Mwanamme Kumfundisha Qur-aan Mwanamke

SWALI:

 

Assalam alaykum, mimi ni mvulana ninapenda kuuliza kwamba, kuna msichana ameniomba nimfundishe Qur-an katika mwezi huu wa ramadhani, Je inaruhusiwa?  Maana nyumbani kwao yupo yeye na wasichana wenzake.


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu mwanamme kumfundisha mwanamke Qur-aan.

 

Ni bora kwa msichana kusomeshwa Qur-aan au masomo mengine yoyote na msichana mwenziwe kwani hiyo itaondosha tashwishi na matatizo yanayotarajiwa. Kumetokea matatizo mengi kwa sababu ya wanaume kufundisha wanawake hata watu kutumbukia katika maasi. Hivyo, hili ni jambo lenye kuhitajika kuwa makini sana na waalimu wanaume wajitahidi sana kujiepusha nalo ila kwa dharura tu.

Ikiwa hapana budi kwako kumfundisha itaruhusiwa lakini kwa masharti. Masharti yenyewe ni kuwa:

 

1.     Kusiwe na faragha baina yako na yeye. Kwa hiyo, ima umsomeshe yeye pamoja na wengine au kuwepo na Mahram yake kama mama, kaka au baba au mwengine yeyote ili kusiwe na hiyo faragha.

2.     Ajisitiri inavyotakiwa kishariy'ah hususan avae Niqaab na kuwepo na pazia.

3.     Kusiwe na mzaha baina yenu wala mazungumzo yasiyohusu somo.

4.     Uchukue muda unaohitajika tu si zaidi ya hapo.

 

Hayo ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza:

 عن عمر رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم : ((ما خلا رجل بامرأة إلا كان الشيطان ثالثهما)) الترمذي

Kutoka kwa 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hachanganyiki mwanamume na mwanamke ila shaytwaan huwa ni watatu wao)) [At-Tirmidhiy]

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Awawezeshe kumpata mwanamke wa kuweza kumsomesha mwanamke mwenziwe.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share