Kuhusu Zabuur, Tawraat, Injiyl Na Qur-aan

SWALI:

 

Assalam Aleikum,

 

1- Kitabu cha mwisho kushuka ni Qur´ani cha kwanza kilikuwa Biblia au vipi?

 

2- Nifahamisheni maana ya Taurati, Injili na Zaburi na kazi zake?

 

3- Nini maana ya Agano la kale na Agano Jipya?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Zabuur, Tawraat na Injiyl. Tufahamu kuwa Biblia si kitabu kitakatifu kama wanavyofahamu wengi miongoni mwa Waislamu wa kawaida. Biblia imetokana na neno Biblos, ambalo ni neno la Kigirki lemye maana ya mkusanyiko wa Vitabu. Katika Biblia utapata maneno ya Allaah Aliyetukuka yaliyobaki katika usahihi wake, kauli za Mitume (‘Alayhimus Salaam) na maneno ya watu wasiojulikana. Na yapo maneno mengi yaliyozuliwa ambayo hayawezi kuwa maneno ya Allaah wala Mitume.

 

Kitabu cha kwanza kuteremshwa ni kile alichopewa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam). Allaah Aliyetukuka Anasema:

Suhufi (vitabu) vya Ibraahiym na Muusa” (87: 19).

 

Tawraat ni kitabu alichoteremshiwa Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam) kilichokuwa na amri kumi. Ama Injiyl ni habari njema, nacho ni kitabu alichoteremshiwa na Allaah Aliyetukuka Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) ama maana ya Zabuur ni nyimbo na maombi. Hicho ni kitabu alichoteremshiwa Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam). Kazi za vitabu vyote ambavyo kwa sasa vimepotea katika mfumo wake wa kiasili ni kuwaongoza Bani Israili katika kumjua na kufuata maamrisho ya Allaah Aliyetukuka pamoja na kuwa na maadili mema hapa duniani ili kupata ufanisi Kesho Akhera.

 

Ama maana ya Agano la kale kwa Wakristo ina maana vile vitabu vya kale kabla ya kuja kwa ‘Iysa mwana wa Maryam katika Biblia. Vitabu vyenyewe vinaanza kitabu cha Mwanzo hadi Malaki. Ilhali Agano Jipya ni vitabu vinavyosimulia kuhusu Yesu pamoja na barua ambazo wafuasi Wakristo waliokuwa wakiandikiana. Hivi ni vitabu ambavyo vipo katika Biblia inayofuatwa na Wakristo, hata hivyo Mayahudi hawaiamini Agano hiyo mpya. Vitabu vyenyewe vinaanza kuanzia Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo hadi Ufunuo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share