Mume Aliyetoa Talaka kwa Simu, Je, Talaka Inakuwa Imesihi?

SWALI:

 

Asalaam alaikuma warhamtullaah wabarakatuh, ama baada ya salaam napenda kutoa shukrani zangu kwa kunijibu swali langu la awali mungu awape kheri duniani na akhera akufanyie wepesi katika kazi yenu hii. katika swali langu la mwanzo nililouliza kuhusu tatizo la ndoa yangu nimefuata ushauri mlonipa nizungumze na mume wangu nimuulize huko kuhama kakusudia nini ameniacha au mie bado mkwewe? nilifanya hivyo japo ilikuwa vigumu kuwasiliana naye na jibu alonipa ni mie sina mke na siwezi kushi na wewe. lakini alovyotamka hakukuwa na shahidi mwanamme alikuwepo mwanamke mgeni ambae ni rafiki, na mie ninavyoelewa talaka inakuwa sahihi mbele ya mashihidi wawili wanaume. Kisha baada ya hapo mie sikuridhika kama hiyo ndio talaka nikaamua kuzungumza na sheikh ambae alietufingisha ndoa akazungumza naye, akamjibu kuwa ameniacha sheikh akaamuuliza kama kulikuwa na shahidi akasema yeye anavyoelewa ameniacha iwapo kulikuwa na shahidi ama la. lakini sheikh akajaribu kumshauri tukutane yeye, mie na sheikh itamkwe talaka tukapanga siku ya kukutana bahati mbaya hiyo siku mwili wangu haukuwa tohara kutonana na hedhi tukaahirisha siku basi ikapangwa siku nyingine siku ilopangwa hakuja hakupokea simu na baade akasema anasafiri kwenda Africa. hapa tuliko ni uingereza.


Basi ndio kweli akasafiri na aliondoka mwezi may hadi sasa hivi na hana mawasiliano yeyote na mimi nina mtoto mdogo ana miaka minne.
Sasa swali langu ndugu zangu je hiyo talaka aloitamka kwa mdomo bila shahidi nichukulie ndio talaka? Na kama si talaka nifanyaje manake kama dini yetu ilivyo yeye ni mwanamme huko alipo ataweza kuoa akaendelea na maisha, mimi sitaweza kuolewa kwa sababu sijaachika kwa hivyo mie ndio nitakuwa nadhulumiwa, nasikitika na nina majonzi sana manake nalilia haki yangu ambayo sijui kwanini inakuwa vigumu kuipata, nawaomba ushauri ndungu zangu manake huyu bwana bado yuko Afrika nitaipataje talaka yangu? mimi siwezi kusafiri kwa sasa kwenda Afrika

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume kutoa talaka kwa simu bila ya shahidi. Hakika ni kuwa mwanzo talaka haina mzaha, ikitolewa kwa matamshi huwa imepita na hahitajii mashahidi wawili. Mashahidi wakiwepo itakuwa ni vyema kwa kuwa hawezi kukanusha kwa kuwepo wao.

 

Kwa jinsi ulivyosema kuwa ulikwenda mpaka kwa shaykh aliyewaozesha naye akatamka tena ni kuwa tayari wewe umeachwa kuanzia wakati huo ulikuwa uhesabu eda yako. Na kulingana na mwezi ambao umesema umeachwa kwa sasa eda lako litakuwa limekwisha.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akupe subira kwa yaliyo kufika na Akuletee mume mwingine atakaye kuwa kheri kwako.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

Share