupita. Sasa mwanaume amekuja kwetu anasema hataki tena ndoa kwani mke na mama yake wamekataa. Roho inaniuma sana mwisho wa mwezi jana niliumwa sana kwenda kwa shekh akaniambia huyu mwanamke amekutupia mambo uwe mwehu lakini sala zako ndo zinakulinda. Nampenda mchumba wangu na sijui la kufanya.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Dada yetu inataka uwe na Imani thabiti ya kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) yupo na mambo yote yanayotokea ni kwa ujuzi na elimu Yake, Naye Ana habari ya yote yanayotokea. Usiwe ni mwenye kulaumu kwani hujui kheri yako iko wapi.

 

Jua kuwa Muislamu hupatiwa mitihani tofauti na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kutegemea Imani yake. Kila Imani inavyokuwa kubwa basi mitihani inakuwa mingi. Na fahamu kuwa kila mmoja anapata mtihani wake wa aina yake ambao haufanani na wa mwingine. Naomba usome Suwrah Al-Baqarah (2), Aayah ya 155-156 kuhusu suala hilo la mitihani. Ukizifahamu Aayah hizo utakuta kuwa mtihani wako ni mdogo sana kulingana na wengine waliopata mitihani mikubwa zaidi.

 

Kulingana na swali lako umetueleza kuwa wewe ni binti wa Ibadah, hasa Swalah lakini inaonyesha unazivunja Ibadah zako kwa kwenda kwa mtazamiaji. Tunasema hivyo kwa kuwa umesema umekwenda kwa sheikh, naye akakwambia kuwa huyu mwanamke amekurushia mambo. Kawaida Shaykh wa kisawa sawa aliyesoma Dini ya Kiislamu hawezi kukwambia kuwa umefanyiwa mambo na mtu fulani. Jambo ambalo anaweza kukamwambia ni baada ya kukusomea kisomo cha sheria sio kupitia ushirikina kuwa umefanyiwa kadhaa baada ya Shaykh kuzungumza na yule jini uliorushiwa. Ikiwa ni uchawi basi lile ambalo litajulikana ni aliyefanya na kitu kilichofanyiwa. Ikiwa huyo Shaykh anafanya kulingana na Sunnah itakuwa ni kheri na lau ni kinyume cha hivyo itakuwa umeingia katika ushirikina. Kuwa na tahadhari.

 

Ama kuhusu kujibu kwa unayempenda hiyo ni kheri kubwa uliyoipata kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Mara nyingi sisi tunapopenda huona maisha yetu kuwa mazuri ni lazima tupate tunachotaka, ilhali kheri yetu anaijua Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Twaomba usome na ufahamu sana Aayah ifuatayo:

 كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ 

Mmeandikiwa shariy’ah kupigana vita nako kunachukiza mno kwenu. Na asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni khayr kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. [Al-Baqarah: 216].

 

Nasaha zetu kwako ni wewe kumsahau huyo mume kwani huenda Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amekuepusa na shari na mabaya mengi. Kitu cha wewe kufanya ni kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akusahaulishe huyo mwanamme na Akuletee mwengine aliye mzuri na bora kuliko huyo wa awali.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akuletee kheri nyingine na Akuepushie na shari yoyote ile.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share