Ameolewa Na Mume Mwengine Bila Kupewa Talaka Na Mumewe – Talaka Imetolewa Na Viongozi Wa Taasisi – Nini Hukmu Yake?

SWALI:

 

Mke wa mtu kaolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe hajamwacha kwa talaka ya njia yoyote (ya kumtamkia kwa mdomo wala kumwandikia maandishi).  Talaka alipewa na moja ya taasisi za Kiislamu bila mumewe kushirikishwa. Mume alishiriki kikao kimoja tu cha usuluhishi kwenye taasisi hiyo, suluhu haikupatikana baada ya mke kung'ang'ania kudai apewe talaka. 

 

Hata hivyo, katika kikao hicho mume hakutoa talaka, bali wasuluhishi wakaahirisha kikao hadi siku nyingine. Hata hivyo, siku ilifika na kikao hakikufanyika, lakini mke na viongozi wa taasisi wakakutana na kuamua kumwandikia mke talaka ya kuvunja ndoa wakampa huyo mke.

 

Mosi, nini hukumu ya ndoa hiyo? Pili, je, bado anahesabika kuwa ni mke wa mume wa kwanza?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu Mwanamke kuolewa na mwanamme baada kikao cha upatanishi kufeli mara ya kwanza.

 

Hakika mara nyingi hutokea matatizo baina ya wanandoa lakini upatanishi ukawa mgumu kwa kuwa mahakimu au taasisi za kuleta suluhu hazina uwezo huo kabisa au hazifanyi uadilifu.

 

Ikiwa mke amekwenda kushitaki na vikao vya upatanishi vimeanza inabidi vikao hivyo viendelee kwa umoja wao mpaka wafikie hitimisho kuhusu suala hilo. Haifai kabisa katika vikao hivyo kufanywe kando ilhali mmoja wao hajashirikishwa. Ilikuwa ni makosa kwa taasisi hiyo kutoa talaka kabla ya kufika hitimisho kabisa. Ikiwa kikao hakikufanyika siku hiyo basi kingeakhirishwa hadi siku nyingine ili waendelee. Lengo kuu la vikao hivyo ni kuweza kupata suluhu muafaka ambayo itawafanya wanandoa warudiane ili waweze kuishi tena pamoja kama mume na mke. Kwa hiyo, ni makosa makubwa kwa taasisi au hakimu kumuachisha mke kabla njia zote kutumika katika kuwarudisha wanandoa katika hali yao ya awali.

 

Ilitakiwa taasisi hiyo iwe ni yenye kutoa fursa hadi wakati watakapoona kuwa pengine mume ni mkosa hivyo aachishwe na mkewe. Na ikiwa makosa ni ya mke basi ifanywe khul‘u kwa kuwa makosa ni yake hivyo arudishe mahari aliyopewa na mume wakati wa ndoa. Wakati huo baada ya kutoa mahari hayo ndoa itakuwa imevunjika. Kwa hiyo atakuwa na nafasi ya kuolewa na mwengine. Au mume atake kuondoka na shida hizo hivyo atoe talaka kwa khiyari yake.

 

Kwa kuwa hayo yote hayajafanika kisheria mwanamke huyo bado ni mke wa mume wa kwanza na hivyo hakuna ndoa na mume huyu wa sasa. Ikiwa mume wa pili alijua kuwa mke hajaachwa naye akaenda akamuoa atakua na makosa. Na lau kama hakujua hilo atakuwa hana makosa yoyote, lakini ili kujiondoa katika madhambi, itabidi aachane na mke huyo haraka.

 

Baada ya yote hayo tunataka kusema kuwa hii ni kesi ya upande mmoja ambayo tumeisikiliza na tunajibu kama swali lilivyoulizwa tu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

 

Share