Mashairi: Deni Lipa Duniani, Akhera Husamehewi

 

  Lipa Deni Duniani, Akhera Husamehewi

     ‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

 

 

Salaam bila kiasi, na zivuke mipakani,

Ninawaomba nafasi, niseme yalo moyoni,

Kukopa kweli "harusi", "matanga" kulipa deni,

Deni lipa duniani, akhera husamehewi.

 

Akhera husamehewi, deni lipa duniani,

Usijifanye kiziwi, ndugu sikia maoni,

Usiseme siambiwi, leo liwe sikioni,

Deni lipa duniani, akhera husamehewi.

 

Kulipa fanya haraka, bado upo maishani,

Huwezi kuliepuka, ukifika kaburini,

Bora wasia kuweka, warithi walipe deni,

Deni lipa duniani, akhera husamehewi.

 

Kama kulipa huwezi, ukaombe samahani,

Mwenye deni hapotezi, haki yake kwa Manani,

Usijifanye mjuzi, majuto huja mwishoni,

Deni lipa duniani, akhera husamehewi.

 

Upo katika hatari, ni kamba hio shingoni,

Usijifanye hodari, kwa kukwepa mitaani,

Usifanye ujeuri, umekopa kwa hisani,

Deni lipa duniani, akhera husamehewi.

 

Sema nae kwa vizuri, akuonee imani,

Akisamehe tayari, umetoka hatarini,

Yeye huko kwa Kahari, atalipwa kwa yakini,

Deni lipa duniani, akhera husamehewi.

 

Kwa Mola wako akhera, ufike mahakamani,

Thawabu watakupora, itapungua mizani,

Utajitia hasara, usiingie peponi,

Deni lipa duniani, akhera husamehewi.

 

 

Na kama huna thawabu, utakua matatani,

Madhambi ya huyo  babu, utayabeba kichwani,

Ya nini yote adhabu, mwisho wake ni motoni,

Deni lipa duniani, akhera husamehewi.

 

Haliswalii jeneza, Mtume wa Rahmani,

Kwanza anawauliza, ana deni nambieni ?

Ukweli wakitangaza, ndipo anapoamini,

Deni lipa duniani, akhera husamehewi.

 

Wako wapi wa zamani, wamekufa wahisani,

Wakati huu jamani, atakulipia nani ?

Watakubwaga shimoni, hapo tena huwaoni,

Deni lipa duniani, akhera husamehewi.

 

Kukopa mali hatari, bora ufe masikini,

Akhera uwe tajiri, huna deni asilani,

Hivyo tujitahadhari, tuwe mbali na madeni,

Deni lipa duniani, akhera husamehewi.

 

Tuombe Mungu sitara, Atusitiri nchini,

Deni kweli ni izara, akhera na ardhini,

Samahani kuwakera, nawaaga kwaherini,

Deni lipa duniani, akhera husamehewi.

  

 

Share