Mashairi 7: Kufunga Sita Ni bora, Kutimiza Msafara

  

Mashairi 7: Kufunga Sita Ni Bora, Kutimiza Msafara 

   

 

      ‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

 

 Alhidaaya.com

 

 

 

Allaahu Akbar Kabira, Walhamdulaahi Kathira,

Tunaomba maghfira, na maisha yalobora,

Na dini ipo imara, inapepea bendera,

Kufunga Sita  ni bora, kutimiza msafara.

 

 

 

Kutimiza msafara, kufunga sita ni bora,

Itupandishe mnara, juu tuzidi kung’ara,

Itufundishe subira, na kupunguza hasira,

Kufunga Sita  ni bora, kutimiza msafara.

 

 

 

Wavaao matambara, Allaah Awape sitara,

Awaepushe izara, Allaah Anajua bora,

Dunia ipo duwara, faida au hasara,

Kufunga Sita  ni bora, kutimiza msafara.

 

 

 

Tuacheni kuzurura, watu kwenda kuwapora,

Ni tabia ya Wakora, wenye mengi ya madhara,

Kheri twende mihadhara, Allaah Atupe ujira,

Kufunga Sita  ni bora, kutimiza msafara.

 

 

 

Wafanyao biashara, toa zaka ni tohara,

Ugawe kwa mafukara, Ibarikiwe tijara,

Hio iwe ndio dira, dira ya yako idara,

Kufunga Sita  ni bora, kutimiza msafara.

 

 

 

Tukumbuke kila mara, mauti kwenye fikira,

Tukumbukeni harara, ya moto kule akhera,

Tuacheni maskhara, dunia tutaigura,

Kufunga Sita  ni bora, kutimiza msafara.

 

 

 

Hapa mwisho wa kuchora, pengine ninawakera,

Beti saba ni ishara, kuwa nimetia fora,  

Nipeni yangu bakora, niivuke barabara,

Kufunga Sita  ni bora, kutimiza msafara.

 

 

 

 

 

Share